Dar es Salaam. Kamati za Kudumu za Bunge la Jamhuri ya Muungano zinatarajia kuanza vikao vya kuanzia Januari 6 hadi 24, 2025 jijini Dodoma, ambapo pamoja na mengine zitachambua taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali na kuchambua taarifa za uwekezaji wa mitaji ya umma.
Taarifa iliyotolewa na Kitengo cha Mawasiliano na Elimu kwa Umma leo Januari 3, 2025 imesema vikao hivyo vinatangulia mkutano wa 18 wa Bunge unaotarajiwa kuanza siku ya Jumanne Januari 28, 2025.
Taarifa hiyo imesema katika kipindi hicho, Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Sheria Ndogo na Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma (PIC) zitatangulia kuanza vikao Januari 6, 2025, huku Kamati zilizosalia zikianza vikao Januari 13, 2025.
Katika vikao hivyo, kamati mbili zinazosimamia matumizi ya fedha za umma, zitachambua Taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kuhusu Hesabu za Wizara, Mashirika ya Umma na Mamlaka za Serikali za Mitaa zilizokaguliwa kwa Mwaka wa Fedha unaoishia Juni 30, 2023.
“Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma (PIC) itapokea na kuchambua taarifa za uwekezaji wa mitaji ya umma ili kubaini iwapo uwekezaji huo una ufanisi na kwamba, umezingatia taratibu na miongozo mujarabu ya biashara.
Shughuli nyingine zilizotajwa ni pamoja na kuchambua Miswada ya Sheria itakayofanywa na Kamati nne za Bunge ambazo ni Kamati ya Utawala, Katiba na Sheria, Kamati ya Ustawi na Maendeleo ya Jamii, Kamati ya Maji na Mazingira na Kamati ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma (PIC).
Nyingine ni kuchambua Sheria Ndogo itakayofanywa na Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Sheria Ndogo.
“Itafanya uchambuzi wa Sheria Ndogo zilizowasilishwa Bungeni katika Mkutano wa Bunge wa Kumi na Nne na Kumi na Tano.”
Kazi nyingine itakuwa ni kupokea taarifa za utendaji wa Serikali na taasisi zake.
“Kamati 11 za kisekta zitapokea na kujadili taarifa mbalimbali za utendaji wa Serikali na Taasisi zake. Aidha, Kamati ya Bajeti itapokea na kujadili taarifa kuhusu utekelezaji wa Bajeti ya Serikali katika kipindi cha nusu mwaka (Julai – Desemba 2024),” imesema taarifa hiyo.