AKILI ZA KIJIWENI: Jibu la Chalamanda ni rahisi sana

 MDAU mmoja hapa kijiweni amehoji kwa nini kipa wa Kagera Sugar, Ramadhan Chalamanda kaitwa katika kikosi cha timu ya Tanzania Bara ‘Kilimanjaro Stars’ kitakachocheza kwenye Kombe la Mapinduzi.

Ameshangaa kuitwa kwa Chalamanda huku akiwa hayupo hata katika orodha ya makipa watano wanaoongoza kwa kucheza mechi nyingi bila kuruhusu mabao (clean sheet).

Na akatoa mfano wa kipa wa Mashujaa FC, Patrick Munthali kuwa ana clean sheet nyingi kumzidi Chalamanda lakini yeye hajaitwa ila kipa huyo wa Kagera Sugar ameitwa sambamba na Metacha Mnata wa Singida Black Stars na Anthony Mpemba wa Azam FC.

Sasa jamaa asichoelewa pengine ni kwamba ‘klinishiti’ huwa sio kipimo pekee cha ubora wa kipa na badala yake kuna mambo mengine ambayo hutazamwa katika kumuita kipa kwenye timu ya taifa.

Klinishiti inaweza kumsaidia kipa pale kunapokuwa na ushindani wa tuzo lakini kwa maana ya timu ya taifa wanaangalia kiwango binafsi na uzoefu kwa wakati huo timu inaitwa na hapo ndipo Chalamanda alipotokea.

Chalamanda amefanya vizuri sana akiwa na Kagera Sugar japo hana klinishiti nyingi kwani amekuwa akiokoa hatari nyingi hasa za ana kwa ana kutoka kwa wachezaji wa timu pinzani kiasi kwamba kama hizo hatari zingeingia nyavuni basi timu yake ingefungwa mabao pengine mara mbili au tatu ya waliyofungwa hadi sasa.

Kingine ambacho kinambeba Chalamanda ni ile sifa ya uongozi aliyonayo ambayo unaweza kuiona pindi akiwa anazungumza na wachezaji wenzake au marefa na wakati mwingine hata wachezaji wa timu pinzani.

Tukumbushane kwamba nafasi ya unahodha kwa mchezaji huwa haitolewi kirahisi na ni lazima awe na nidhamu na pia tabia za kiongozi lazima ziwepo ndani mwake.

Mwisho wa yote kijiweni tumefurahia kuona kumeanza kuibuka kwa makipa wa klabu nyingine tofauti na Simba, Yanga na Azam ambao wanaonyesha viwango bora.

Related Posts