Wananchi Mkuranga wataka ufanisi barabara za ndani

Dar es Salaam. Baadhi ya wakazi wa Mkuranga mkoani Pwani wametaka kuongezwa kasi ya kuboresha ujenzi wa barabara ndani za jimbo upatikanaji wa huduma za afya, umeme, kilimo na elimu ndani ya mwaka 2024.

Hata hivyo, Mbunge wa Mkuranga na Waziri wa Ujenzi, Abdallah Ulega amewatoa wasiwasi kuhusu ujenzi wa barabara hizo, akisema ni miongoni mwa maeneo yatakayoongezewa msukumo ili kuboresha huduma za kijamii wilayani humo.

Wananchi hao walieleza hayo leo Jumanne Desemba 31, 2024 wakati hafla ya kuuga mwaka 2024 na kuukaribisha mwaka mpya 2025, shughuli iliyoandaliwa na mbunge huyo aliyetoa mrejesho wa mafanikio yaliyopatikana mwaka 2024.

Hafla hiyo iliyofanyika uwanja wa Shule ya Msingi Mwandege, ilienda sambamba na ugawaji wa zawadi na vitendea kazi vya ujenzi ikiwamo saruji na fedha taslimu kutoka mfuko wa jimbo hilo.

Mkazi wa Mwandege, Fatuma Khamis  amesema ndani ya mwaka 2024 wanaishukuru Serikali kwa kufanikisha ukarabati na uboreshaji wa hospitali ya Wilaya ya Mkuranga sambamba na ujenzi wa shule mbalimbali zenye viwango kwa sekondari na msingi.

“Hapa Mwandege kulikuwa na sekondari moja sasa hivi zipo sita, fedha nyingi zimeletwa kupitia mfuko wa jimbo na Serikali kuu kwa msukumo wa mbunge wetu,” amesema.

Mariam Masanyila aliungana na Fatuma kuishukuru Serikali kwa ukarabati mkubwa uliofanyika katika hospitali sambamba uboreshaji wa huduma za upatikanaji wa umeme kwenye vijiji vyote 125 vya jimbo hilo, huku akisisitiza ujenzi wa barabara za ndani.

“Katika ukarabati huo tumepata jengo la wagonjwa wa nje ambao hivi sasa wanapata huduma matibabu. Pia, ujenzi wa zahanati na vituo vya afya vimesaidia upatikanaji wa huduma za afya ngazi za chini,” amesema.

Juma Athumani ambaye ni mkulima wa korosho anasema katika kipindi cha mwaka 2024 Serikali imefanikiwa kuwapa viuatilifu kwa wakati kwa ajili ya zao hilo.

“Hatua hii imeongeza tija kubwa kwa wakulima kuzalisha kwa wingi korosho, kama hii haitoshi miaka ya nyuma ulikuwa unazalisha, lakini huna uhakika wa kuuza, mwaka 2024 imekuwa tofauti tumeuza kwa bei ya juu kabisa,” amesema Athumani.

Akitoa mrejesho wa masuala mbalimbali yaliyofanyika ndani ya mwaka 2024, Ulega amewatoa hofu wananchi kuhusu ujenzi wa barabara za ndani, akiwaita watendaji wa Wakala wa Barabara za Mijini na Vijiji (Tarura), Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads), kushirikiana kufanikisha hilo.

Ulega amesema mwaka 2021 wakati Rais Samia anashika madaraka Mkuranga ilikuwa na shule za msingi 114 hivi zimeongezeka hadi 127 zilizojengwa kwa nyakati tofauti ikiwemo mwaka 2024.

“Mwaka 2021 kulikuwa na shule za sekondari 25 leo tunavyoongea kuna shule za sekondari 53 mpya zilizojengwa kwa viwango, tunaishukuru Serikali na Rais Samia, wananchi na viongozi wa CCM kwa kwa hatua hii kazi kubwa imefanyika.

“Niwaambie kulikuwa na shida kubwa ya vivuko, ndani ya mwaka 2024  tumejenga vivuko 11 kila mahali kulipokuwa na mtu tumejenga daraja ili kuunganisha mawasiliano, tutaendelea kuifanya kazi hii kubwa, yajayo yanafurahisha,” amesema Ulega.

Kwa upande wa sekta ya nishati, Ulega amesema hakuna kijiji ndani ya Mkuranga ambacho hakina umeme.

“Tuna kazi ya kubwa mbele yetu ya kusambaza umeme kwenye vitongoji, ndio kazi iliyobaki,” amesema Ulega.

Related Posts