KIPA wa Kagera Sugar ambaye amejumuishwa kwenye kikosi cha Kilimanjaro Stars kwa ajili ya michuano ya Kombe la Mapinduzi, Ramadhan Chalamanda amesema ataitumia kama daraja kujihakikishia namba katika mashindano mengine.
Pia amesema wakati akijiandaa kisaikolojia kukabiliana na michuano hiyo kwa mara ya kwanza kwake, akili nyingine ipo Ligi Kuu namna ya kuipambania timu yake na aibu ya kushuka daraja.
Kagera Sugar haijawa na matokeo mazuri katika Ligi Kuu Bara msimu huu ambapo imekusanya pointi 11 ikiwa nafasi mbili za chini kwenye msimamo baada ya mechi 15 na kuwa katika presha ya kushuka daraja.
Chalamanda ameliambia Mwanaspoti kuwa anaenda kushiriki Kombe la Mapinduzi kwa hesabu kali kuhakikisha anaonyesha kiwango bora ili kutengeneza mazingira ya kuitwa tena kuitumikia timu ya taifa.
Amesema pamoja na mipango hiyo, akili nyingine ipo kwa timu yake ambayo haipo sehemu nzuri katika Ligi Kuu, hivyo anahitaji kuipambania kubaki salama.
“Nashukuru nimekuwa na mwenendo mzuri, lakini kiwango changu hakiendani na matokeo ya jumla kwa timu, kwa sasa nawaza timu ya Taifa kushiriki Kombe la Mapinduzi kabla ya mengine.
“Lazima nitumie fursa hii kama daraja kuonyesha nilichonacho, ndoto ya kila mchezaji ni kuichezea Taifa lake, baada ya hapo nageuzia hesabu Ligi Kuu kuipigania Kagera Sugar kubaki salama,” alisema kipa huyo.
Nyota huyo ambaye amedumu Kagera Sugar kwa takribani misimu mitano, amekiri ushindani wa namba akieleza kuwa wakati wa mazoezi ndio utaamua benchi la ufundi nani aanze.
Kilimanjaro Stars inashiriki michuano ya Kombe la Mapinduzi itakayoanza Ijumaa wiki hii Kisiwani Pemba kwa kushirikisha timu sita za taifa. Zingine ni wenyeji Zanzibar Heroes, Kenya, Uganda, Burundi na Burkina Faso.