Shehena nyingine ya mali za Tanesco, Dawasa na TRC yakamatwa

Mkuranga. Watu kadhaa wanashikiliwa na Polisi Mkoa wa Pwani wakituhumiwa kukutwa na mali mbalimbali za mashirika ya umma.

Mali hizo ni za Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco), Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (Dawasa) na Shirika la Reli Tanzania (TRC).

Kukamatwa kwa watuhumiwa hao ambao idadi yao haijatajwa na mamlaka za Serikali kunaelezwa ni baada ya ufuatiliaji uliofanywa na kikosi kazi kilichoongozwa na Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Abubakari Kunenge akishirikiana na watumishi wengine.

Imeelezwa shehena hiyo imekutwa imehifadhiwa kwenye moja ya viwanda vya vifaa vya ujenzi wilayani Mkuranga.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Alhamisi Januari 2, 2025 akiwa eneo la tukio, Kunenge amesema wapo baadhi ya wananchi wanaoisaliti Serikali kwa kuiba na kuhujumu miundombinu inayokusudiwa kwa ajili ya maendeleo ya Taifa.

Amesema licha ya jitihada zinazofanywa na Serikali kuboresha miundombinu, wapo wachache wanaoshiriki vitendo vya kuhujumu, jambo ambalo linahatarisha maendeleo na huduma muhimu kwa jamii.

“Hatutavumilia yeyote atakayehusika kurudisha nyuma maendeleo ya Serikali. Tutachukua hatua kali na kuwasaka wahusika popote walipo,” amesema.

Mwishoni mwa mwaka jana, Jeshi la Polisi liliwakamata watu walikamatwa kwa vipindi tofauti wakidaiwa kuhujumu miundombinu ya Tanesco na TRC.

Wanne hao walikamatwa wakati ambao tayari TRC ilishaeleza kuwapo kwa baadhi ya watu wanaokula njama za kuharibu miundombinu ili kuzorotesha usafiri wa treni ya kisasa (SGR).

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Mkoa wa Kipolisi Rufiji, watuhumiwa wawili walikamatwa Desemba 13, 2024 wakiwa na vitofari vya shaba 426 vyenye uzito wa kilo 7,728 na nyaya za shaba zenye uzito wa kilo 2,628.5 zilizotambuliwa kuwa ni mali zilizoibwa kwenye miundombinu ya Tanesco.

Pia wanadaiwa kukamatwa na nyaya za shaba za TRC zenye uzito wa kilo 430 na vipande vya shaba vilivyotengenezwa kutoka kwenye nyaya ambazo zimeibiwa Tanesco na TRC ili kuficha uhalisia wake.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo iliyotolewa Desemba 14, 2024 watuhumiwa walikamatwa baada ya kukamatwa gari aina ya Fuso lililobeba shehena ya vipande na nyaya za shaba walizotoa kiwandani.

Wawili hao walidaiwa kukamatwa ikiwa ni saa chache tangu Jeshi hilo kutangaza kuwashikilia watuhumiwa wengine wawili wenye asili ya Asia Desemba 12, 2024 katika Wilaya ya Mkuranga, Mkoa wa Kipolisi Rufiji.

Katika tukio la awali raia hao wa kigeni walidaiwa kukutwa na nyaya za shaba ambazo zilitambuliwa kuhujumiwa kutoka miundombinu ya Tanesco na TRC zilizokutwa katika kiwanda chao.

Wawili hao walikutwa na nyaya za shaba za Tanesco zilizokuwa na kilo 608.6 na kilo 5,500.17 za TRC.

Related Posts