iDar es Salaam. Wakati msimu wa wanafunzi kurudi shuleni ukikaribia, jamii imeaswa kuwakumbuka watoto wanaoshi katika mazingira magumu ili wapate vifaa vya shule kama wanavyopata watoto wengine.
Hayo yameelezwa na mfanyabiashara Celine Richard baada ya kuwakabidhi vifaa vya shule watoto hao, waishio katika mazingira magumu leo Manzese Dar es Salaam leo Desemba 31, 2024.
Celine ambaye ni miongoni mwa walezi wa watoto katika Shirika la Macho kwa Jamii amesema watoto yatima na waliopo mazingira magumu wanahitaji madaftari, mabegi kalamu na nguo kama alivyofanya hii leo.
“Watoto wenye mazingira magumu wanapaswa kukaa eneo moja wapate malezi na uangalizi maalumu kwa ajili ya ustawi na ukuaji katika maisha yao,” amesema.
Mkurugenzi wa Shirika la Macho kwa Jamii linalojishughulisha na haki za watoto, Theresia Lihanjala amesema kuna watoto wanaohitaji vifaa vya shule, hivyo anaomba wadau kuwashika mkono.
“Huwa tunaenda shuleni tunakutana na watoto wanaoishi katika mazingira magumu na yatima wasio kuwa na vifaa vya shule. Tumeamua kufanya kila Juni na Desemba kuwapatia vifaa hivyo ili kuwarejeshea tabasamu,” amebainisha.
Amesema wanatamani kuona watu wengine wakiwasaidia watoto hao ambao wako zaidi ya 70 vifaa muhimu zikiwamo nguo, madaftari, mafuta, sabuni ili kuwagusa watoto hao.
Mmoja ya watoto hao aliyejitambulisha kwa jina Moshi amesema anashukuru kwa msaada huo huku akiomba wadau kujitokeza kuwasaidia zaidi.
Naye, Shakila Nantambalele, Mkurugenzi wa Shirika la Nantambalele Niokoe Foundation amesema ni jambo la heri kuwarejeshea watoto tabasamu.
“Nitoe rai kwa Watanzania wenzetu tuunganike tuwasaidie watoto hawa waende shule wakiwa na vifaa vyote. Tukiwa wengi tunaamini tutafanya jambo kubwa zadi ya hapa,” amesema Shakila.