TPSF yabainisha mambo matano ya kuangazia mwaka 2025

Dar es Salaam. Shirikisho la Sekta Binafsi Tanzania (TPSF) limeainisha mambo matano makuu litakayoyasimamia mwaka 2025 ili kuendelea kuongeza mchango wake katika uchumi wa nchi.

Mambo hayo ni: kuendelea kusukuma ajenda ya ukuaji jumuishi ndani ya sekta binafsi, kuimarisha sera zinazotabirika, kuimarisha mashirika ya sekta binafsi, kukuza mazingira rafiki ya biashara, na kuhamasisha mazungumzo kati ya sekta binafsi na Serikali.

Hayo yameelezwa leo, Alhamisi, Januari 2, 2025, na Mkurugenzi Mkuu wa TPSF, Raphael Maganga, kupitia ujumbe wake wa mwaka mpya.

Katika ujumbe huo, Maganga amebainisha kuwa mwaka 2024 uchumi wa Tanzania ulikua kwa wastani wa asilimia 5.4, huku sekta za kilimo, viwanda, usafirishaji na vifaa, pamoja na benki na huduma za kifedha zikichangia ukuaji huo.

Amesema ukuaji huo ni wa kupongezwa, lakini wakati ambapo ukuaji wa zaidi ya asilimia 10 ya pato la Taifa (GDP) unatarajiwa, sekta binafsi inapaswa kupewa nafasi ya kuongoza ukuaji huo.

Kutokana na hali hiyo, mwaka 2025 TPSF itashirikiana kwa karibu na wadau wote kutetea vipaumbele vya sekta binafsi kuelekea Dira ya Maendeleo ya 2050. Lengo ni kuhakikisha mahitaji ya jamii ya biashara yanasikika, kushughulikiwa, na kujumuishwa katika sera za kitaifa.

Kuimarisha mazingira ya biashara

TPSF imeeleza kuwa itaendelea kufanya kazi na Serikali na wadau wengine kuunda mazingira thabiti ya sera zinazochochea ukuaji na uvumbuzi. Hatua hiyo imelenga kuongeza imani ya wawekezaji na kuimarisha sekta binafsi.

Aidha, TPSF imepanga kuimarisha Mashirika ya Sekta Binafsi (PSOs) kupitia programu maalumu zinazowasaidia kushirikiana kwa ufanisi na Serikali katika utetezi wa masuala mbalimbali ya sekta hiyo.

Katika kukuza mazingira rafiki ya biashara, TPSF itahakikisha mabadiliko ya sera za kodi, uboreshaji wa taratibu za biashara na vivutio vya uwekezaji vinapewa kipaumbele.

“Tutahamasisha mazungumzo kati ya sekta binafsi na Serikali kwa kushirikisha wadau wa sekta binafsi ili kuongeza nguvu ya ushawishi wa pamoja na kuimarisha mchango wetu katika maendeleo ya kitaifa,” Maganga amesema.

Mkurugenzi huyo ameeleza kuwa mwaka 2024 ulikuwa wa kihistoria kwa TPSF, kwani walikamilisha mabadiliko ya jina kuwa Shirikisho la Sekta Binafsi Tanzania. Hili limefanyika miaka 25 tangu kuanzishwa kwa TPSF, hatua ambayo inalenga kuunganisha vyama vya sekta binafsi kote nchini chini ya sauti moja.

“Hii ni hatua muhimu inayodhihirisha kujitolea kwetu kwa ujumuishi, uratibu, na utetezi wa hali ya juu wa masuala yote ya sekta binafsi katika ngazi ya kitaifa,” amesema Maganga.

Licha ya mafanikio, sekta binafsi ilikumbana na changamoto kama athari za kiuchumi za kimataifa, mfumuko wa bei, mabadiliko ya bei za bidhaa, na vikwazo vya kisheria na kiutawala.

Maganga amepongeza hatua mbalimbali zilizochukuliwa na Serikali kutatua changamoto hizo, ikiwa ni pamoja na kumaliza uhaba wa dola za Marekani na marekebisho ya usimamizi wa kodi yanayoendelea kupitia Tume ya Rais ya Marekebisho ya Kodi.

“Marekebisho haya yanaonyesha maendeleo katika kushughulikia masuala muhimu na kuongeza uthabiti wa kiuchumi,” amehitimisha.

Related Posts