PAMOJA na heshima aliyopata kutoka Championship hadi Ligi Kuu, kocha mpya wa Tanzania Prisons, Aman Josiah anakabiliwa na mtihani mzito kutoboa.
Josiah anatarajia kuinoa Prisons baada ya mtangulizi wake, Mbwana Makata kufungashiwa virago kutokana na matokeo yasiyoridhisha katika Ligi Kuu.
Katika michezo 15 aliyoiongoza Makata, Prisons imeshinda miwili, sare tano na kupoteza saba na kuiacha katika nafasi ya 14 kwa pointi 11 kabla ya Shaban Mtupa kuipa alama tatu zilizoipandisha hadi nafasi ya 11.
Josiah amejiunga na maafande hao akitokea Geita Gold ya Championship lakini kabla ya hapo aliitumikia Biashara United na Tunduru Korosho ya First League na kesho Januari 3 ataanza kazi rasmi.
Mtihani wa kwanza kwa kocha huyo ni kukabiliana na wachezaji majeruhi kikosini humo ambao wengi wao ni wakongwe na tegemeo ndani ya timu.
Mastaa kama Samson Mbangula, Jeremia Juma, Salum Kimenya, Nurdin Chonya, Lambart Sabiyanka na Jumanne Elfadhil ni nyota wanaotegemewa kwa kiasi kikubwa.
Waandamizi hao ni sehemu ya kikosi cha kwanza ambao wote kwa sasa wanaandamwa na majeraha ambapo bado haijajulikana kurejea kwao kikosini kuendelea na Ligi Kuu na kuiokoa timu hiyo na kushuka daraja.
Pamoja na kufanya kazi kwa kujiamini, lakini Josiah hana uzoefu wa Ligi Kuu kwani kwa muda mwingi amekuwa katika timu za Championship.
Mara ya mwisho kusimama kwenye benchi kwa timu ya Ligi Kuu ilikuwa msimu wa 2018/19 wakati Biashara United ikishiriki michuano hiyo akiwa chini ya kocha mkuu Hitimana Thierry.
Msimu uliopita akiiongoza Biashara United aliifikisha hatua ya play off ya kupanda Ligi Kuu, lakini matokeo ya jumla ya 2-1 dhidi ya Tabora United yaliinyima nafasi ya kupanda daraja.
Pamoja ugumu wa matokeo wanayopitia Prisons bado haijafanya usajili wowote huku ikiondokewa na staa wake tegemeo, Zabona Hamis aliyejiunga na Pamba Jiji FC ya Mwanza.
Maafande hao bado hawana mwenendo mzuri ambapo kama watazembea lolote linaweza kuwakuta kama ilivyowahi kutokea mwaka 2012, waliposhuka daraja kabla ya kurejea msimu uliofuata.
Licha ya ushirikiano walionao viongozi wa timu jijini Mbeya, lakini uamuzi wa mambo yote yahusuyo Prisons huamuliwa na mabosi waliopo makao makuu Dodoma hivyo kuweka ugumu katika uamuzi wa mambo kadhaa.
Kaimu Mtendaji Mkuu wa timu hiyo John Matei amesema matarajio yao mzunguko wa pili ni kusahihisha makosa na kujinasua nafasi za chini kwa usajili watakaoufanya.
“Tutaboresha kikosi, mzunguko wa pili utakuwa wa mafanikio kwetu, tutajitahidi kutekeleza ripoti ya benchi la ufundi kwakuwa tunao majeruhi wengi ambao lazima tuwe na mbadala wao,” amesema kigogo huyo.