Vikosi vya Syria vyaanzisha operesheni Homs – DW – 02.01.2025

Shirika la Uangalizi wa Haki za Binadamu la Syria linasema operesheni hiyo inalenga waandamanaji wa Alawi, maandamano ambayo serikali mpya imeyatafsiri kama uchochezi.

Maandamano hayo yalichochewa na video ya shambulio kwenye jumba la ibaada, ingawa serikali inadai ni ya zamani.

Hatua hii imeongeza hofu ya kulipiziwa kisasi ndani ya jamii ya Alawi baada ya kuondolewa kwa utawala wa Bashar al-Assad.

Utawala mpya, unaoongozwa na kundi la Hayat Tahrir al-Sham, umejaribu mara kadhaa kuwahakikishia usalama jamii za wachache, wakiwemo wa Alawi.

Hata hivyo, operesheni za hivi karibuni dhidi ya wapiganaji wanaomuunga mkono Assad katika maeneo kama Tartus na ukandamizaji wa waandamanaji wa Alawi zimeongeza hofu kuhusu nia ya kweli ya serikali. 

Soma pia: Sura mpya ya Syria: Ujumbe wazuru Saudi Arabia, waandamanaji Douma wadai haki

Viongozi wapya wameanzisha pia mabadiliko makubwa katika mtaala wa elimu wa Syria, yanayojumuisha kuondoa mashairi yanayohusiana na wanawake, kubadilisha tafsiri za baadhi ya aya za Quran, na kubadilisha misemo ya kitaifa na jumbe za Kiislamu.

Wakosoaji wanahofia kwamba mabadiliko haya yanatishia mshikamano wa kijamii na utulivu wa muda mrefu wa Syria. 

Syria Damascus: Vikosi vya usalama
Vikosi vya usalama vya serikali mpya ya Syria vikiimarisha ulinzi katika eneo la waandamanaji wa Alawi katika wilaya ya Mazzeh mjini Damascus, Jumatano, Desemba 25, 2024.Picha: Omar Sanadiki/AP Photo/picture alliance

Zelenskiy asema Ukraine kurejesha uhusiano na Syria

Katika hatua nyingine, Rais wa Ukraine Volodymyr Zelenskyy ametangaza mipango ya kurejesha mahusiano ya kidiplomasia na Syria, hatua inayoweka msingi mpya wa ushirikiano kati ya nchi hizo mbili.

Maendeleo haya yanakuja baada ya uhusiano kukatika mwaka 2022 kufuatia hatua ya utawala wa Assad kutambua maeneo yanayokaliwa na Urusi mashariki mwa Ukraine.

Ukraine pia inalenga kuongeza mara mbili biashara na Lebanon mwaka huu, ikionyesha mkakati wa kuimarisha mahusiano ya kiuchumi katika Mashariki ya Kati.

Hatua hii inaonyesha azma ya Ukraine ya kutafuta ushirikiano mpana wa kikanda huku ikiendelea kukabiliana na mgogoro na Urusi. 

“Pia, tutaongeza biashara na Lebanon, ambapo mauzo ya bidhaa za kilimo yataongezwa mara mbili kutoka dola milioni 400 za sasa. Napenda kushukuru idara za kijasusi kwa kuwezesha hatua hizi,” alisema Zelenskiy.

Rais wa Ukraine Volodymyr Zelenskiy
Rais wa Ukraine Volodymyr Zelenskiy, amesema Ukraine inapanga kurejesha uhusiano na Syria baada ya kuanguka kwa Bashar al-Assad.Picha: Ukrainian Presidential Press via REUTERS

Jumuiya ya kimataifa imeendelea kusisitiza umuhimu wa viongozi wapya wa Syria kulinda jamii mbalimbali za nchi hiyo na kuepuka sera zinazoweza kuchochea mgawanyiko wa kidini.

Soma pia: Watawala wapya wa Syria waanza kuwasaka masalia wa Assad

Mashirika ya uangalizi na wanaharakati wanaendelea kutoa wito wa uwajibikaji na uongozi jumuishi ili kuhakikisha utulivu. 

Syria inakabiliwa na changamoto za kipekee katika mchakato wake wa kujijenga upya chini ya serikali mpya.

Ingawa juhudi za kurekebisha taasisi za serikali na kurejesha mahusiano ya kimataifa zinaonyesha matumaini, operesheni za usalama, mabadiliko ya elimu yenye utata, na hofu za wachache zinaonyesha ugumu wa kufanikisha mshikamano wa kitaifa katika taifa hilo lililogawanyika.

Related Posts