KIKOSI cha Yanga kesho kitapiga tizi la mwisho kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, kabla ya keshokutwa kurejea kambini Avic Town kujiandaa na pambano la Kundi A la Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya TP Mazembe ya DR Congo, huku kiungo wa zamani wa timu hiyo ya Jangwani akiitabiria ushindi wa mapema nyumbani.
Raymond Nduguru aliyewahi kuichezea Yanga baada ya kumsajili kutoka Abajalo ya Sinza, amesema kwa hii falsafa ya kocha Sead Ramovic ya ‘Gusa Achia Twende Kwao’ anaamini TP Mazembe inakufa mapema tu iwapo tu timu itaamua kucheza kama ilivyocheza katika mechi nne mfululizo za Ligi Kuu Bara.
Yanga inatarajiwa kuwa wenyeji wa mchezo huo wa kimataifa keshokutwa Jumamosi (Januari 4, 2025) dhidi ya Mazembe ikiwa ni wa nne kwa kila moja katika kundi hilo lenye Al Hilal ya Sudan inayoongoza msimamo na MC Alger ya Algeria inayoshika nafasi ya pili, huku zikiwa na kumbukumbu ya kutoka sare zilipokuwa jijini Lubumbashi.
Vijana wa Jangwani wanahitaji ushindi ili kujiweka pazuri, kwani kwa sasa inaburuza mkia ikiwa na pointi moja, nyuma ya Mazembe inayoshika nafasi ya pili kutokana na kuwa na pointi mbili zote zikitokana na sare.
Akizungumza na Mwanaspoti, Ndunguru aliichezea Yanga mwanzoni mwa miaka ya 2000 amesema wababe hao wa soka nchini, wana nafasi kubwa ya kushinda mchezo huo, ila akashaurui kutumia mbinu za kushambulia mwanzo mwisho ili kutowapa utulivu wapinzani.
Ndunguru amesema kutoonekana kwa muda mrefu kwa kipa wa kimataifa raia wa Mali, Djigui Diarra haiwezi kuathiri chochote kutokana na uwezo alionao Abuutwalib Msheri kuonesha kiwango bora kwa mechi tatu alizocheza.
“Ile gusa achia twende kwao ndio inatakiwa katikamechi hiyo, iwe ni kushambulia mwanzo mwisho kutowapa nafasi TP Mazembe kutulia kwa namna yoyote, pia hata kama Diarra atakosekana, bado sioni tatizo kwani Msheri anaweza kusaidia kama ilivyokuwa katika michezo iliyopita alipoonesha ubora,” amesema Ndunguru, aliyewahi pia kuweika na Coastal Union na JKT Ruvu (sasa JKT Tanzania).
Nduguru amekiri haitakuwa mechi rahisi kutokana na timu zote kuhitaji ushindi ili kujiweka mazingira mazuri ya kufuzu robo fainali ya michuano hiyo, lakini wenyeji wanauhitaji zaidi mchezo huo kwani ikipoteza dira na muelekeo wa kutimiza ndoto za kucheza kwa msimu wa pili mfululizo hatua hiyo ya robo ya Mabingwa.
“Benchi la ufundi halina tatizo tumeona kazi yake, zaidi ni Yanga kutoruhusu makosa yoyote, mechi itakuwa ngumu kwakuwa wapinzani nao watakuja na mbinu zao” alisema mchezaji huyo aliyestaafu soka mwaka 2006.
Katika mechi nne zilizopita za Ligi Kuu Yanga ilipata ushindi dhidi ya Mashujaa iliyowanyuka 3-2, TZ Prisons na Dodoma Jiji zilizopigwa 4-0 kila moja, kisha kuifumua Fountain Gate kwa mabao 5-0 huku kikosi kikicheza kwa kasi mwanzo mwisho, tofauti na ilivyocheza mechi tatu za Ligi ya Mabingwa ambapo mbili dhidi ya Al Hilal na MC Alger ilipoteza kwa mabao 2-0, kisha kutoka sare ya 1-1 na Mazembe ugenini.
Kocha wa Yanga, Sead Ramovic anayeinoa kwa sasa akichukua nafasi ya Miguel Gamondi atakuwa akisaka ushindi wa kwanza katika mechi za kimataifa, baada ya kushindwa kutoboa kwenye michezo mitatu iliyopita, mbali na kuweka rekodi tamu katika Ligi Kuu akiiongoza mechi tano mfululizo na zote akishinda akikusanya jumla ya mabao 18-2, kwani iliifumua pia Namungo kwa mabao 2-0 kabla ya kuanza kutoa dozi nene kwa staili hiyo ya Gusa Achia…!