Mwanza. Dereva wa basi la Kisire linalofanya safari zake kati ya Mwanza na Sirari mkoani Mara, Adam Charles (30) amepandishwa kizimbani na kusomewa shtaka la kuendesha gari kwa mwendokasi na kusababisha majeruhi 21 na uharibifu wa mali.
Katika kesi hiyo ya trafiki namba 188/2025, Charles ameitwa katika Mahakama ya Wilaya ya Magu mkoani humo mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Erick Kimaro na kusomewa shitaka hilo lenye makosa 22.
Akimsomea shtaka hilo leo Ijumaa, Januari 3, 2025, Mwendesha Mashtaka wa Serikali, Nuru Nko ameieleza Mahakama, mshtakiwa pia anakabiliwa na kosa la uharibifu wa mali ambayo ni basi alilokuwa akiendesha gari lenye namba za usajili T229 DST.
Nko ameieleza Mahakama kuwa mshtakiwa akiendesha basi la kampuni ya Kisire Desemba 19, 2024, alisababisha ajali eneo la Kisamba wilayani Magu mkoani humo na kusababisha majeruha kwa abiria 21.
“Mshtakiwa (Charles) ambaye ni Mkazi wa National jijini Mwanza ukiendesha gari kwa mwendokasi na bila umakini ulisababisha ajali na majeraha kwa abiria 21,” ameeleza Nko.
Nko ameieleza Mahakama kuwa mshtakiwa alisababisha majeraha hayo kwa abiria kinyume na kifungu namba 40 na 63 (2) (b) cha Sheria ya Usalama Barabarani Sura ya 168 marejeo ya mwaka 2002.
Kuhusu kosa la kuharibu mali, Nko ameieleza Mahakama hiyo kuwa mshtakiwa alitenda kosa hilo kinyume na kifungu namba 61 na 63(2)(b) cha Sheria ya Usalama Barabarani Sura ya 168 marejeo ya mwaka 2002.
Hata hivyo, mshtakiwa huyo (Charles) amekana kutenda makosa hayo.
“Mheshimiwa Hakimu (Kimaro) upelelezi wa kesi hii umeshakamilika tunaomba tarehe nyingine kwa ajili ya kumsomea mshtakiwa maelezo ya awali (PH) na kuleta mashahidi,” ameeleza Nko.
Baada ya hoja hizo, Hakimu Mkazi Mkuu wa Mahakama hiyo, Erick Kimaro amesema dhamana kwa mshtakiwa iko wazi huku akimtaka kuwa na wadhamini wawili wenye barua ya utambulisho wa Serikali ya Mtaa wanaoishi.
Pia, Kimaro amesema wadhamini hao wanapaswa kusaini dhamana ya maneno ya Sh3 milioni na kuwa na kitambulisho kinachotambulika.
“Mshtakiwa dhamana yako iko wazi, kama unawadhamini wanatakiwa kuwa na barua ya utambulisho na wasaini dhamana ya maneno ya Sh3 milioni,” amesema hakimu Kimaro.
Mshtakiwa ameshindwa kukidhi masharti ya dhamana kutokana na kuwa na mdhamini mmoja pekee ambaye naye hakuwa na barua ya utambulisho iliyokidhi masharti hayo.
Kimaro ameahirisha shauri hilo hadi Januari 16, 2025, litakapoitwa kwa ajili ya mshtakiwa kusomewa maelezo ya awali ya shtaka linalomkabili.