Ziara ya Bibi Aisha ni ya kwanza tangu mahusiano ya mataifa hayo mawili kuingia dosari, takribani mwaka mmoja uliopita, baada ya kuwepo kwa mpango wa Ethiopia kutaka kufanya ujenzi wa bandari na kambi ya jeshi la wanamaji katika eneo lililojitenga na Somalia la Somaliland.
Kupitia Shirika la Habari la Uingereza Reuters, Waziri wa Mambo ya Nje waSomaliaAli Omar amethibitisha ziara ya Aisha Mohammed lakini hakusema kile kinachotarajiwa kujadiliwa katika ziara hiyo.
Ijumaa hii katika ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa X zamani Twitter, wizara ya mambo ya nje ya Ethiopia imeandika mataifa hayo mawili yamekubaliana kushirikiana katika mpango mpya amani wa Umoja wa Afrika kwa Somalia (AUSSOM) ulianza rasmi Januari Mosi, pamoja na mahusiano baina ya mataifa hayo.
Ethiopia ina wanajeshi takriban 10,000 wa ulinzi wa amani Somalia
Ethiopia ina wanajeshi takriban 10,000 huko Somalia wenye kusudio la kupambana na wanamgambo wa Al Shabaab lakini Somalia ilitishia kuwaoondoa iwapo Ethiopia haitobatilisha makubaliano yake yaliyofikiwa mwaka mmoja uliopita na Somaliland la ujenzi huo.
Makubaliano hayo yalihusisha Somaliland kukodisha eneo lake la Pwani kwa Ethiopiakwa ajili ya ujenzi wa bandari na kambi ya jeshi la wanamaji ili Ethiopia iweze kuitambua Somaliland kama taifa huru. Somaliland imekuwa na kiasi fulani cha uhuru wake tangu mwaka 1991 lakini uhuru huo bado haujaweza kutambuliwa na taifa lolote hadi wakati huu.
Serikali ya Somalia inaitambua Somaliland kama sehemu yake
Serikali ya Somalia kimsingi inalitambua eneo hilo kama sehemu ya ardhi yake na hivyo kuiita hatua ya makubaliano ya Ethiopia kama uchokozi. Baada ya miezi kadhaa ya juhudi za upatanishi wa kimataifa, hatimae Disemba 11 Somalia na Ethiopia zilifikia makubaliano kufanya kazi pamoja kumaliza tofauti zao katika mazunguzmo yalioratibiwa na Uturuki. Hatua ambayo itafuatiwa na majadiliano ya kitaalamu baina yao ifikapo mwishoni mwa Februari.
Soma zaidi:Ethiopia na Somalia kufanya mazungumzo ya kumaliza mzozo
Wanajeshi wa Ethiopia nchini Somalia wamekuwepo katika ardhi ya taifa hilo kama sehemu ya mpango wa ulinzi wa amani wa Umoja wa Afrika na kwa misingi ya makubaliano ya mataifa hayo. Mamlaka za kikanda zimekuwa katika hofu kwamba kujiondoa kwao kungedhoofisha sana mapambano dhidi ya kundi la al Shabaab, mshirika wa al Qaeda ambalo limekuwa likifanya uasi tangu 2007.
Mzozo huo wa Ethiopia na Somalia kadhalika umeibua wasiwasi kuhusu ukosefu wa utulivu zaidi katika eneo pana la Pembe ya Afrika, huku Somalia ikiijibu Somaliland kwa mpango wake huo kwa kujisogeza karibu na wapinzani wa jadi wa serikali mjini Mogadishu yaani Ethiopia, Misri na Eritrea.