YANGA itaingia rasmi kambini Avic Town kesho Ijumaa kufanya maandalizi ya mwisho kabla ya kuikaribisha TP Mazembe katika pambano la raundi ya nne ya Ligi ya Mabingwa kwa Kundi A, huku benchi la ufundi na vigogo wa klabu hiyo wakiweka mkakati kabambe ili kurejesha heshima anga za kimataifa.
Kwa sasa Yanga ndio inayoburuza mkia katika kundi hilo, ikiwa na pointi moja tu iliyoipata kwenye mchezo wa kwanza ugenini dhidi ya Mazembe na keshokutwa Jumamosi inatarajiwa kuwa wenyeji wa timu hiyo ya DR Congo ili kusaka ushindi wa kwanza katika michuano hiyo na kujiweka pazuri kuvuka hatua ya robo fainali.
Unaambiwa wakati timu ikimalizia mazoezi ya mwisho jioni hii kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa kabla ya kwenda kujichimbia Avic, kuna hesabu mbili za maana zinazopihwa ndani ya klabu hiyo ambazo huenda zisiwe taarifa njema kwa Wakongomani hao.
Taarifa hizo ni namna benchi la ufundi chini ya kocha Sead Ramovic walivyoitolea macho mechi hiyo ili kuvuna pointi zitakazorejesha uhai kwa timu hiyo kutinga robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika kwa msimu wa pili mfululizo, lakini nyingine ni matajiri wa klabu hiyo walioamua kuweka mzigo wa maana mezani.
Yanga inatarajiwa kuwa wenyeji wa Mazembe katika mechi ya Kundi A ya Ligi ya Mabingwa Afrika, itakayopigwa kuanzia saa 10:00 jioni kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, jijini Dar es Salaam ikiwa ni wiki zaidi ya mbili tu tangu zilipovaana jijini Lubumbashi, DR Congo na kumalizika kwa sare ya 1-1.
Mazembe inatarajiwa kutua nchini usiku wa leo kutoka Congo, ili kuwahi mchezo huo, lakini wenyeji Yanga imeutolea macho mchezo huo, kama ambavyo ulimsikia Msemaji wa klabu hiyo, Ally Kamwe juzi na hesabu za kwanza zimeanzia kwa kocha Sead Ramovic aliyesisitiza kwamba mpango walionao ni uleule wa kutotaka kuona Mazembe inapumua Kwa Mkapa.
Ramovic, aliliambia Mwanaspoti kuwa, sasa falsafa zake ya soka la gusa achia twende kwao, imeanza kuishi ndani ya vichwa vya wachezaji wa kikosi hicho na kwamba anataka kuona Mazembe inabanwa kila eneo.
Kocha huyo aliyeiongoza Yanga katika mechi nane za mashindano yote, ikishinda tano, ikitoa sare moja na kupoteza mbili, alisema anataka kuona wachezaji wakiendeleza ukomavu wao waliouonyesha katika mechi nne za ligi zilizopita akitaka timu yake iwabane wapinzani wao na kutengeneza ushindi.
Ramovic hajashinda mechi yoyote ya Ligi ya Mabingwa akipoteza mbili na kutoa sare moja atarudi nyumbani kutafuta ushindi wa kwanza wa mechi hizo kabla ya kumalizana na Al Hilal ya Sudan na MC Alger ya Algeria itakazocheza nao kati ya Januari 12 na 18 kufunga hesabu za makundi.
“Tunahitaji ushindi hilo ndio lengo kuu kwenye mechi hii inayokuja( dhidi ya Mazembe), kitu kizuri sasa kwenye kikosi chetu ni kuimarika kwa wachezaji wetu, nilisema hatutakiwi kumuacha mpinzani anapumua kitu ambacho tunakifanya kwa kiwango kikubwa ingawa bado nataka kuona hilo linaongezeka,” alisema Ramovic na kuongeza;
“Nidhamu tuliyoionyesha kwenye mechi nne hizi tunatakiwa kuiendeleza na sasa ije na huku kwenye mashindano ya Afrika, Mazembe ni timu ngumu lakini tutapambana nao, tuliwabana sana kwennye mechi iliyopita kule kwao lakini sasa tunataka kuwa bora zaidi hapa kwetu ili tupate ushindi.
Yanga jana ilifanya mazoezi kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa chini ya ulinzi mkali, ikiwa ni masharti ya kocha Ramovic aliyetaka kuhakikisha hakuna mtu anaona hata kwa bahati mbaya hesabu zao kuelekea mchezo huo wa Mazembe na leo itarudi Uwanja wa Avic kufanya mazoezi ya mwisho mwisho.
Wakati benchi la ufundi likijipanga hivyo, vigogo na matajiri wa klabu hiyo nao hawalali wakiendelea na mipango ya nje ya idara ya ufundi na sasa wachezaji wa timu hiyo wamewekewa mzigo wa maana mezsji kama njia ya kuongeza mzuka wa kupata ushindi mbele ya Mazembe.
Matajiri na vigogo hao wamewatamkia mastaa wa Yanga mamilioni mapya katika kuwapandisha mzuka ili wakausake ushindi kesho Kwa Mkapa, baada ya kutofurahishwa na kipigo cha mchezo wa kwanza wa nyumbani dhidi ya Al Hilal uliowatibulia hesabu mapema kabla ya kupoteza tena ugenini kwa MC Alger.
Mwenyekiti wa Kamati ya Mashindano ya Yanga, Rodgers Gumbo, ameliambia Mwanaspoti uongozi wa klabu hiyo unaridhishwa na maendeleo ya mabadiliko ya kikosi chao na sasa wanasubiri kuona timu yao inapata ushindi wa kwanza wa Ligi ya Mabingwa chini ya Ramovic.
Gumbo alisema hawatakaa kusubiria ushindi pekee lakini wamejipanga kuwapa motisha kubwa wachezaji wao ili mechi hizi tatu zilizosalia za makundi wanafanya kweli na kupata ushindi.
“Kiukweli tunaendelea kuona mabadiliko ya kikosi tunaridshishwa na maendeleo lakini bado tunaendelea kusubiri makubwa zaidi tumeshinda mechi za ligi na sasa tunataka kuona tunashinda na mashindano haya ya Afrika tukiwa na kocha wetu,” alisema Gumbo na kuongeza;
“Bado tunaamini tunaweza kutinga robi fainali ingawa haitakuwa rahisi tunatakiwa kushinda hizi mechi tatu kuanzia huu mchezo wa Mazembe maandalizi yanaendelea vizuri sisi viongozi tunajipanga na kila Mwanayanga anajipanga.”
Gumbo alisisitiza kwa kusema; “Hatma yetu kutinga makundi ipo kwenye hizi mechi tatu, uongozi utakuwa na neno zito kwa wachezaji wetu tutawapa motisha mpya kabisa ambayo itawafanya wakafie uwanjani kweli kuanzia mechi hii ya Mazembe, tunataka wahamasike kuusaka ushindi, ahadi hii tutawatamkia kwanza wao kesho (leo Ijumaa) mara baada ya mazoezi yao ya mwisho.
“Tunawaita pia mashabiki wetu, wakaithibitishie Mazembe nguvu yetu kwa kuwapa nguvu wachezaji wetu muda wote wa dakika 90, tunahitaji kuona mashabiki wanafurika uwanja wa Mkapa.”
Yanga ambayo ipo kundi A inashika mkia ikiwa na pointi moja, juu yake ikiwa Mazembe yenye pointi mbili wakati MCL Alger ikishika nafasi ya tatu na pointi zao nne huku Al Hilal Omdurman ikiongoza kundi hilo na pointi zao tiza ikishinda mechi zotre tatu za kwanza.
Yanga inautaka ushindi ili iishushe Mazembe kisha itaifuata Al Hilal ambayo kama ikishinda leo nyumbani dhidi ya MC Alger itafikisha pointi 12 ambazo zitaihakikishia kuongoza kundi hilo hata kama ikipoteza mechi mbili zilizosalia.