BAADA ya kiungo mshambuliaji wa KMC, Ibrahim Elias ‘Mao’ kutoonekana kikosini uongozi wa timu hiyo umemalizana na Offen Chikola kwa ajili ya kuongeza nguvu kikosini humo.
Elias tangu alipoonyeshwa kadi nyekundu kwenye mchezo wa ligi dhidi ya Fountain Gate ugenini huku timu yake ikikubali kichapo cha mabao 2-0 hajaonekana kikosini.
Chanzo cha kuaminika kutoka ndani ya KMC kimeliambia Mwanaspoti kuwa kutokana na kutoweka kwa kiungo huyo ambaye wakimpigia simu hashiki wameamua kufanya uamuzi wa kusajili kiungo mwingine ambaye wanaamini ni mbadala sahihi.
“Ni kweli Elias hayupo pamoja na timu tunasikia tu yupo Kenya kwasababu hata simu tukimpigia hapokei hilo kama viongozi tunaendelea kulifanyia kazi lakini ili kuendana na kasi tumesajili mchezaji mwingine,” alisema mtoa taarifa huyo na kuongeza;
“Chikola ndio usajili mpya tulioufanya eneo la kiungo na tuna imani na uwezo alionao kutokana na kuwa na uzoefu na ligi lakini pia ana uwezo mkubwa wa kutengeneza mashambulizi na kutumia nafasi akipata.”
Chanzo hicho kilisema mbali na Chikola wapo kwenye hatua nzuri za kumalizana na aliyekuwa mshambuliaji wa Simba, Shabaan Chilunda kwa lengo la kuongeza nguvu eneo la mwisho huku akiweka wazi kuwa wana mpango wa kusajili washambuliaji wawili.
“Chilunda alikuwa pamoja na timu kwa muda akifanya mazoezi kama kocha alivyokuwa anataka afanye, amegundua kuwa ni mchezaji mzuri lakini sio wa kumtegemea na kusisitiza tuhakikishe tunapata mshambuliaji mwingine kabla ya dirisha kufungwa.”