Danadana zagubika ununuzi mabasi ya mwendo kasi

Dar es Salaam. Danadana zimegubika ununuzi wa mabasi katika Mradi wa Mabasi yaendayo Haraka (BRT) chini ya Wakala wa Mabasi Yaendayo Haraka (Dart) katika awamu ya kwanza na ya pili.

Rais Samia Suluhu Hassan, alipotoa salamu za Mwaka Mpya kwa Watanzania Desemba 31, 2024 alisema katika mwaka 2025 miongoni mwa miradi itakayotekelezwa kwa uwekezaji kwa njia ya ubia baina ya Serikali na Sekta Binafsi (PPP) ni wa BRT.

Alieleza Serikali itatoa kipaumbele kutekeleza miradi ya kupunguza msongamano katika majiji likiwamo la Dar es Salaam, kwa kutekeleza awamu ya tatu na ya nne za miundombinu ya barabara za mwendo kasi na kuanza huduma kwenye awamu ya pili kwa njia ya Mbagala iliyokamilika.

Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa leo Januari 2, 2025 amesema Serikali imeshafanya uamuzi wa kushirikisha sekta binafsi kupitia PPP kununua mabasi ya mwendokasi ambayo yameagizwa na yanatarajiwa kuwasili nchini Februari hadi Machi, 2025.

Akizungumza katika kipindi cha Morning Trumpet cha Azam TV, Msigwa amesema kwa njia ya Kimara sekta binafsi italeta mabasi takribani 177 na njia ya Mbagala yameagizwa mabasi 755 kwa ajili ya kutoa huduma kuanzia Machi, 2025.

“Tumefanya hivi kwa sababu tuna changamoto kubwa ya uchache wa mabasi kwenye njia zetu zinazotoa huduma na kusababisha usumbufu kwa watu kwani hii nayo ni biashara,” amesema.

Msigwa amesema hiyo ni sehemu ya kutoa huduma pia ni biashara, hivyo Serikali ingependa kufungua milango ya namna hiyo kwa ajili ya sekta binafsi kufanya kazi.

Katika kuhakikisha changamoto za huduma za usafirishaji zinatatuliwa, amesema wapo katika hatua za mwisho, hivyo Mkoa wa Dar es Salaam wataanza kunufaika na mradi huo.

Awali, iliahidiwa mabasi hayo yangewasili nchini Desemba, 2024. Hata hivyo, Dart ilieleza kuwa, suala hilo lipo Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG).

Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano na Uhusiano kwa Umma wa Dart, William Gatambi akizungumza na Mwananchi Desemba 20, 2024 kuhusu utekelezaji wa agizo la Serikali kuwa mabasi hayo yawe yamewasili Desemba, alisema suala hilo lipo mikononi mwa AG.

Agosti 2, 2024 akizindua mageti na kadi janja kwa ajili ya usafiri huo, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Mohammed Mchengerwa, aliwaagiza Dart ifikapo Desemba 2024, mabasi ya mwendokasi yanayotakiwa katika Barabara ya Morogoro na ile ya Mbagala yawe yamepatikana.

Mchengerwa alisema wananchi wamechoka na danadana za ujio wa mabasi hayo akaagiza Desemba iwe mwisho, yawe yamekuja lakini mpaka sasa ukimya umetawala.

“Watanzania wamesubiri kwa muda mrefu kupatikana kwa mabasi hayo na sasa inatosha hatatuki tena kusikia changamoto hii wizarani.

“Pia, lile suala linaloitwa mchakato kila siku wala ubishani kuhusu utekelezaji wa suala hilo kati ya Wakala wa Mabasi (Dart) na Kampuni ya uendeshji Mradi (Udart) nisisikie,” aliagiza Mchengerwa.

Alisema taarifa alizokuwa nazo ni kuwa, Barabara ya Morogoro inahitaji mabasi 170, huku ile ya Mbagala ikihitaji mabasi 500.

Mwananchi ilipozungumza na AG, Johari Hamza Desemba 20, 2024 alikiri suala hilo limeshamfikia akaeleza linafanyiwa kazi.

Johari alisema wanatarajia kukamilisha mchakato kabla ya Desemba kuisha kama ilivyoagizwa na Serikali.

Akizungumzia mchakato huo kuchukua muda mrefu alisema: “Hii ni kutokana na mradi huo kuhusisha taasisi nyingi, hivyo kila mahali Serikali lazima kujiridhisha kabla ya kuingia mkataba.

“Niwaombe wananchi wawe na subira, Desemba hii kabla haijaisha mkataba utakuwa umesainiwa kama ambavyo Serikali iliahidi,” alisema.

Gatambi alisema katika utekelezaji wa agizo la Serikali, kazi waliyofanya ni kufuata taratibu za kupata dhamana ya Serikali kuwezesha mkataba kati ya Dart na mwekezaji Emirates National Group (ENG) kutoka Falme za Kiarabu.

“Dhamana ya Serikali imepitia ngazi mbalimbali na sasa ipo kwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali, ikitoka hapo kitakachofuata ni kufuata taratibu zingine za kuleta mabasi,” alisema.

Alisema mwekezaji ataleta mabasi kwa ajili ya awamu ya kwanza inayohusisha barabara ya Morogoro, kazi ambayo atapaswa kuitekeleza ndani ya miezi mitatu tangu watakaposaini mkataba.

Kwa barabara ya Mbagala, alisema wameshaanza upembuzi yakinifu na kinachosubiriwa ni kupitiwa na kupewa idhini na kamati ya uongozi.

“Katika Barabara ya Morogoro, baada ya kamati kumaliza kazi yake na kupata idhini, taratibu zingine za mabasi awamu ya pili ya barabara iendayo Mbagala zitaendelea.

“Kwa hiyo zote hizo zinafanyiwa kazi kwa hatua mbalimbali ambazo nimezitaja, huku zile za awamu ya tatu na ya nne nazo zipo katika hatua mbalimbali ambazo hatuwezi kuzizungumzia kwa sasa,” alisema.

Alisema ujenzi wa barabara utakapokamilika na ujio wa mabasi utakuwa umekamilika.

Wakati mradi unaanza kufanya kazi mwaka 2016, Udart ilileta mabasi 140 baadaye ikaongeza 70.

Hata hivyo, kutokana na mabasi mengine kuchakaa na kuharibika, hivi sasa mabasi yanayofanya kazi barabarani hayazidi 100.

Related Posts