2025 ni mwaka wa uchaguzi Afrika

Dar es Salaam. Wakati ulimwengu ukiupokea mwaka mpya 2025, mataifa 10 ya Afrika, ikiwemo Tanzania, yanatarajia kufanya uchaguzi mkuu mwaka huu kuchagua viongozi watakayoyaongoza kwa mujibu wa katiba zao.

Mwaka 2024, mataifa 19 ya Afrika yalifanya uchaguzi mkuu ambapo imeshuhudiwa wagombea wa upinzani wakifanya vizuri kwenye chaguzi zilizofanyika kwenye mataifa kadhaa yakiwamo Senegal, Mauritius na Botswana.

Vilevile, katika mwaka uliopita, vyama vikongwe vilivyotawala kwa muda mrefu vimetikiswa na upinzani, jambo ambalo halikutarajiwa. Mfano wa vyama hivyo ni African National Congress (ANC) cha Afrika Kusini na Botswana Democratic Party (BDP) cha Botswana.

Huko Namibia, mwanamke, Netumbo Nandi-Ndaitwah ameweka rekodi kwa kushinda uchaguzi mkuu kwa kuchaguliwa kuwa rais wa tano wa Jamhuri ya Namibia, akichukua nafasi ya Nangolo Mbumba aliyetwaa wadhifa huo baada ya kifo cha rais wa tatu, Hage Geingob.

Katika uchaguzi wa mwaka huu, Mataifa 10 yatafanya uchaguzi kwa nyakati tofauti zikiwemo nchi zinazoongozwa kijeshi kufuatia mapinduzi yaliyotekelezwa na kuangusha utawala wa kiraia kwenye mataifa hayo.

Tanzania inatarajia kuwa na uchaguzi mkuu Oktoba mwaka huu ambapo vyama 19 vyenye usajili wa kudumu vina fursa sawa ya kusimamisha wagombea wenye sifa kwenye nafasi ya Rais, wabunge na madiwani.

Uchaguzi huo utakuwa wa saba tangu kuanza kwa mfumo wa vyama vingi nchini mwaka 1992. Hata hivyo, uchaguzi uliopita wa 2020 ulikuwa na malalamiko ya ukiukwaji wa sheria na taratibu, jambo lililosababisha wapinzani wengi kuondolewa bungeni.

Nchi nyingine inayotarajiwa kufanya uchaguzi Septemba 16, mwaka huu, ni Malawi ambapo rais wa sasa, Lazarus Chakwera, aliyechaguliwa mwaka 2020 anatarajiwa kugombea tena muhula wake wa pili. Itakumbukwa kwamba Chakwera alimshinda mtangulizi wake, Peter Mutharika kwenye uchaguzi uliopita.

Gabon na Niger, mataifa ya Afrika Magharibi yanayoongozwa kijeshi, pia yatafanya uchaguzi mwaka huu ili kuzipa uhalali serikali zao za kijeshi zilizoingia madarakani kwa njia ya mapinduzi dhidi ya utawala wa kiraia. Gabon itafanya uchaguzi huo Agosti mwaka huu wakati Niger bado tarehe rasmi haijafahamika.

Ali Bongo wa Gabon alipinduliwa na mmoja wa walinzi wake, Brice Nguema, Agosti 2023 wakati huko Niger, Mohamed Bazoum naye alipinduliwa na jeshi la nchi hiyo na Abdourahamane Tchiani kuwa kiongozi wa taifa hilo baada ya mapinduzi ya Julai 2023.

Cameroon itafanya uchaguzi wake Oktoba 2025 ambapo rais Paul Biya ambaye amekuwa madarakani kwa miaka 42 sasa, bado ana nafasi ya kugombea tena kwenye uchaguzi huo dhidi ya upinzani unaokandamizwa.

Ikumbukwe kwamba mwaka 2008, Cameroon iliondoa ukomo wa muda madarakani ili kumruhusu Biya kuendelea kuwa madarakani kwa muhula mwingine wa miaka saba. Biya amekuwa madarakani tangu mwaka 1982.

Kadhalika, Jamhuri ya Afrika ya Kati (CAR) itafanya uchaguzi wa viongozi wa kitaifa. Taifa hilo limekuwa kwenye mapigano ya wenyewe kwa wenyewe ambayo yamekuwa yakikwamisha michakato ya kidemokrasia nchini humo.

Uchaguzi mkuu mwingine wa Rais utafanyika Togo, taifa dogo la Afrika Magharibi. Uchaguzi wa mwaka huu utakuwa wa kwanza tangu yalipofanyika mabadiliko ya katiba kuondoa utaratibu wa wananchi kumchagua rais, bali bunge ndiyo linamchagua kiongozi huyo.

Oktoba 2025, Ivory Coast pia itakuwa na uchaguzi wa rais ambapo rais Alassane Ouattara, aliyeingia madarakani mwaka 2010, anasukumwa na wafuasi wake kugombea tena licha ya kwamba alisema angependa kupumzika. Duru zinaeleza kwamba huenda akagombea tena muhula wake wa nne.

Wakati mataifa mengine yakiwa na uchaguzi, Visiwa vya Shelisheli vitakuwa na uchaguzi mkuu Septemba 27, mwaka huu. Rais Wavel Ramkalawan ambaye aliingia madarakani mwaka 2020, anatarajiwa kugombea tena muhula wa pili.

Related Posts