Sababu bidhaa za Tanzania kununuliwa zaidi nje ya nchi

Biashara ya kuvuka mipaka imeendelea kuimarika wakati ambao Tanzania imeendelea kuuza zaidi kuliko inavyonunua bidhaa za nje, Ripoti ya Uchumi wa Kikanda ya Benki Kuu ya Tanzania (BoT) inaeleza.

Wakati biashara hiyo ikikua, Chama cha Wamiliki wa Malori Tanzania (Tatoa) kimetaka jitihada zaidi katika kupunguza misongamano ya magari mipakani, hasa Tunduma ili kuongeza ufanisi wa upelekaji bidhaa nchi jirani.

Ripoti hiyo ya BoT inayoakisi mwaka wa fedha 2023/2024 inaonyesha kuwa uuzaji wa bidhaa za Tanzania katika masoko ya nje kupitia mipaka mbalimbali uliongezeka kwa asilimia 13.96 kati ya mwaka 2020/2021 hadi mwaka 2023/2024.

Hiyo ikiwa na maana kuwa bidhaa za Sh9.25 trilioni ziliuzwa nje kupitia mipaka hiyo, kiwango ambacho kiliongezeka hadi kufikia Sh10.54 trilioni mwaka 2023/2024.

Hata hivyo, wakati uuzaji wa bidhaa za Tanzania ukiendelea kuongezeka kidogo kidogo, uingizaji bidhaa kwa kipindi hicho uliongezeka kwa zaidi ya asilimia 80 katika kipindi hicho.

Bidhaa za thamani ya Sh3.23 trilioni ziliingizwa nchini mwaka 2020/2021 na ziliongezeka hadi kufikia Sh6.06 trilioni mwaka 2023/2024.

Akizungumzia suala hilo, Makamu Mwenyekiti wa Tatoa, Rahim Dossa anasema kama wasafirishaji, wameshuhudia ukuaji wa biashara, hasa inayokwenda Zambia na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), lakini foleni kubwa iliyopo mipakani, ikiwemo Tunduma imekuwa ikiwapa tabu.

Anasema kufuatia foleni hiyo, magari yamekuwa yakilazimika kusubiri kati ya siku saba hadi 10 kabla ya kuvuka upande wa pili, jambo linalofanya usafirishaji wa mizigo kwenda polepole.

“Kinachofanyika sasa, magari yanavuka kwa awamu, kama leo litavuka kontena, kesho litavuka tenki la mafuta…Hii ni changamoto katika mzunguko wa usafirishaji, kwani muda mwingi tunautumia mipakani,” anasema Dossa.

Anasema Serikali ya Tanzania kwa upande wake imejitahidi kuhakikisha inafanya kila liwezekanalo huduma zinaboreshwa, ili kuondoa foleni iliyopo katika mpaka wa Tunduma, lakini changamoto ipo upande wa pili.

“Kwa foleni ya Tunduma, changamoto ni upande wa pili, imefikia hatua hadi Tanzania imewapa scanner ili foleni iishe, lakini bado. Tunaiomba Serikali iweke msisitizo mkubwa kuhusu foleni hii ili kuweka urahisi kwetu sisi wasafirishaji bidhaa iwe rahisi kuvuka kushusha mzigo na kurudi kuchukua mzigo mwingine,” anasema.

Katika hili, Waziri wa Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa anasema kwa upande wa Tanzania wameshughulikia vikwazo vilivyokuwapo na sasa wameunganisha nguvu ili kutatua changamoto zilizopo upande wa pili.

“Upande wa Tanzania hakuna tatizo, nafikiri shida ipo upande wa pili, kwetu tumepiga hatua, kwani awali tulikuwa tukikaa wiki mbili hadi tatu, hivyo sasa tunafanya kazi na wenzetu ambapo nahisi taratibu zao, ikiwemo scanner bado hazifanyi vizuri, ila tunaendelea kushirikiana nao kuhakikisha tunapata ufumbuzi,” anasema Profesa Mbarawa.

Mbali na hilo, Profesa Mbarawa anasema huenda treni ya Zambia kuja Tanzania ingekuwa inafanya kazi ipasavyo ingesaidia kuondoa changamoto hiyo ya mizigo inayokwama mipakani.

“Ndiyo maana tunataka kufufua reli ya Tazara, kwa mfano treni hii ikichukua tani milioni tano za mizigo, yaani kwenda tani milioni 2.5 na kurudi tani milioni 2.5 itasaidia kuondoa hii kadhia ya kuchelewa kwa bidhaa katika mpaka wa Tunduma,” anasema Profesa Mbarawa.

Anasema katika kufufua reli hiyo mambo mengi yanafanyika, ikiwemo kuwepo kwa ushirikiano kati ya Serikali ya Tanzania na Serikali ya Watu wa Jamhuri ya China ili kuhakikisha utendaji wake unaimarika kuliko ilivyo sasa.

“Tunaamini kama reli hii itafanya kazi hata ajali zitapungua, itapunguza sana kuharibika kwa barabara na Serikali inafanya haya yote ili kuhakikisha kuwa mipaka na biashara zinazofanyika huko zinakuwa salama,” anasema Profesa Mbarawa.

Kuhusu ushirikiano na China kufufua reli hiyo, takriban Dola bilioni moja za Marekani (zaidi ya Sh2.5 trilioni), zinatarajiwa kutumika kwa ajili ya matengenezo ya reli ya Tazara, yenye umri wa karibu miongo mitano sasa.

Taarifa kuhusu gharama za maboresho ya reli hiyo, ilitolewa na Balozi wa China nchini Zambia, Du Xiaohui Februari 8.

Reli hiyo inayounganisha bandari ya Dar es Salaam kwa upande wa Mashariki na Mji wa Kapiri Mposhi nchini Zambia, ni miongoni mwa miradi mikubwa ambayo China ilifadhili ujenzi wake uliokamilika mwaka 1975.

Mbali na China ambayo imeweka bayana kufufua reli hii, pia Machi 20, 2024, kampuni binafsi ya Bravo iliingia makubaliano na Tazara yanayohusisha kuingiza treni mbili za mizigo zenye mabehewa 20 kila moja ambapo kila behewa litakuwa na uwezo wa kubeba mzigo wa tani 50 (sawa na malori mawili).

Makubaliano hayo na Bravo yalifanyika ikiwa ni miezi mitano baada ya Rais Samia Suluhu Hassan kufanya ziara ya kimkakati nchini Zambia na miongoni mwa mambo yaliyozungumziwa, ni kuifanyia maboresho reli hiyo ili kuongeza kiwango cha mizigo kinachosafirishwa katika reli hiyo.

Reli hiyo yenye urefu wa kilomita 1,860, ikianza kazi yake mwaka 1976, ilikusudiwa iwe na uwezo wa kusafirisha mizigo tani milioni tano kwa mwaka, lakini hadi Juni mwaka jana ilielezwa ilikuwa ikisafirisha chini ya tani milioni moja.

Mhadhiri Mwandamizi Chuo Kikuu Huria Tanzania (OUT), Dk Lawi Yohana anasema biashara hizo zinaweza kustawi zaidi ikiwa nchi itaongeza uzalisha na utoaji huduma ili kupata bidhaa nyingi zinazokwenda nje ya nchi ambayo ni muhimu katika kukuza uchumi wa nchi.

“Tuwe na urari wa biashara mzuri na inakuwa ni vema zaidi kama tutauza zaidi kuliko kuingiza. Japo kuna kuimarika, lakini ni vizuri kuangalia maeneo yenye manufaa zaidi yanayoweza kutubeba,” anasema Dk Lawi.

Miongoni mwa maeneo hayo ni kilimo, ikiwemo cha mbogamboga na matunda ambacho bado hakijafanyika kiasi cha kutosha ili kukidhi mahitaji ya masoko yaliyopo katika nchi za Ulaya.

“Wenzetu Kenya wanafanya vizuri na wakati mwingine wanatumia mazao yetu ya kilimo kuuza nje na hii inawapa fedha nyingi, uuzaji wao wa mazao nje ya nchi unakua, lakini mazao ni ya Tanzania,” anasema Dk Lawi.

Mbali na mazao, eneo lingine linaloweza kuleta fedha nyingine ni mifugo, kwani kama nchi ina mifugo mingi, lakini bado haina viwanda vya nyama na ngozi.

“Tupunguze uingizaji wa bidhaa kwa kujenga viwanda zaidi kwa kuangalia maeneo ambayo tunaingiza zaidi. Eneo la kwanza ni bidhaa za petroli ambazo zinatumia fedha nyingi ambalo linaweza kupunguzwa kwa gesi asilia nyingi, hivyo ni vyema jitihada za kimkakati zifanyike ili vifaa vyetu, mashine na magari zitumie gesi,” anasema na kuongeza:

“Kuwe na juhudi za kisera kwa kuweka unafuu wa kodi kwa magari yanayoingizwa nchini yakiwa na mfumo wa gesi, jambo ambalo litachochea ukuaji wa uchumi wa ndani.

“Tunapoagiza zaidi nje tunaimarisha uchumi wa mataifa mengine, lakini tukiuza zaidi nje tunatengeneza ajira za ndani. Tungependa kuona vituo vya kujaza gesi kwenye magari vinapewa kipaumbele na upendeleo ili vijengwa kwa wingi kama ilivyokuwa kwa vile vya mafuta. Tunaweza kupunguza matumizi ya dola kwa kupunguza utegemezi wa petroli kutoka nje,” anasema Dk Lawi.

Anasema kama nchi, inayo nafasi ya kukuza matumizi ya gesi asilia wakati ambao dunia inahamasisha matumizi ya nishati safi, huku ikiwa mbioni kukomesha matumizi ya mafuta.

Related Posts