Waliofariki kwa kugongwa gari Marekani wafikia 15

Marekani. Idadi ya vifo vilivyotoka na kugongwa na gari aina ya Pickup eneo la Bourbon, New Orleans nchini Marekani imefikia 15 baada ya majeruhi watano kati ya 35 kufariki usiku wa kuamkia leo.

Ajali hiyo ilitokea siku ya mkesha wa mwaka mpya 2025, uliohudhuriwa na mamia ya watu katika eneo, hilo huku dereva wa gari hiyo akitambuliwa kuwa ni Mkazi wa Texas na mwanajeshi mstaafu wa jeshi la nchi hiyo, Shamsud-Din Jabbar, (42).

Shamsud aliyehudumu katika jeshi la nchi hiyo ikiwemo nchini Afghanistan aliendesha gari hiyo kisha kuparamia umati wa watu waliokuwa wakisherehekea sikukuu hiyo.

Kwa mujibu wa Mkuu wa Polisi katika jiji hilo, Anne Kirkpatrick alidai mtuhumiwa baada ya kuugonga umati huo alishuka kwenye gari na kuanza kumimina risasi jambo lilisababisha majeraha kwa maofisa wawili wa Polisi nchini humo.

Hata hivyo, aliuawa muda mfupi baada ya majibizano ya risasi hizo huku uchunguzi uliofanywa na maofisa wa FBI, ukibaini kuwepo vilipuzi katika eneo ilipokuwa gari hiyo.

Kufuatia tukio hilo, Rais Joe Biden wa Marekani amehutubia taifa hilo leo Januari 2, 2025 akisema idadi ya vifo imefikia watu 15 baada ya majeruhi wengine watano wa tukio hilo kufariki dunia wakipatiwa matibabu.

Biden pia amesema mhusika wa tukio hilo baada ya kuchunguzwa imebainika kuwa alikuwa na ushirika na kundi la kigaidi la ISIS.

Kwa mujibu Rais Biden maofisa wa FBI, wamemueleza kuwa mtuhumiwa huyo ambaye aliuawa kwa kupigwa risasi na maofisa wa polisi alikuwa akishirikiana na kundi hilo lenye makao yake Mashariki ya Kati.

“Ninaungana na kila mmoja wetu ambaye anaomboleza vifo vya wenzetu ambao wamefariki katika ajali hii.

 “Maofisa wa FBI wamebaini kwamba Shamsud-Din Jabbar alikuwa peke yake na ndani ya gari yake kulikutwa bendera ya kundi hilo la ISIS,” amesema Biden.

Hata hivyo, FBI ilitoa taarifa kuwa haimini iwapo Shamsud aliweza kutekeleza tukio hilo peke yake, badala yake imeanzisha uchunguzi dhidi ya watu wake wa karibu ili kufahamu ushiriki wao katika tukio hilo.

Kipande cha video kilichochapishwa kwenye tovuti ya AlJazeera kimeonyesha baadhi ya washerehekeaji wakikimbia kwa kuchanganyikiwa kutokana na ajali hiyo na mrushiano wa risasi kati yake na polisi.

Katika hatua nyingine, Mkuu wa Polisi katika jiji hilo, Anne Kirkpatrick aliliita tukio hilo kama la kigaidi huku akisisitiza kuwa upelelezi wake unaendelea.

Related Posts