Maafisa wa Palestina wamesema shambulio la anga laIsrael limewaua zaidi ya watu 10 katika Ukanda wa Gaza, wakiwemo watoto watatu na maafisa wawili wa vyeo vya juu katika jeshi la polisi linaloongozwa na Hamas. Wakati huo huo aliyekuwa waziri wa ulinzi wa Israel Yoav Gallant ametangaza kwamba atajiuzulu bungeni.
Shambulizi la mapema Alhamisi limeyalenga mahema katika eneo la Muwasi ambalo Israel ilitangaza kwamba ni eneo la kibinadamu. Eneo hilo linatumika kwa mamia ya maelfu ya watu waliokimbia makazi yao kujihifadhi wakati wa baridi na mvua.
Shambulio hilo limewaua watoto watatu, wanaume wanne na na wanawake watatu kwa mujibu wa hospitali ya Nasser iliyopokea miili hiyo.
Miongoni mwa waliofariki ni Meja Jenerali Mahmoud Salah, mkurugenzi mkuu wa polisi ya Gaza inayosimamiwa na Hamas na naibu wake Brigedia Jenerali Hossam Shahwan, kulingana na taarifa ya hospitali hiyo.
Soma zaidiWahuthi waendelea kuwa mwiba kwa Israel: Wachambuzi.
Jeshi la Israel limesema mashambulizi hayo yamewalenga wapiganaji wa Hamas na Waziri wa Ulinzi wa Israel, Katz ametishia kwamba vikosi vyake vitazidisha mashambulizi yake huko Gaza ikiwa Hamas itaendelea kurusha maroketi nchini Israel.
Ama katika hatua nyingine, Mamlaka ya Palestina imelizuwia shirika la habari la Al Jazeera kutangaza katika eneo la ukingo wa Magharibi wa Gaza kufuatia kile ilichodai kuwa shirika hilo linatoa taarifa za uchochezi na kupotosha.
Al Jazeera imekuwa ikiripoti matukio mbalimbali katika ukanda huo tangu kuanza kwa vita Oktoba 7 mwaka 2023.
Gallant: Nitajiuzulu bungeni
Mbali na hayo yanayoendelea huko Gaza, ndani ya Israel kwenyewe aliyekuwa waziri wa ulinzi wa nchi hiyo Yoav Gallant, ambaye alifutwa kazi mwezi Novemba baada ya kuongoza kampeni ya kijeshi huko Gaza kwa zaidi ya mwaka mmoja, ametangaza hapo jana kwamba atajiuzulu kutoka bungeni.
“Kama Waziri wa zamani wa Ulinzi, ninawajibika kwa kila kitu kilichotokea tangu mwanzo kwenye nafasi yangu katika miezi kabla ya vita hadi mwisho wa nafasi yangu zaidi ya mwaka mmoja baada ya kuanza kwa vita.” amesema Gallant.
Mnamo Novemba, Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu ilitoa waranti wa kukamatwa kwa Waziri Mkuu wa Israel Benjamini Netanyahu na Yoav Gallant pamoja na mkuu wa jeshi la Hamas, Mohammed Deif, ambaye jeshi la Israel linasema lilimuua huko Gaza.
Mahakama hiyo iisema kwamba imepata sababu zenye mashiko za kuamini kwamba Netanyahu na Gallant wamefanya uhalifu dhidi ya ubinadamu.