AKILI ZA KIJIWENI: Mara wameamua kuishusha Biashara Utd

WIKI iliyopita ambayo ilikuwa ya mwisho kwa mwaka 2024, haikumalizika vizuri kwa mkoa wa Mara baada ya kamati ya usimamizi na uendeshaji wa ligi ya Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB) kutoa uamuzi ambao ni wa maumivu kwa mkoa huo.

Uamuzi huo ni wa kuipoka pointi 15 timu ya Biashara United ya mkoani humo inayoshiriki ligi ya Championship baada ya kushindwa kutokea uwanjani katika mechi dhidi ya Mbeya City, Desemba Mosi, 2024.

Kutokana na adhabu hiyo, Biashara United imeporomoka kwenye msimamo wa Championship kutoka nafasi ya 11 iliyokuwepo mwanzoni hadi nafasi ya mwisho kwenye msimamo wa Championship.

Uchunguzi wa kiandamizi tulioufanya hapa kijiweni umegundua kwamba sababu ya Biashara United kushindwa kwenda Mbeya kucheza mechi hiyo ni hali ngumu ya kifedha ambayo imeikumba timu hiyo.

Biashara United ina viongozi ambao ni watu wa mpira hasa na katika hali ya kawaida hawawezi kuamua kutopeleka timu uwanjani hivyo hadi ukiona timu haijasafiri basi wamejitahidi kwa kadri ya uwezo wao lakini maji yakazidi unga.

Kwa sasa hesabu zimeshakuwa ngumu kwa Biashara United kupanda Ligi Kuu na matumaini pekee ambayo yamebakia kwao ni kujinusuru kutoshuka daraja maana hakuna hayo maajabu ambayo yanaweza kutokea ikamaliza kwa pointi nyingi kuzidi timu nne zilizo juu ya msimamo wa ligi ya Championship.

Chochote kitakachotokea kwa Biashara United mwishoni mwa msimu, lawama zinapaswa kuelekezwa kwa wakazi wa mkoa wa Mara kwani wao wanahusika kwa kiasi kikubwa kusababisha timu hiyo kutosafiri kwenda Mbeya.

Wameiacha timu kwa viongozi ambao wamekuwa wakihangaika huku na kule kusaka fedha za kuisafirisha timu hadi inafikia hatua wamekwama wakati timu hiyo inawakilisha mkoa na uwepo wake ni faida kwa mji mzima wa Musoma na maeneo ya jirani.

Ni aibu kwa mkoa ambao una watu wazito na wengine wadau wakubwa wa soka kukosa angalau Sh2 milioni ili kuiwezesha Biashara United kusafiri kwenda Mbeya kucheza mechi ya Championship.

Katika kijiwe chetu tunaamini wenye mkoa wao wameichoka timu ndo maana wameamua kutoichangia ili ishuke ingekuwa kinyume wasingeshindwa kuichangia.

Related Posts