Dili la Fountain Gate lamtega Kapama

LICHA ya kutajwa kumalizana na Fountain Gate (FOG), kiungo wa zamani wa Simba, Nassoro Kapama huenda akakutana na rungu la kufungiwa baada ya kudaiwa kusaini mkataba na timu hiyo akiwa bado ana mkataba na Kagera Sugar.

Kapama alirudi katika klabu ya zamani ya Kagera kwa mkataba wa mwaka mmoja na kuitumikia kwa miezi sita baada ya kumaliza mkataba na Mtibwa Sugar iliyoshuka daraja.

Chanzo cha kuaminika kutoka ndani ya Kagera, kimeliambia Mwanaspoti Kapama bado ni mchezaji wao na hawana mpango wa kumuachia kwenda popote dirisha hili la usajili.

“Hatuna taarifa yoyote juu ya mauzo ya Kapama bado ni mchezaji wetu hadi mwisho wa msimu japo hairuhusiwi kufanya mazungumzo na timu nyingine lakini sisi bado tunamuhitaji kutokana na uzoefu wake,” kilisema chanzo hicho na kuongeza;

“Timu haipo kwenye nafasi nzuri tunapambana kuhakikisha inakuwa sehemu ya timu zitakazoshiriki ligi msimu ujao hatuwezi kuruhusu wachezaji waondoke zaidi tunaongeza nguvu ili tujihakikishie nafasi ya kubaki.”

Mwanaspoti lilijaribu kumtafuta Kapama ili kutoa ufafanuzi juu ya tuhuma hizo za kusajili FOG huku akiwa na mkataba wa Kagera, lakini simu ilikuwa ikiita bila kupokewa.

Mbali na Kapama anayehusishwa kumalizana na Fountain akifanya mazoezi na timu hiyo kwa siku mbili, timu hiyo tayari imewatambulisha Said Mbatty na Faria Ondongo waliotokea Tabora United, Jackson Shiga (Coastal Union), Mtenje Albano (Dodoma Jiji), Jimmyson Mwanuke (Singida Black Stars) na winga, Kassim Haruna ‘Tiote’.

Related Posts