UNAWEZA kuona kama mapema hivi lakini sio kwa Singida Black Stars baada ya kumshusha kocha Hamid Miloud na kumwambia anatakiwa kuhakikisha timu inashiriki michuano ya kimataifa msimu ujao.
Kocha huyo ambaye ametambulishwa rasmi juzi, amewahi kuifundisha Al-Khaldiya FC, USM Alger na JS Kabylie za kwao Algeria, Al-Salmiya ya Kuwait, Athletico Marseille na ES Vitrolles za Ufaransa na Al-Ettifaq FC (U-23) kutoka Saudi Arabia.
Hamdi atafanya kazi na wasaidizi wawili, Nassim Anisse na David Ouma, huku aliyekuwa kaimu kocha mkuu, Ramadhan Nswanzurimo akirejeshwa katika nafasi ya mkurugenzi wa ufundi.
Taarifa za ndani zililiambia Mwanaspoti kuwa, Singida ni timu yenye mastaa wakubwa hivyo hakuna sababu ya kikosi hicho kushuka nafasi iliyopo sasa.
“Kocha ameshaambiwa kabisa msimu ujao malengo ni kushiriki michuano ya CAF, hivyo basi anapoanza kazi na timu anajua kabisa mabosi wanachotaka.
“Imani ya klabu ni kubwa kwa kocha kwani amefundisha timu kubwa hivyo hatakuwa na changamoto sana ya kuwanoa mastaa ili wafikie malengo,” alisema mtu huyo.
Kocha huyo anaichukua timu ikiwa nafasi ya nne kwenye msimamo wa Ligi Kuu Bara ikicheza mechi 16 na kukusanya pointi 33.