Jinsi Maisha yalivyo mchana, usiku Stendi ya Magufuli

Dar es Salaam. Ukiweka kando usafiri unaounganisha maeneo ya ndani na nje ya nchi, Stendi ya Magufuli ni sehemu ambayo wasafiri na wakazi wengine wa Jiji la Dar es Salaam wanaweza kununua bidhaa za mahitaji mbalimbali.

 Stendi hiyo iliyogharimu Sh50.9 bilioni, iliyopo Mbezi Luis, Wilaya ya Ubungo, ilizinduliwa Februari 22, 2021 na hayati Rais John Magufuli.

Mwananchi iliweka kambi ya saa 48 katika stendi hiyo kufuatilia yanayojiri mchana na usiku kama anavyosimulia mwandishi wa makala haya.

Ni ukweli ulio wazi, stendi hii imejengwa kisasa, ikiwa na miundombinu rafiki kwa watu wote, ikizingatia mahitaji ya wenye ulemavu katika baadhi ya majengo.

Si mchana wala usiku, muda wote kumekuwa na makundi ya watu wanaoingia na kutoka.

Alfajiri saa 11:30 nilishuka kituo cha daladala Mbezi Mwisho, nikitokea Ubungo kuelekea stendi ya Magufuli.

Nikiwa kwenye ngazi za daraja kuelekea ilipo stendi, nilivamiwa na wapigadebe, wanawake watano na wanaume wawili, kila mmoja akinadi basi anakofanyia kazi.

“Dada wapi, Tanga, Arusha, Mwanza? Achana nao hao, twende huku kuna usafiri wa kwenda Iringa, Mbeya hadi Tunduma. Sema anti, nikupeleke ofisini kwetu,” ni kauli za wapigadebe, kila mmoja akinivuta niende kwake.

“Kwa nini mnasumbua, imekuwa kero sasa?” niliwaeleza, ndipo mmoja akanijibu:

“Anti, ndiyo tunatafuta maisha hapa, na sisi watoto waende shule.”

Ili kukwepa usumbufu niliwaeleza sisafiri. Bado haikuwa suluhisho, mwingine alisema: “Hata kama unakwenda kuchukua mzigo au kumpokea mgeni, tuambie tukuelekeze, au unaenda kukata tiketi ya kesho?”

Baadaye waliachana nami nikaendelea kushuka ngazi kuelekea stendi. Nilipomaliza kuvuka barabara kuelekea lango kuu la kuingia stendi, nilikutana na wapigadebe wengine wenye sare zenye nembo za kampuni za mabasi.

Wapo walionishika mkono wakitaka niende kwenye ofisi zao kukata tiketi, wengine wakielekeza yalipo mabasi.

Hayo hayakufanyika kwangu pekee, wengi waliokatiza eneo hili iwe wamebeba begi au la, walipata usumbufu wa wapigadebe.

Ili kuingia stendi, unapaswa kulipa Sh300 ndipo upatiwe kadi ya malipo ya Ncard yenye thamani ya fedha hiyo ambayo hutumika mara moja. Ukilipia Ncard ya Sh1,000 utaondoka nayo.

Ndani ya stendi nilikutana na wapigadebe wengine, kila mmoja akitaka nisafiri kwa basi la kampuni anayoipigia debe.

Si wapigadebe pekee, pia nilifuatwa na muuza mikate akaniambia, “Dada mikate hii ya kupeleka nyumbani, chagua unachotaka kula utuungishe ndugu zako asubuhi hii.”

Ilipofika saa 12.45 asubuhi, mabasi mengi yalikuwa yameondoka eneo la maegesho kuanza safari nje ya Dar es Salaam.

“Kufanya kazi hii, unatakiwa kutafuta wadhamini wawili wanaofanya kazi humu ndani, ambao watakusaidia kupata mzigo kwa sababu hawatoi kwa pesa, bali mali kauli. Kisha unaenda kununua fulana Sh15,000 unaanza kazi,” anasema.

Alinielekeza eneo chini ya stendi, ambako kuna mawakala wanaouza mikate, keki na maji.

Kwa mujibu wa Rehema, kazi ya uchuuzi ni ngumu, kikubwa kinachohitajika ni jitihada.

Biashara zilizopo ndani ya maduka ya Stendi ya Magufuli.

Anasema ukipambana kutafuta wateja kwenye mabasi, kwa kutwa moja unaweza kuondoka na kati ya Sh10,000 hadi Sh20,000.

“Hawakatazi kufanya biashara, unaweza kukaa hadi usiku,” anasema mchuuzi mwingine aliyejitambulisha kwa jina la Chuga.

Anasema: “Changamoto ni mgambo, usipovaa sare zinazotakiwa utakuwa kwenye matatizo makubwa. Kitu cha kuzingatia, hakikisha una fulana; hata ikitokea hukuivaa, basi uwe nayo kwenye mfuko. Kinyume cha hapo, utakamatwa utapelekwa kituo cha polisi na kupoteza mali yako.”

Chuga anasema hairuhusiwi kupanga bidhaa chini, na ukifanya hivyo ukabainika zitachukuliwa na mgambo.

Nikiendelea kuzungumza na Chuga, lilisikika tangazo kutoka kwa mtumishi ndani ya stendi akielekeza abiria kwenda kukaa kwenye jengo maalumu kwa ajili yao na si eneo la maegesho ya mabasi.

“Ndugu abiria ambao mmefika usiku au alfajiri, na mnaosubiri kuondoka baadaye, usikae chini eneo la maegesho ya mabasi wala usitoke kwenda pasipojulikana unaposubiri ndugu waje kuwachukua, uliza maofisa wetu wakuelekeze jengo la kupumzikia abiria ghorofa ya kwanza,” ilisikika sauti ya tangazo kwenye vipaza sauti vilivyopo ndani ya stendi.

Mtoa tangazo aliendelea: “Pia huko mtakutana na wajasiriamali wanaotoa huduma mbalimbali.”

Ili kufika huko yakupasa kutoka nje ya eneo la maegesho ya mabasi kupitia lango lililopo jirani na eneo la kuingia stendi.

Kuna namna tatu za kufika eneo la mapumziko la abiria, ama kwa kupanda ngazi, kupita njia maalumu isiyokuwa na ngazi kwa ajili ya watu wenye ulemavu na wasukuma toroli za mizigo au kutumia lifti.

Niliamua kupanda lifti, lakini nilipotaka kubonyeza kitufe nikasikia sauti, “dada haifanyi kazi hiyo, tumia ngazi kama wenzako wengine. Wafuate wale wanaopita kwenye ngazi kule.”

Anasema kijana anayeonekana kuwa mzoefu hapa stendi.

“Sikumbuki iliwashwa lini zaidi ya alipokuja mkuu wa wilaya na sijui kiongozi gani nimemsahau, hapa ni mwendo wa kupanda ngazi tu,” anasema kijana huyo na kuongeza:

“Si lifti pekee, ngazi za umeme ziliwashwa siku tatu kama sijakosea, baada ya hapo walizima hadi leo.”

Ghorofani yaliko mapumziko ya abiria kuna vibanda vingi vya wachuuzi wa bidhaa, zikiwamo viatu, nguo, simu na vifaa vyake, migahawa ya mama na baba lishe na huduma za kifedha.

Katika moja ya maduka ya vifaa vya simu nilizungumza na mchuuzi.

“Huku juu biashara ni ngumu, wateja si wengi maana watu wengi wanaishia kule chini. Hivyo kuna nyakati, tunalazimika kuwa na vitoroli tunapakia bidhaa tunaenda kuuza kule chini,” anasema.

Baadhi ya maeneo ya biashara yalikuwa yamefungwa.

Kwa mujibu wa mchuuzi huyo ambaye hakutaka kutajwa jina, eneo la biashara linapimwa kwa mita za mraba. Lake ni mita nne za mraba na huzilipia Sh100,000 kwa mwezi, sawa na Sh25,000 kwa kila mita moja ya mraba.

Ili kutumia choo unapaswa kulipia Sh200 ambazo inaelezwa ni kwa ajili ya kugharimia usafi. Tiketi zinazotolewa baada ya malipo ni za kielektroniki.

Licha ya kulipia, kuna wakati watumiaji wa huduma hii hupata changamoto ya kukosa maji.

Pia, kwa baadhi ya vyoo miundombinu zikiwamo koki zimeharibika.

Katika eneo la mapumziko usiku nilijumuika na abiria wengine kutazama runinga.

Mmoja wa abiria niliokuwa nimekaa nao aliniuliza:

“Ndugu yangu, nimekuja hapa nimekatiwa tiketi hii ya kawaida, wameniambia ile ya elektroniki nitapewa kesho kwenye basi, ni kweli au nimedanganywa?” Sikuwa na majibu kwake.

Baadhi ya watu walikuwa wamelala kwenye viti vya chuma vilivyopo eneo hili. Hata hivyo, baadaye walielezwa hawapaswi kulala hapa.

Baadaye nikiwa nazunguka niliona ngazi, nilipouliza kwa kuli mmoja alinieleza zinaenda chini ya jengo ambako pia kuna shughuli kadhaa zinazoendelea.

Nilianza kushuka chini, kulikuwa na giza totoro, hakuna taa huku eneo hilo la ngazi likiwa na maji na harufu za mikojo.

Kibanda cha kuuzia nguo kilichopo ndani ya Stendi ya Magufuli.

Nilikutana na mtu niliyemuuliza kuhusu hali hiyo naye alijibu: “Humu ndani kuna vyoo vingi, lakini nyakati za usiku watu wanatumia giza kujisaidia kuepuka malipo ya Sh200 kwa huduma ya choo.”

Nilipofika chini nilikuta eneo la maegesho ya magari madogo. Huku mwanga ni hafifu.

Katika eneo hili nilikutana na mwanamke aliyebeba beseni lenye mikate. Alikuwa akiirejesha kwa wakala iliyobaki.

Katika mazungumzo naye, nilibaini kutokana na mwanga hafifu na maeneo mengine kutokuwa na taa wapo wanaotumia eneo hili kufanya vitendo viovu.

Baadhi ya hivyo ni ngono zinazofanyika kwenye vyoo vilivyopo eneo hili.

Kwa mujibu wa mtoa taaifa niliyezungumza naye, baadhi ya wafanyabiashara ni wahusika wa vitendo hivyo nyakati za usiku.

“Hivyo vitu vipo hapa, mara nyingi asubuhi tunakuta mipira ya kiume (kondomu)” anasema mtoa taarifa.

Oktoba 12, 2023 gazeti hili liliandika habari kuhusu rushwa ya ngono katika stendi hii.

Hii inawahusisha wanaoomba ajira kwenye kampuni za usafirishaji na abiria waliokosa fedha za kujikimu.

Licha ya eneo la maegesho kuwa kubwa lenye uwezo wa kuegeshwa magari 100, ni machache yanayoegeshwa, moja ya changamoto ni watu kutofahamu uwepo wake.

Maeneo mengine yanatumika kuhifadhia mizigo, kushusha mikate na hata kwa malazi usiku kwa wasio na makazi.

“Magari mengi yanaegeshwa kule juu kwa sababu hawaelekezwi huku chini, hivyo ni ngumu kwa mgeni kufahamu kama kuna eneo hili,” anasema Amos, kijana anayefanya shughuli eneo hili.

Anasema wanaoegesha magari hapa ni wafanyabiashara ndani ya stendi ambao huenda asubuhi hadi jioni na wengine wamegeuza sehemu ya kulaza magari kutokana na uwepo wa usalama wa kutosha.

Kituo cha mabasi Magufuli kimekuwa kama vile makazi ya baadhi ya vijana wanaojishughulisha na kazi za kuli.

Wengi wao hulala eneo la maegesho ya magari madogo. Baadhi hutandika mikeka na wengine hulala juu ya toroli zao za kazi. Si hivyo tu, wapo ambao hufua na kuanika nguo katika eneo hilo.

“Si kwamba tumelala, bali tunajiegesha kwa ajili ya kusubiri abiria wanaoingia usiku japo kuna wakati usingizi unatupitia,” anasema kuli aliyejitambulisha kwa jina moja la Salum.

Ukiacha biashara ya chakula inayofanyika kwenye jengo la abiria, wapo mama lishe eneo la maegesho ya mabasi yaendayo kaskazini na Morogoro Vijijini.

Wateja hapa ni makondakta, madereva, abiria, wafanyabiashara wadogo, waosha magari na makuli.

Hapa kumejengwa vibanda vingi vinavyotoa huduma hadi za uuzaji pombe.

Jengo hili ambalo ndilo sura ya Kituo cha Mabasi cha Magufuli lina ofisi kadhaa, zikiwamo za wasimamizi wa kituo, Polisi, Uhamiaji, Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF), sehemu ya kulala wageni (Lodge) na Kituo cha Afya cha Kairuki.

Kuna maduka ya vifaa vya magari, mini-supamaketi, duka la dawa, nguo, mgahawa na huduma za kifedha.

Hata hivyo, katika jengo hili baadhi ya maeneo yako matupu.

Jengo hili sehemu ya juu inatumika kuanikia nguo, kukiwa na tangazo la kutoruhusu mtu asiyehusika kupanda huko. Hata hivyo, bado wapo watu wanaolala kwenye ngazi usiku.

Jengo hili la ghorofa bado halijafungwa lifti, hivyo kuwawia vigumu kupanda wenye changamoto ya kutumia ngazi.

Kwa mwenye usafiri binafsi, anapaswa kulipa Sh500 za tozo ya maegesho anapotoka kituoni.

Teksi zinazoegeshwa hulipa Sh3,000 na bajaji Sh2,000 kwa siku, mabasi hutozwa Sh2,000 kila linapotoka kwenye stendi, huku likilala hapo gharama ni Sh4,000.

Hata hivyo, wapo wanaotozwa tozo hizo lakini hakuna risiti inayotolewa.

“Mara nyingi sichukui risiti, nikifika ninalipia Sh500 naondoka,” anasema dereva wa bodaboda.

Katika ufuatiliaji, Mwananchi imebaini risiti za kielektroniki hutolewa kwa wachache, huku kwa bodaboda na bajaji, hutolewa pale dereva atakapodai.

Eneo la maegesho ya magari madogo pia, kuna watu wanaotoza tozo ya maegesho, hivyo kwa anayetozwa kwa kuingia kituoni pia hutozwa chini.

Mbali ya hayo, baadhi ya wanaotumia huduma za vyoo hawapatiwi risiti.

Kumeibuka pia hoja kwa baadhi ya watumishi kwenye kampuni za usafirishaji, kwamba wenye vituo nje ya stendi ya Magufuli hawatozwi fedha za maegezo wala ukaguzi sawa na wao wanaotumia kituo hicho.

“Serikali inapoteza mapato hapa Magufuli ndiyo maana jengo haliishi. Ukifuatilia kila sehemu hapa stendi unalipia, lakini wenzetu wanaopakia nje ya kituo wanalipa wapi?” alihoji mmoja wa watumishi hao ambaye hakupenda kutajwa jina.

Anasema hivi sasa wakaguzi magari kutoka Jeshi la Polisi hawapelekewi orodha ya abiria wanaosafiri, hivyo ni rahisi baadhi yao kutopewa risiti za kielektroniki na kusababisha kukwepa kodi.

Anadai inapotokea tatizo kama vile ajali huwapigia simu mawakala kutaka majina ya abiria waliosafiri.

Miongoni mwa vituo vya maegesho nje ya stendi hii kipo Shekilango, ambako kwa mujibu wa maelezo ya mmoja wa watumishi, mabasi yanayopita njia ya Bagamoyo hayalipi ushuru isipokuwa yale yatakayoingia stendi ya Magufuli.

“Huku hakuna utaratibu wa kukaguana wala kulipa ushuru, labda kama gari litaingia Mbezi, tofauti na hapo utalipia unakoenda na huko inategemea kama hutaingia stendi kuu hakuna malipo,” anasema mtumishi huyo (jina limehifadhiwa).

Meneja wa kituo hicho, Isihaka Waziri akizungumza kwenye mkutano na wadau wanaofanya kazi katika stendi hiyo Machi, 2024 alisema ujenzi wa stendi umekamilika kwa asilimia 97, lakini kwa sasa umesimama baada ya mkandarasi kuondoka kwa kutolipwa kwa wakati. Mkandarasi ni Kampuni ya Hainan International Limited ya China. Amesema kuelekea bajeti ya 2024/25 Halmashauri ya Ubungo imetenga Sh3.2 bilioni kutoka kwenye mapato ya ndani kwa ajili ya kuendeleza ujenzi.

Maeneo ambayo ujenzi haujakamilika amesema ni maegesho ya magari ambako sasa wako wafanyabiashara.

Akizungumzia mapato yanayokusanywa kwa njia ya kielektroniki, anasema yameongezeka kutoka Sh3 milioni hadi kufikia Sh5 milioni.

Hata hivyo, anasema mabasi kutoingia ndani ya kituo kunashusha mapato, pamoja na kutokamilika kwa baadhi ya majengo ya biashara na wafanyabiashara kushindwa kumudu gharama za upangishaji.

Meneja huyo anabainisha kwa siku wamekuwa wakipoteza mapato ya Sh6 milioni.

Serikali inatarajia kukusanya Sh10 bilioni kwa mwaka pindi ujenzi utakapokamilika.

Kwa mujibu wa taarifa, wakati wa uwekaji jiwe la msingi la ujenzi wa stendi hiyo, ujenzi ungegharimu Sh71 bilioni, ikiwa ni pamoja na daraja la kuingia kituoni.

Stendi itakapokamilika itakuwa na uwezo wa kuhudumia mabasi ya abiria 1,000 na teksi 280 kwa siku, pia kutakuwa na maeneo ya bodaboda, bajaji na mama na baba lishe.

Mkuu wa Wilaya ya Ubungo, Hassan Bomboko akiwa katika ziara kituoni hapo Machi 28, 2024 aliagiza mabasi yote kuingia katika stendi hiyo wakati wa kutoka na kuingia mkoani Dar es Salaam.

Amesema kutoingia kwa mabasi kituoni hapo kunasababisha upotevu wa mapato ya Sh700 milioni kwa mwezi, hivyo kwa mwaka Halmashauri ya Ubungo inapoteza Sh2 bilioni.

“Mabasi yote yanapaswa kuanza safari na kushusha abiria kwenye stendi hii, nimezungumza na wapangaji wamesema walichopangisha ni ofisi na si stendi, Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri Ardhini (Latra) nao wanasema vibali vilivyotolewa vimemalizika tangu Septemba, 2023,” amesema Bomboko.

Related Posts