Massawe ‘Bwana harusi’ apata dhamana

Dar es Salaam. Mfanyabiashara Vicent Masawe (36) maarufu Bwana harusi, anayekabiliwa na mashtaka ya wizi wa gari na kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu amepata dhamana.

Masawe aliyekula sikukuu za Krismasi na Mwaka Mpya akiwa gerezani baada ya kushindwa kutimiza masharti, amepata dhamana leo Ijumaa Januari 3, 2025 katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu.

Mshtakiwa amedhaminiwa na mke wake, Jackline Mtui na shemeji yake, Mohamed Mkoko.

Wakili wa Serikali Titus Aaron, ameieleza Mahakama mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Beda Nyaki kuwa mshtakiwa amefikishwa mahakamani kutoka rumande kwa ajili ya mahakama kuangalia iwapo ametimiza masharti ya dhamana.

“Mshtakiwa siku ya kwanza alipofikishwa mahakamani hapa Desemba 24, 2024 alishindwa kutimiza masharti ya dhamana, hivyo leo ameletwa ili mahakama iangalie kama amekamilisha masharti ya dhamana ili apate dhamana,” amesema.

Baada ya kueleza hayo, wadhamini wa Masawe walitoa barua na kuziwasilisha mahakamani kwa ajili ya kukaguliwa kama zimekidhi vigezo.

Masharti ya dhamana yaliyotolewa na hakimu Nyaki yalikuwa ni mshtakiwa kuwa na wadhamini wawili wenye vitambulisho vya Taifa watakaosaini bondi ya Sh5 milioni kila mmoja.

Pia mshtakiwa alitakiwa kuwasilisha fedha taslimu Sh9 milioni au mali isiyohamishika yenye thamani hiyo.

Wadhamini walikamilisha masharti hayo na Masawe aliachiwa kwa dhamana. Kesi imeahirishwa hadi Januari 7, 2025 kwa ajili ya kutajwa.

Hadi anaachiwa kwa dhamana, mshtakiwa amekaa mahabusu siku 11, kuanzia Desemba 24, 2024 hadi leo.

Alipofikishwa mahakamani kwa mara ya kwanza Desemba 24, alisomewa mashtaka kwamba Novemba 15, 2024 katika Jiji la Dar es Salaam aliiba gari lenye namba za usajili T 642 EGU aina ya Toyota Ractis lenye thamani ya Sh15 milioni mali ya Silvester Masawe.

Anadaiwa gari hilo aliazimwa na Silvester ili alitumie katika sherehe ya harusi yake lakini baadaye hakulirudisha kama walivyokubaliana.

Shtaka la pili anadaiwa kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu.

Anadaiwa kutenda kosa hilo Novemba 15, 2024 katika Jiji la Dar es Salaam.

Masawe anadaiwa kwa lengo la kuiba na kutapeli, alijipatia fedha taslimu Sh3 milioni kutoka kwa Silvester kwa kujipambanua kuwa atamrudishia fedha hizo baadaye, wakati akijua ni uongo na hakuweza kurudisha fedha hizo hadi alipokamatwa.

Related Posts