Warundi 31 washindwa kulipa faini Sh1 milioni kila mmoja, waenda jela

Dar es Salaam. Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, imewahukumu raia 31 wa Burundi kulipa faini ya Sh1 milioni kila mmoja au kutumikia kifungo cha miezi 12 gerezani, baada ya kupatikana na hatia ya kuwepo nchini Tanzania bila kuwa na kibali.

Pia mahakama hiyo, imeelekeza washtakiwa hao baada ya kumaliza kutumikia adhabu hiyo, warejeshwe nchini kwao kila mmoja.

Hata hivyo, washtakiwa hao wameshindwa kulipa faini na hivyo wamepelekwa gereza kuanza kifungo cha miezi 12 jela.

Waiohukumiwa adhabu hiyo ni Said Jafari (40), David Erick (25), Mukowimana Bienvenue (27) na wenzao 28.

Hukumu hiyo imetolewa leo Alhamisi Januari 2, 2025 na Hakimu Mkazi Mkuu, Anna Magutu, baada ya washtakiwa kukiri shtaka hilo na mahakama kuwatia hatiani kama walivyoshtakiwa.

Akisoma hukumu hiyo, hakimu Magutu amesema kosa linalowakabili washtakiwa hao lina adhabu ya kifungo au faini au Mahakama inaweza kutoa adhabu zote kwa pamoja.

Amesema washtakiwa wametiwa hatiani kwa mujibu wa sheria kama walivyoshtakiwa baada ya kukiri shtaka lao.

“Kila mmoja anatakiwa kulipa faini ya Sh1milioni na kama hataweza kulipa faini hii, basi atatumukia kifungo cha miezi 12 jela,” amesema Hakimu Magutu

Kabla ya kutolewa kwa adhabu hiyo, washtakiwa waliomba mahakama iwape adhabu ndogo kwani wamekiri shtaka lao wenyewe na kwamba ni kosa lao la kwanza.

Awali, Wakili wa Serikali Raphael Mpuya amemba mahakama itoa dhabu kwa mujibu wa sheria.

Washtakiwa hao wanadaiwa kutenda kosa hilo Desemba 19, 2024 walipokutwa eneo la Jangwani, wilaya ya Ilala wakiishi nchini bila kuwa na kibali au nyaraka inayowatambulisha uhalali wao.

Kwa mara ya kwanza, washtakiwa hao walifikishwa mahakamani hapo Desemba 24, 2024.

Related Posts