Mawasiliano Same bado baada ya daraja kukatika

Same. Mawasiliano ya barabara kuu ya Same-Mkomazi, wilayani Same, Mkoa wa Kilimanjaro yameendelea kukwama kwa siku ya pili, mamlaka husika zikiendelea kutafuta ufumbuzi.

Mkwamo wa mawasiliano unatokana na Daraja la Mpirani kukatika jana Januari 2, 2025 saa mbili asubuhi kutokana na mvua zinazoendelea kunyesha.

Daraja hilo ndilo kiungo cha kata na makazi ya wananchi wanaoishi katika safu za milima ya Upare.

Akizungumza na Mwananchi leo Januari 3, diwani wa Kata ya Maore, Rashid Juma amesema kukatika kwa mawasiliano ya barabara kumesababisha adha ya usafiri kati ya wananchi wanaoishi nyanda za juu na wanaotoka tambarare.

Amesema kabla ya daraja kukatika mvua zinazoendelea kunyesha ziliaharibu kingo za daraja hilo.

“Daraja limevunjika jana (Januari 2) asubuhi, mpaka sasa ni changamoto ya watu kupita kwenye daraja hili. Kwa sasa barabara imefungwa, hakuna mawasiliano ya pande hizi mbili,” amesema.

Amesema hakuna magari yanayoweza kupita wala pikipiki, ila baadhi ya wananchi wanalazimika kubebwa kuvushwa upande wa pili.

“Watu wanavushwa kwa kubebwa, hakuna chombo chochote cha usafiri kutoka upande wowote kinaweza kupita,” amesema.

Amesema wanachofanya ni kutafuta njia mbadala kwa ajili ya watembea kwa miguu na pikipiki kupita.

“Tanroads (Wakala wa Barabara Tanzania) wako hapa wakishirikiana na wananachi kuona namna njia hiyo inaweza kupatikana kwa haraka ili pikipiki na watembea kwa miguu waweze kupita,” amesema.

Akizungumzia kukatika daraja hilo, Meneja wa Tanroads Mkoa wa Kilimanjaro, Mota Kyando amesema wanaendelea na jitihada mbalimbali kuwezesha kurejesha mawasiliano eneo hilo.

Alisema jana (January 2) kuwa daraja limevunjika kutokana na mvua zilizonyesha kuharibu msingi wa nguzo, hivyo gari lilipopita daraja likakatika.

Kyando alisema mipango iliyopo ni kutumia madaraja ya akiba ya chuma ili kurejesha mawasiliano.

Amesema kwa sasa wanaendelea na jitihada za kutengeneza daraja dogo kuhakikisha wananachi  wanavuka kutoka upande mmoja kwenda mwingine pamoja waendesha pikipiki.

Mvua zilizonyesha usiku wa Desemba 20, mwaka 2024 wilayani Same zilisababisha vifo vya watu sita, nyumba kadhaa kubomoka, kuharibu miundombinu ya barabara na mazao shambani.

Related Posts