Makamanda wawatolea macho watakaovunja sheria mkesha mwaka mpya

Morogoro/Mwanza/Arusha. Wakati zimesalia saa chache kuumaliza mwaka 2024 na kuingia mwaka mpya wa 2025, makamanda wa polisi wa mikoa, wamepiga marufuku uchomaji moto matairi, kupiga mafataki sambamba ulevi uliopitiliza.

Hayo yamesemwa leo Jumatano Desemba 31, 2024 kwa nyakati tofauti na makamanda wa polisi wa mikoa ya Mwanza, Arusha na Morogoro.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Justine Masejo amesema jeshi hilo limejipanga kuhakikisha watu wanaadhimisha mkesha na Sikukuu ya Mwaka Mpya  2025 kwa amani na utulivu.

Hata hivyo, kamanda huyo amepiga marufuku uchomaji wa matairi, upangaji wa mawe barabarani na kusisitiza wamiliki wa baa na kumbi za starehe kuzingatia masharti ya leseni zao ikiwemo muda wa kufunga na kuepuka msongamano wa watu.

“Wamiliki wa baa na kumbi za starehe wazingatie masharti ya leseni zao ambazo zinaonyesha muda halisi wa kufunga na kuepuka kujaza watu kupita uwezo wa kumbi zao,” amesema.

Akizungumza mbele ya waandishi wa habari mkoani Mwanza, Kamanda wa Polisi Wilbrod Mutafungwa amewataka pia madereva kujiepusha na uendeshaji hatarishi unaoweza  kusababisha ajali, badala yake wazingatie sheria, taratibu na kanuni za usalama barabarani.

“Wajiepusha na unywaji wa pombe uliopitiliza na kuendesha chombo cha moto ukiwa umelewa, naomba washerehekee kwa kiasi kama umekunywa pombe ni vyema usiingie barabarani, la sivyo sheria itachukua mkondo wake,” amesisitiza kamanda Mutafungwa.

Ametoa rai kwa wazazi kutowaruhusu watoto kwenda matembezi au maeneo ya burudani bila kuwa na uangalizi wa watu wazima.

“Endapo familia itawalazimu kwenda kusherehekea sikukuu nje ya mazingira ya nyumba zao, wasiache maeneo yao bila uangalizi lakini pia tunaomba kila mwananchi atii sheria bila shuruti,” amesema.

Kamanda huyo amewaomba wananchi atakaye ona viashiria vyovyote vya kihalifu kutoa taarifa kwa viongozi wa Serikali katika maeneo yao, Jeshi la polisi au vyombo vingine vya ulinzi na usalama.

Naye Kamanda wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Mkoa wa Morogoro, Shabani Marugujo amewaonya wananchi kuacha tabia ya kupiga baruti hovyo, kutumia dawa za mbu na kukimbia nazo barabarani bila tahadhali.

Lakini niwaonye wananchi, tumebakiza muda mfupi sana, tabia ya kuufurahia mwaka kwa  kuchoma moto matairi ya magari barabarani hazileti picha nzuri na ni uvunjaji wa sheria, hivyo ni marufuku kwa usiku wa leo,” amesema Marugujo.

Pamoja na katazo hilo, amewataka wamiliki wa nyumba na kumbi za starehe zikiwamo klabu za usiku kutojaza watu kwenye maeneo hayo kupita kiasi.

“Askari wa Jeshi la Zimamoto na uokoaji tunaendelea kuwa na utayari kwa ajili ya kukabiliana na majanga yoyote yanayoweza kutokea,” amesema.

Naye Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, Alex Mkama amesema ulinzi umeimarishwa kwenye maeneo yote ya Mkoa wa Morogoro.

“Namna tulivyojiandaa hapa mjini ndivyo tumefanya hata huko wilayani, natoa onyo kwa wale wanaopanga kuleta vurugu na kuhatarisha usalama wao na wa watu wengine nawaambia tupo timamu tutawashughulikia,” amesema Kamanda Mkama Mkama huku akipiga marufuku upigaji holela wa fataki isipokuwa kwa wale waliopewa vibali huku akiwataka wamiliki wa nyumba za sterehe kuzingatia sheria za leseni zao za biashara.

Related Posts