Dar es Salaam. Serikali imeeleza kuwa upelelezi wa kesi ya kusafirisha kilo 332 za heroini na methamphetamine inayomkabili mvuvi Ally Ally (28) maarufu kama Kabaisa na wenzake wanane, bado unaendelea.
Wakili wa Serikali Roida Mwakamele ameeleza hayo katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, leo Desemba 31, 2024, wakati kesi hiyo ilipotajwa.
Mwakamele ametoa maelezo hayo, mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi, Godfrey Mhini, kuwa bado wanaendelea na upelelezi, hivyo wanaomba tarehe nyingine kwa ajili ya kutajwa.
Tofauti na siku nyingine kesi hiyo huahirishwa kwa njia ya video, leo washtakiwa hao wamepelekwa mahakamani kwa hati ya wito kutoka mahabusu.
Hakimu Mhini baada ya kusikiliza maelezo ya pande zote aliahirisha kesi hiyo hadi Januari 13, 2025 itakapotajwa.
Washtakiwa wamerudishwa rumande kutokana na kesi inayowakabili haina dhamana.
Mbali na Ally, washtakiwa wengine ni Bilal Hafidhi(31)ambaye ni mfanyabiashara; Mohamed Khamis(47) mvuvi na Idrisa Mbona(33) muuza magari.
Wengine ni Rashid Rashid (24) Beach Boy na mkazi wa Ubungo Maji, Shabega Shabega (24) mbeba mizigo na mkazi wa Saadan Kasulu.
Pia, yupo Dunia Mkambilah (52) ambaye ni mlinzi na mkazi wa Madale Kisauke, mfanyabiashara Mussa Husein (35)mkazi wa Mwambani na Hamis Omary(25).
Katika kesi ya msingi, washtakiwa kwa pamoja wanadaiwa Aprili 16, 2024 karibu na Hotel ya White Sands, iliyopo Wilaya ya Ilala, wanadaiwa kusafirisha kilo 100.83 za dawa aina ya methamphetamine, kinyume cha sheria.
Shtaka la pili, washtakiwa kwa pamoja wanadaiwa kusafirisha kilo 232.69 za heroini, kinyume cha sheria.
Kwa mara ya kwanza, washtakiwa hao walifikishwa mahakamani hapo, Aprili 22, 2024 wakikabiliwa na mashtaka hayo.