Kambi za Mbowe, Lissu zategeana umakamu mwenyekiti Chadema

Dar es Salaam. Wakati Tundu Lissu na Freeman Mbowe wanachuana kuwania uenyekiti wa Chadema, kinyang’anyiro kingine kinatarajiwa kushuhudiwa kwenye nafasi ya umakamu mwenyekiti-bara ambayo kambi hizo mbili bado zinategeana.

Uliacha Ezekiel Wenje ambaye ametangaza nia hiyo, wengine wanaotajwa ni John Heche na Godbless Lema.

Mbowe anayetetea nafasi hiyo aliyeiongoza kwa miaka 20, ataumana vikali na Lissu ambaye kwa sasa ni Makamu wake-bara ambaye  amekwisha kutangaza dira yake ya kwenda kufanya mabadiliko makubwa ya kiutendani na kiutawala na wengine wawili.

Makada wengine wanaowania uenyekiti ni Romanus Mapunda na Charles Odero.

Dirisha la uchukuaji na urejeshaji fomu kwa ngazi hiyo ya taifa linahitimishwa saa 10:00 jioni ya Januari 5, 2024.

Lissu na Mbowe tayari wamechukua na kurejesha fomu huku kwenye nafasi ya makamu mwenyekiti-Bara bado wafuasi wa kambi hizo wanamtegeana.

Hata hivyo, taarifa zilizopatikana wakati tunakwenda mitamboni ni kuwa Francis Garatwa aliyewahi kuwa diwani amechukua fomu kugombea nafasi ya makamu mwenyekiti -Bara.

Taarifa za ndani ya chama hicho, zinaeleza timu ya Lissu na ile ya Mbowe kila mmoja ijipanga kuangalia nani atasimamishwa umakamu ili kuhakikisha wanapata nafasi zote za juu, endapo upande wao utashinda.

Taarifa kutoka vyanzo mbalimbali zinaeleza Wenje, mwenyekiti wa Kanda ya Victoria na  aliyewahi kuwa mbunge wa Nyamagana, huenda akachukua fomu kesho au keshokutwa, akitajwa kuwa upande wa Mbowe.

Timu ya Lissu bado iko kimya lakini duru za siasa ndani ya upande huo, zinawataja wanasiasa wawili waliowahi kuwa wabunge, John Heche (Tarime Vijijini) na Godbless Lema (Arusha Mjini na aliyekuwa mwenyekiti wa Kanda ya Kaskazini) kuwania nafasi hiyo.

Heche ambaye ni mjumbe wa kamati kuu ametafatwa kuzungumzia hilo bila mafanikio, lakini siku za karibuni aliandika kwenye mtandao wa X kuwa atatoa kauli siku si nyingi.

Pamoja na kwamba hajaeleza wazi, amekuwa akiweka picha na maelezo ya kumuunga mkono Lissu kwenye mitandao ya kijamii.

Lema naye amekuwa kimya na maandishi yake mitandaoni hayaonyeshi kumuunga mkono Mbowe au Lissu. Hata hivyo, vyanzo vya ndani vimekuwa vikimhusisha na upande wa Lissu.

Ikiwa Wenje atachukua fomu kama alivyotangaza na mmoja kati ya Heche au Lema naye atachukua, kutakuwa na mnyukano mwingine ukiacha ule wa Mbowe na Lissu.

Hii inatokana na watatu hao kwanza ni marafiki, wanajuana na wamekuwa pamoja kamati kuu, bungeni na wana wafuasi wengi ndani na nje ya chama hicho.

Gervas Lyenda, mmoja wa waratibu wa kampeni za Lissu, amelieleza Mwananchi kuwa wanakamilisha maandalizi ya mwisho mwisho ili mgombea wa nafasi ya makamu mwenyekiti atakayemuunga mkono Lissu achukue fomu.

“Timu Lissu itakuwa na mgombea wake wa makamu mwenyekiti, ninachoweza kusema leo au kesho atachukua fomu,” amesema Lyenda.

“Mgombea huyo amewahi kuwa mbunge machachari, mmoja wa watu makini kabisa mwenye wafuasi wengi Tanzania nzima bara na visiwani,” amesema.

Alipoulizwa kama ni kati ya Heche na Lema, Lyenda hakukubali wala kukataa zaidi ya kusema: “Naomba nisiseme leo au kesho, taarifa inatosha.”

Mmoja wa viongozi waandamizi ndani ya Chadema alipoulizwa alisema: “Ninachojua mimi huenda Heche au Lema wakachukua fomu kuwania umakamu uenyekiti upande wa Lissu, kuna mambo yanawekwa sawa tu, wanaweza wakachukulia kwenye kanda au makao makuu. Tusubiri tuone maana siku zimebaki chache.”

Desemba 31, 2024, Heche ‘ali-post’ kwenye akaunti yake ya X picha yake akiwa na Lissu na kuandika: “Tuna taasisi ya kuilinda, tuna nchi ya kutetea, tuna Watanzania wa kupigania. Chadema ikifa madhara yake ni makubwa mno kwa Nchi yetu. Lissu sio muongo ni mkweli, muadilifu na muwazi.”

Desemba 30, 2024, Lema kwenye akaunti yake ya X yeye aliweka picha ya Lissu na Mbowe na kuandika: “Ingewezekana mkutano mkuu wa chama chetu utakaofanyika Januari utoke na jina la mgombea urais. Na pia utoe mamlaka kwa kamati kuu/baraza kuu kutafuta mgombea mwenza na kumthibitisha kwa niaba ya mkutano mkuu ili chama kitoke na jina la mgombea sambamba na viongozi wakuu wa Chama.

“Jambo hili ni muhimu kwa ajili ya branding ya mgombea urais na masuala ya uratibu wa masuala ya kampeni na raslimali fedha kwa mgombea. Pengine wazo hili likifanyiwa kazi bila shaka tunaweza kumaliza salama zaidi na kupunguza kelele nyingi zisizokuwa na maana. Kamati kuu inaweza kufikiri hivi.”

Wakati hali ikiwa hivyo, Charles Odero, mmoja wa wagombea uenyekiti amesema kwenye chama hakuna makundi, nafasi zinatangazwa na mtu anagombea  yoyote anayoona inafaa.

“Mimi nagombea uenyekiti na yoyote atakayechukuwa fomu na kushinda nitafanya naye kazi. Lakini ukiwa na makundi sijui timu nani, ni mwanzo wa vurugu za uchaguzi na kila mmoja agombee kwa kujiona anafaa,” amesema Odero na kuongeza:

“Lakini mkisema mtu wetu ni huyu, mtakwenda hivyo hivyo Bavicha, Bawacha, Bazecha, Baraza kuu na kamati kuu. Kwa hiyo kila mmoja agombee nafasi anayoona inafaa.”

Wakati Bara kukiwa hakuna aliyejitosa kuchukua fomu, upande wa Zanzibar tayari wanachama wanne wakijitokeza kuwani ukamau mwenyekiti, akiwemo Said Issa Mohamed anayetetea nafasi hiyo.

Akizungumza na Mwananchi, Naibu Katibu Mkuu wa Chadema-Zanzibar, Salum Mwalimu amesema kumekuwa na mwitikio mkubwa kwa makada kujitokeza kuchukua fomu za kuwania uongozi wa ngazi mbalimbali ikiwemo umakamu uenyekiti.

“Taarifa ya awali wapo wengi waliojitokeza katika kuwania nafasi zote za juu za kitaifa, tunategemea kuwa na ushindani mkali kwenye nafasi ya umakamu uenyekiti. Hadi sasa waliojitokeza kuwania umakamu wapo wanne akiwemo Mohamed anayetetea,” amesema.

“Kuna makada waandamizi wamejitokeza kuwania ujumbe wa kamati kuu, katika mabaraza ya chama kuna watu wa kutosha waliochukua fomu kuchuana, uchaguzi wa mwaka huu una mabadiliko makubwa tofauti na mwaka 2019,” amesema Mwalimu.

Kwenye mabaraza joto kali

Mchuano mwingine utakuwa kwenye mabaraza ya chama hicho la Wazee Bazecha, la Vijana Bavicha na Baraza la Wanawake Bawacha.

Baadhi ya makada wameonyesha nia kuchukua na wengine kurejesha fomu kuwania uenyekiti, katibu, naibu katibu na mweka hazina, wakiwemo  wanaotetea nafasi hizo.

Wabunge wa zamani wa chama hicho ni miongoni mwa wanaowania nafasi Bazecha na Bawacha.

Mbali ya uongozi katika mabaraza, nafasi nyingine inayotolewa macho ni ujumbe wa kamati kuu.

Kibarua kingine kizito kitakuwa kwenye ujumbe wa kamati kuu katika nafasi tano kwa Tanzania Bara, zinazowaniwa.

Tayari makada zaidi ya watano wakiwemo wanaotetea nyadhifa hizo wamechukua fomu, wengine wakionyesha nia kuwania nafasi hizo.

Pamela kumvaa Catherine Bawacha

Aliyewahi kuwa Mbunge wa Afrika Mashariki, Pamela Maassay amechukua fomu kuwania Ukatibu Mkuu wa Baraza la Wanawake wa Chadema (Bawacha).

Pamela amechukua fomu hiyo leo Alhamisi, Januari 2, 2025 katika Ofisi za Baraza hilo, Kinondoni jijini Dar es Salaam. Pamela atachuana na wagombea wengine akiwemo Catherine Ruge anayetetea nafasi hiyo.

Mara baada ya kukabidhiwa fumo, Pamela amedai baraza hilo linaongoza kwa rushwa akieleza mkakati wa kukomesha vitendo hivyo.

Japo amesema hana vidhibitisho vya kuwatia hatiani wahusika, kigezo alichokitumia kuibua tuhuma hizo ni wagombea wa nafasi hiyo kuwasafirisha wajumbe kutoka mikoani kufika Dar es Salaam kuwapigia kura.

“Baraza letu linaongoza kwa rushwa kwasababu tumeshindwa kujitengenezea mazingira ya kujiinua kiuchumi, hivyo watu wanatumia hali duni ya akina mama kujipatia nafasi,” amesema.

Pamela amesema akina mama wenye kiu ya mabadiliko wakishikamana wataleta mabadiliko kwa Taifa akitupia dongo uongozi wa baraza hilo unaomaliza muda wake kuwa ulilegalega baadhi ya mambo.

Pamela amesema fursa alizoziona akiwa Mbunge wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) aultawaunganisha wanawake wajasiriamali wa baraza hilo na kuwaonyesha fursa endapo atapata nafasi hiyo akisisitiza kama wanawake watakuwa chini kiuchumi hawawezi kuisaidia chama.

“Kama nitateuliwa nitakwenda kuwaunganisha wanawake kuchangamkia fursa za biashara mipakani, wanawake wanahitaji mtu wa kuwaonyesha fursa zilizopo nje na ndani ya nchi na kushikwa mkono watoke walipo”amesema.

Pamela amesema akina mama wenye kiu ya mabadiliko wakishikamana wataleta mabadiliko kwa Taifa akitupia dongo uongozi wa baraza hilo unaomaliza muda wake kuwa ulilegalega baadhi ya mambo.

Amesisitiza mabaraza ya chama hicho ndio yenye uwezo wa kukiunganisha chama.

“Baraza linahitaji watu wenye lugha za upendo,kuunganisha watu na wenye hofu ya Mungu ukiwa na hofu ya Mungu utamheshimu kila mtu bila kujali elimu yake,” amesema.

Related Posts