Changamoto za kisiasa zinazoisubiri Ujerumani mwaka 2025 – DW – 02.01.2025

Kudhibiti uhamiaji, kuzuia mashambulizi ya kimtandao, kulinda utawala wa sheria na taasisi za demokrasia ni mambo makuu matatu ambayo yumkini yatachukua muda mwingi katika siasa za Ujerumani mwaka 2025.

Mamlaka zitakabiliwa na kizungumkuti katika kupambana na uhamiaji holela, wakati huo huo zikiendesha sera ya kuwavutia wafanyakazi wa kigeni wenye ujuzi. Changamoto nyingine itakuwa katika kuimarisha hatua za kuzuia mashambulizi ya kimtandao, sambamba na kuhakikisha utawala wa sheria unaheshimiwa, huku demokrasia ikipewa nguvu kustahimili hila za maadui wa ndani na wa nje.

Lakini baadhi ya wabunge wangependelea kuona haya yote yakiwekwa kando, ili kuweza kushughulikia kwanza Uchumi wa nchi unaodorora. Makampuni kama Volkswagen yenye kupeperusha bendera ya Uchumi wa Ujerumani yanajikuta katika mgogoro mkubwa.

Ujerumani | Magdeburg | 2024 | Soko la Krismasi
Waombolezaji wakiwasha mishumaa na kuweka shada la maua kwa wahanga wa shambulio kwenye soko la Krismasi la Magdeburg.Picha: Christian Mang/REUTERS

Watu wana hofu juu ya usalama wa ajira zao, wakijikongoja kumudu gharama ya maisha inayopanda kwa kasi. Kwa maoni ya Marco Wanderwitz, mbunge wa chama cha kihafidhina cha CDU aliyezungumza na DW, kuzorota kwa uchumi wa Ujerumani kunatikisa msingi wa mustakabali wa nchi.

‘”Tatizo kubwa zaidi ni kuwa uchumi wa nchi unalegalega, na hali hiyo inadhoofisha msingi wa siku za usoni. Matokeo yake ni viongozi wa kiuchumi kupoteza Imani yao katika siasa za nchi.”

Juu ya changamoto hiyo kuna kitisho cha mashambulizi ya kimtandao, hususan kutoka Urusi, dhidi ya miundombinu muhimu kama gridi ya umeme.

Kitisho cha mashambulizi ya mtandao

Katika mahojiano na Omid Nouripour mbaye ni mbunge wa chama cha walinzi wa mazingira amesisitiza haja ya kuilinda miundombinu hiyo nyeti, kwa kuimarisha jeshi la polisi na huduma za ujasusi. Anasema taasisi hizo mbili zitakuwa na umuhimu mkubwa mnamo mwaka huu tunaouanza.

Uhamiaji na namna nchi hii itakavyokabiliana na kuongezeka kwa mitazamo mikali ya mrengo wa kulia ni maeneo mengine ambayo yataikosesha usingizi serikali mpya itakayoingia madarakani baada ya uchaguzi mkuu wa tarehe 23 Februari.

Takwimu za shirika la ulinzi wa mipaka ya Umoja wa Ulaya, Frontex, zinaonyesha kupungua kwa idadi ya waomba hifadhi na wahamiaji wa kiholela mnamo miaka ya hivi karibuni. Hata hivyo, kwa mujibu wa takwimu hizo, watu wapatao 166,000 walijaribu kuingia katika nchi za Umoja wa Ulaya mnamo miezi tisa ya kwanza ya mwaka 2024.

Ukraine Fluechtlinge aus der Ukraine im Berliner zentralen Ankunftszentrum
Wakimbizi kutoka Ukraine wakifika katika kituo cha kusajili wakimbizi mjini BerlinPicha: Jochen Eckel/IMAGO

Mamlaka za miji zinasema zimefika katika ukomo wa uwezo wao wa kuwahudumia wakimbizi. Stefan Seidler kutoka chama cha SSW kinachowakilisha maslahi ya watu wenye asili ya Denmark na Frisia, anasema anaweza kuwa shuhuda wa hali hiyo.

“Ninachoweza kusema, kwa maoni yangu, ni kwamba mamlaka za miji zinakabiliwa na hali ngumu ya kuweza kuzimudu gharama hizi. Zinahitaji msaada wa serikali ya shirikisho ili kuweza kutimiza majukumu yake.”

Kisha ni suala la kuilinda mahakama ya katiba. Kupanuka kwa ushawishi wa chama cha mrengo mkali wa kulia cha Mbadala kwa Ujerumani, AfD kunakwenda sambamba na kitisho dhidi ya jamii za wachache kama zile zinazowakilishwa na chama cha SSW cha Stefan Seidler.

Ni kwa maana hiyo kwamba vyama vyote vikubwa vimedhamini muswada bungeni, unaotaka kulindwa kwa mahakama ya katiba ili isiingiliwe kisiasa. Hiyo ni hoja inayoungwa mkono na theluthi mbili za wabunge wa Ujerumani, hata wakati huu wa kampeni zenye mgawanyiko mkali wa kisiasa.

 

Related Posts