Kina Sanga wa Chadema waachiliwa huru kesi ya mauaji

Njombe. Mahakama Kuu Kanda ya Iringa imewaachia huru wanachama watatu wa Chadema akiwamo aliyekuwa Katibu wa Jimbo la Njombe, George Sanga na wenzake wawili waliokuwa wakituhumiwa kwa mauaji ya kada wa CCM, Emmanuel Mlelwa.

Wengine walioachiliwa huru ni Gooddluck Mfuse na Octatus Mkwela, baada ya Mahakama hiyo kuona hawana hatia.

Katika kesi iliyoendeshwa tangu mwaka 2020, upande wa Jamhuri uliwakilishwa na mawakili Elise James, Cecilia Mkonong’o na Geres Tesha huku mawakili wa upande wa utetezi wakiongozwa na Dickson Matata, Frank Ngafumika, Innocent Kibadu na Neema Msafiri.

Akisoma hukumu hiyo kwa njia ya mtandao mkoani Njombe leo Desemba 31, 2024, Jaji mfawidhi Kanda ya Iringa, Danstan Ndunguru amesema washtakiwa hao wameachiwa huru kutokana na upande wa Jamhuri kushindwa kuthibitisha mashitaka yao.

Amesema ushahidi pekee uliotolewa na mashahidi hao ni wa kimazingira, kwani hakuna ambaye ameona washtakiwa hao wakifanya kosa hilo, hivyo Mahakama kushindwa kujiridhisha kuwa washtakiwa hao wamefanya kosa hilo.

“Ili uweze kuthibitisha ushahidi wa kimazingira lazima ujitosheleze, lakini Jamhuri imeshindwa kuthibitisha,” amesema Jaji Ndunguru.

Amesema sababu nyingine iliyofanya washtakiwa hao kutokuwa na hatia ni baadhi ya mashahidi muhimu akiwamo mkuu wa upelelezi wa mkoa huo kushindwa kufika mahakamani.

Akizungumza baada ya hukumu hiyo, wakili wa utetezi, Dickson Matata amesema kesi hiyo ilikuwa na mashahidi 14 upande wa Jamhuri na watano upande wa utetezi.

Amesema katika kesi hiyo Na.5236 ya mwaka 2020 kati ya mashahidi hao 14 hakuna hata mmoja aliyesema mahakamani kuwa amemuona mmoja kati ya washtakiwa hao akimuua Emmanuel Mlelwa.

“Kwenye kesi hii hakuna mshtakiwa aliyekiri kwa kufuata utaratibu kukiri kulikozungumziwa mahakamani ni kwa shahidi polisi akiwa kwa RCO alimsikia George Sanga akikiri na kuwataja wenzake,” amesema Matata.

Mwenyekiti wa Chadema Kanda ya Nyasa, Joseph Mbilinyi, maarufu Sugu amesema bado kuna kesi nyingine kama hiyo inayowahusu makada wa Chadema wa Kibaha Mkoa wa Pwani.

“Tunaitaka Serikali imalize kesi hizi kwa sababu nchi yenye wafungwa wa kisiasa kwenye mipaka yake huwa haiheshimiki duniani,” amesema Mbilinyi.

Akizungumza kwa niaba ya wenzake,  Sanga amewashukuru Watanzania wote waliokuwa wakiwaombea katika kipindi chote walichokuwa gerezani.

“Sina mengi ya kusema leo, kwani kimsingi naona kama naota lakini kwa niaba ya wenzangu tunamshukuru Mungu kwa kututunza na Watanzania ilikuwa safari ndefu,” amesema Sanga.

Related Posts