Dar/mikoani. Tunasonga mbele, ndiyo ujumbe unaobeba nasaha za jumla za viongozi wa kiroho katika ibada za mkesha wa mwaka mpya 2025 na kusahau mabaya yaliyopita.
Kwa mujibu wa viongozi hao wa dini, wananchi hawapaswi kuuanza mwaka 2025 kwa kukumbuka changamoto, mabaya na madhila yaliyowatokea mwaka jana, wanapaswa kuganga yajayo kwa kuruhusu faraja ya mwaka mpya.
Ibada hizo za mkesha wa mwaka mpya ziliwakusanya maelfu ya waumini katika makanisa na viwanja mbalimbali zilikofanyika, huku suala la uchaguzi wa haki likiwa moja ya nasaha za viongozi hao wa dini.
Miongoni mwa viongozi hao wa kiroho waliotoa wito wa kusonga mbele, ni Mchungaji Kiongozi wa Kanisa la Kanisa la TAG City Christian Center Upanga, Dk Lucas Shallua amewataka waumini wa kanisa hilo wasijikumbushe mabaya ya mwaka 2024.
Kwa mujibu wa mchungaji huyo, hawapaswi kuwa na kumbukumbu mbaya kwa sababu mwaka mpya 2025 unakwenda kuwafariji.
Katika mahubiri yake wakati wa mkesha wa mwaka mpya kanisani humo, Dk Shallua amesema Mungu anakwenda kutenda mambo mapya mwaka 2025, hivyo mabaya yaliyotokea 2024 hayapaswi kukumbukwa.
“Using’ang’anie ya zamani ya kale yamepita tazama mapya ukisoma Mathayo 6:34 inasema majira na wakati usiogope kuhusu kesho yako utajisimamia mwenyewe hivyo acha kuwaza mambo yaliyotokea mwaka 2024 unatakiwa kusonga mbele,” amesema.
Katika hilo, amesisitiza ni muhimu wa kusimama kiroho na kiimani ili kwenda mbali zaidi, huku akiwanasihi kuacha kukimbilia kwenye makanisa yanayotangaza miujiza.
Wito wa kusonga mbele umetolewa pia na Askofu Mkuu wa Kanisa Katoliki Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Jude Thaddeus Ruwa’ichi, huku akirejea mambo yasiyojenga amani, upendo, mshikamano, haki na ukweli ya mwaka 2024.
Kwa sababu mambo hayo (hakuyataja) hayaleti ustawi wa Taifa, bali yanahatarisha, amewataka Watanzania wasiyashabikie.
Kauli ya kusonga mbele pia, ameielekeza kuelekea uchaguzi mkuu wa mwaka huu, akitaka wananchi waliombee taifa ili usifanyike kwa mazoea na kutozingatia haki.
“Tunaposali tuombee dunia, tunajua dunia imepitia wakati gani, yapo maeneo yamepitia dhuluma na umwagaji damu tunamuomba Mungu ahurumie maeneo yenye vita na umwagaji damu, japo hata kwetu mambo si shwari.
“Mwaka huu ni wa uchaguzi tuombee nchi yetu uchaguzi usifanyike kwa mazoea, kwa hila au namna yeyote isiyo ya haki isiyojali ustawi wa maendeleo ya Taifa letu,” amesema.
Katika mkesha huo ndani ya Kanisa la Kiinjili la Kilutheri (KKKT), Usharika wa Kijitonyama Mchungaji kiongozi, Eliona Kimaro amesisitiza umuhimu wa kuombea uchaguzi.
Amesema Tanzania ndio tumaini pekee la siasa safi lililobakia barani Afrika, hivyo ni muhimu kuilinda heshima hiyo na kufanya uchaguzi kwa haki na amani.
“Tuendelee kutunza heshima ya kisiasa ya Tanzania ni tumaini kwa Afrika na hakuna nchi inayojua siasa zaidi yake na ikisheki kidogo Afrika pia itasheki,” amesema.
Kwa kuwa Tanzania ni moja ya nchi zenye utalii wa siasa kwa kuwa imetumika kuwafunza viongozi mbalimbali akiwemo Rais wa Uganda, Yoweri Museveni, amesema ni muhimu kutunza heshima hiyo.
“Watu walikuwa wanakuja kujifunza siasa hapa Tanzania. Tanzania ndio nchi yenye siasa safi iliyoasisiwa na Mwalimu Nyerere,” amesema.
Kwa upande wa Kiongozi wa Kanisa la Arise and Shine (Inuka Uangaze), Mtume Boniface Mwamposa ametaka watu waenende kulingana na neema walizopewa, wasijishushe iwapo wameinuliwa.
Mmkesha huo ulifanyika katika viwanja vya Tanganyika Packers, Kawe, jijini Dar es Salaam na kupewa jina la “Vuka na Chako.”
“Wale wanaosema siwezi nipo chini usijihesabie katika kiwango cha chini usijihesabie chini bali jihesabie juu kwa imani unasema Mungu amenifanyia mambo mengi mwaka huu piga mara 12,” amesema.
Katika ibada ya mkesha wa mwaka mpya iliyofanyika Kanisa la Kiinjili la Kilutheri (KKKT) Azania Front jijini Dar es Salaam na kuongozwa na Msaidizi wa Askofu na Dean wa kanisa hilo, Mchungaji Chidiel Rwiza, Watanzania wanatakiwa kumshukuru Mungu kwa mambo ambayo hayaelezeki.
Amesema wengi humshukuru Mungu kwa yale wanayoyaona, lakini ukweli ni kwamba kuna makubwa zaidi yanayotendeka kwenye maisha na hayaelezeki.
Amesema katika kipindi cha mwaka kuna watu wengi wamepoteza maisha, kupata majeraha na kadhia mbalimbali hivyo kwa waliobahatika kuwa hai hadi sasa wana kila sababu ya kumshukuru Mungu.
“Inawezekana tunamshukuru Mungu kwa vile ambavyo tunavipima na kuviona vimefanyija kwenye maisha yetu ila kuna yale ambayo hayaelezeki.
Ukimaliza ngazi ya elimu utasherehekea, ukipata mtoto utamshukuru Mungu kwa hilo lakini umewahi kufikiria kushukuru kwa yale ambayo huna uwezo nayo, lakini yanatendeka kwenye maisha yako,” amesema mchungaji Chidiel.
Mchungaji wa Kanisa Anglikana Mtakatifu Gabriel, Kibaha Pwani, Exavia Mpmbichile amehamasisha waumini wake kuanza mwaka mpya wakiwa na malengo mahususi ya maendeleo, hasa katika sekta ya kiuchumi.
Katika mafundisho yake, alielezea mafanikio yanahitaji juhudi za makusudi, akitaja nidhamu ya matumizi ya fedha kama kiungo muhimu cha kufikia malengo.
“Mafanikio hayaji kwa njia ya miujiza, bali yanapatikana kwa kufanya kazi kwa bidii na kuweka malengo madhubuti. Pia, lazima kuwa na nidhamu ya matumizi ya fedha unazozipata,” amesisitiza.
Mpambichile amesisitiza umuhimu wa kuwa na malengo ya kununua viwanja na kujenga nyumba za kuishi kama njia ya kujijengea mustakabali bora wa maisha.
Katika mahubiri yake, mchungaji huyo amesema mafanikio yanahitaji juhudi za makusudi.
Aidha, amewahimiza waumini kuwekeza katika biashara halali na kutumia muda wao katika shughuli za uzalishaji mali badala ya kupoteza muda katika mambo yasiyo na tija.
“Anza mwaka mpya kwa kuweka malengo. Usikubali kukaa kwenye nyumba za kupanga miaka yote, nunua hata kipande kidogo cha ardhi na uanze ujenzi hatua kwa hatua. Safari ya mafanikio ni ya hatua moja baada ya nyingine,” amesema.
Pia amekazia umuhimu wa kuwa na nidhamu ya lugha na kauli njema kwa watu wengine, akisema ni msingi wa mafanikio katika maisha ya kila siku.
“Kauli njema huleta amani na mafanikio. Tukitumia lugha nzuri, tutavutia fadhila na kushirikiana vyema katika safari ya maisha,” amesema.
Ametoa wito pia kwa wazazi kuimarisha mshikamano na kuongeza upendo ndani ya familia zao ili kujenga msingi wa kuishi kwa kufuata maadili.
“Familia zenye mshikamano, umoja, upendo na kumcha Mungu, zina uwezo wa kutatua changamoto na kufanikisha malengo yao kwa pamoja,” amesema.
Imeandikwa na Pamela Chilongola, Baraka Loshilaa, Glorian Sulle, Devotha Kihwelo, Elizabeth Edward na Sanjito Msafiri