Kabamba, Duah watimkia KenGold | Mwanaspoti

MABOSI wa KenGold wako katika harakati za kukisuka kikosi hicho ili kisishuke daraja na tayari wamemali-zana na aliyekuwa nyota wa Yanga Mzambia, Erick Kabamba na kiungo Mghana Stephen Duah aliyezichezea Stand United, Namungo na Kagera Sugar.

Taarifa kutoka ndani ya timu hiyo ya jijini Mbeya inayoburuza mkiani mwa msimamo kwa pointi sita baada ya kushinda mchezo mmoja tu, sare mitatu na kuchapwa 12 kwenye michezo 16, zinaeleza nyota hao wameshakubaliana kila kitu ili kumwaga wino.

“Ni kweli wachezaji hao tuko katika mazungumzo nao na kama kila kitu kitakamilika tutawatangaza kuichezea timu yetu kwa lengo la kuongeza nguvu, hatutaki kuona tunashuka daraja hivyo, lazima tujipange mapema na hilo,” kilisema chanzo chetu.

Ofisa Mtendaji Mkuu wa Kengold, Benson Mkocha alisema kwa sasa asingependa kuzungumza jambo lolote kuhusu usajili kwa sababu bado hawajakamilisha, ingawa ni kweli taratibu hizo zimeanza kutokana na matakwa ya benchi la ufundi.

“Tukikamilisha taratibu zote tutaweka wazi kwa sababu bado mchakato unaendelea na kama unavyojua hiki ni kipindi ambacho ushindani ni mkubwa kutokana na mahitaji ya kila timu, ingawa nikiri mashabiki wetu watarajie mambo mazuri,” alisema.

Kabamba aliyejiunga na Wakiso Giants ya Uganda Julai 25, mwaka jana kwa mkataba wa miaka miwili, amejiunga na KenGold kwa mkopo hadi mwisho wa msimu, huku akicheza timu mbalimbali zikiwamo za, Kabwe Warriors na Buildcon FC za kwao Zambia.

Wengine waliojiunga na kikosi hicho ni, Bernard Morrison aliyetamba na Yanga na Simba, Sadala Lipangile kutokea Biashara United na Stephen Sey ambaye kwa sasa yuko huru.

Nyota wengine ni Obrey Chirwa kutoka Kagera Sugar. beki wa kati, Sandale Komanje kutokea Tabora United na kiungo mshambuliaji, Lassa Kiala aliyepo huru, baada ya kuchezea timu mbalimbali za FC Saint Eloi Lupopo ya kwao DR Congo, Kitwe United na Zanaco FC zote za Zambia.

Related Posts