Wakati Serikali ikitangaza kuanza kwa biashara saa 24 katika Soko Kuu la Kariakoo, wafanyabiashara na wachumi wamesema hiyo ni fursa kuongeza mapato kwa Serikali na wafanyabiashara na pia kuvutia wateja ndani na nje ya nchi.
Hata hivyo, wamesema suala la usalama kwa wateja na wafanyabiashara linapaswa kuimarishwa kuondoa hofu kwa wageni kuingia nchini kufanya manunuzi ndani ya soko hilo.
“Sijajua ni tarehe ngapi, inaweza kuwa Januari 10 au 15, lakini mpaka sasa tuko kwenye mchakato wa kukamilisha hilo, ambacho kinafanyika ni kuweka mazingira rafiki ili kuanza kufanya kazi kwa saa 24 ikiwamo kufunga kamera,” anasema Mwenyekiti wa Wafanyabiashara Soko la Kariakoo, Severin Mushi.
Taarifa ya soko la kimataifa Kariakoo kufanya kazi saa 24 zilitangazwa Desemba 23, 2024 na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila wakati akitoa salamu za sikukuu za Krismasi na Mwaka Mpya kwa wakazi wa Mkoa wa Dar es Salaam na Watanzania.
Katika salamu zake, Chalamila alisema jiji hilo linajiandaa kufanya biashara kwa saa 24 na kamati maalumu imeshaundwa kusimamia jambo hilo.
“Kuanzia Januari 2025 tutafanya sherehe kubwa ya kuzindua rasmi utaratibu wa kufanya wa biashara kwa saa 24. Tutawataka kila Mkuu wa Wilaya, Mkurugenzi, kuanzisha eneo litakalotakiwa kufanya biashara saa 24, wananchi wafanye biashara kwa saa 24.
“Upande wa Kariakoo tumeanza mchakato wa kununua kamera, na tutaanza mchakato wa kununua baadhi ya vifaa vitakavyosaidia ikiwemo taa, tayari tumekaa na wamiliki wa mabenki na taasisi nyingine ili mchakato wa kufungua biashara saa 24 uwe rasmi.”
Chalamila anasema kuna baadhi ya sheria zinakinzana katika Jiji la Dar es Salaam kuwa baadhi ya biashara zifungwe saa sita usiku.
“Sasa utaratibu huo kwa Dar es Salaam, tunaanza kukomesha taratibu, kwa sababu mkoa huu, una miundombinu inayoruhusu kufanya biashara saa 24,” anasema.
Matarajio ya wafanyabiashara
Mfanyabiashara Soko la Kariakoo, Amani Munuo anasema kuanza biashara kwa saa 24 ni fursa kwao kwa kuwa soko hilo ni la kimataifa na linapokea wageni ndani na nje ya nchi.
“Wageni wanaokuja watafanya manunuzi kwa wakati na kurudi kwa wakati, kwenye suala la usalama, Serikali inapaswa kuwa makini, lakini kama biashara itafanyika kwa saa 24 ni muhimu taasisi za kifedha kama benki na mitandao mingine ifanye kazi kwa saa 24,” anasema.
Mfumo huo wa biashara saa 24, Munuo anasema utakuwa na faida kwa wafanyabiashara kuongeza kipato na Serikali kupata fedha nyingi zaidi.
Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wafanyabiashara Tanzania (JWT), Khamisi Livembe anasema Soko la Kariakoo kufanya kazi kwa saa 24 itakuwa nafuu kwa wafanyabiashara wa mikoani ambao hufika kufanya manunuzi katika soko hilo.
“Hii maana yake wafanyabiashara watanunua mzigo na kufungasha usiku, asubuhi wanaondoka, kwa hiyo utoaji huduma kwa saa 24 utapanua wigo wa utoaji huduma,” anasema.
Pamoja na faida ya kuongeza kipato cha wafanyabiashara, Livembe anasema kinachosababisha watu kutofanya biashara hiyo saa 24 ni hofu ya usalama.
Anasema mikoa mingine biashara hufanyika hadi saa nne, lakini inashindikana baadhi ya maeneo kutokana na usalama nyakati za usiku kuwa mdogo.
“Tamko la wafanyabiashara kufanya kazi saa 24 aliwahi kutoa aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda baada ya kukutana na wafanyabiashara, ni taribani miaka minane sasa imepita, kwa mantiki hiyo Serikali imejipanga na usalama hadi wakalisema tena,” anasema.
Katika hilo, anatolea mfano kuanza safari za usiku kwa mabasi, akisema kuna wakati hayakuwa yakisafiri kutokana na usalama kuwa mdogo, lakini baada ya Serikali kujipanga imeruhusu mabasi kutembea saa 24.
Livembe anasema suala la usalama kwa biashara kufanyika saa 24 ni mpana, kwani utahusisha usalama wa mnunuzi na muuzaji yeyote kati yao kutopata changamoto, kwani chochote kitakachotishia usalama wao utadhihirishwa na utaratibu huo.
“Tukifikia hapo suala la usalama lisiwe shida, watu wanunue bidhaa zao na kusafirisha bila changamoto, ila naipongeza Serikali kwa hatua hiyo, kila kitu ni uthubutu, hata kama kuna changamoto zitakazojitokeza zitashughulikiwa,” anasema.
Akizungumza na Mwananchi kuhusu ulinzi na usalama, Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu Dar es Salaam, Muliro Jumanne anasema jeshi hilo limeshajiandaa tangu mwaka 2023 kusimamia usalama biashara kufanyika saa 24.
“Siku nyingi tumejipanga ndiyo maana unaona Kariakoo ipo shwari, polisi imeshajipanga kuimarisha ulinzi na usalama kijamii, kiuchumi na kisiasa. Tumeshaanda mazingira na kufanya maandalizi kuhusu suala hili,” anasema Kamanda Muliro.
Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Kariakoo Magharibi, Said Omary anasema wamejipanga vizuri kutoa ulinzi na usalama, kwa kuimarisha vikosi vyao vya ulinzi shirikishi kwa ushirikiano na wafanyabiashara ili kuleta ustawi.
“Tutakaa na wafanyabiashara kuangalia namna bora ya kubadilisha fedha kwa mitandao badala ya kutumia fedha taslimu. Tumeshaanza kufanya nao kikao, baada ya wao kutoka kikao cha mkuu wa mkoa,” anasema Omary.
Wakati hili likitarajiwa kuanza hivi karibuni, mwaka 2024 hautasahaulika kwa wafanyabiashara wa Kariakoo kufuatia matukio mbalimbali yaliyoshuhudiwa.
Juni, mwaka huu, biashara Kariakoo zilisimama kufuatia mgomo wa wafanyabiashara ambao baadaye ulichukua sura ya kitaifa.
Wafanyabiashara walifunga maduka kupinga taratibu za mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), hususan kamatakamata ya risiti za kodi za kielektroniki (EFD) na faini kubwa zisizolingana na hali halisi ya biashara zao.
Mgomo huo ulianza Kariakoo, lakini baadaye ulienea katika mikoa mingine ya Arusha, Morogoro, Kagera, Dodoma, Mbeya, Iringa, Ruvuma, Mwanza na Mtwara, hali iliyosababisha Serikali kusimamisha ukaguzi na kuahidi marekebisho ya sera za kodi.
Novemba 16, 2024, Kariakoo ilikumbwa na msiba mwingine baada ya jengo la ghorofa kuporomoka ghafla, lililosababisha vifo vya watu 31 na majeruhi 86 na kuharibu mali za wafanyabiashara.
Kutokana na tukio hilo, ilibidi baadhi ya maduka na mitaa kufungwa kwa ajili ya kurahisisha utendaji kazi katika uokoaji na kuondoa vifusi katika jengo lililoporomoka.
Tukio lingine ni la Oktoba 30, 2024 baada ya moto kuzuka na kuteketeza maduka na nyumba Mtaa wa Kipata, Kariakoo jijini Dar es Salaam.