Mpanda. Christina Kalilo (8), mwanafunzi wa darasa la tatu katika Shule ya Msingi Uruwila, wilayani Mpanda Mkoa wa Katavi, anadaiwa kujiua kwa kujinyonga kwa kutumia sweta, chumbani kwake.
Inadaiwa chanzo cha kujinyonga ni mawazo baada ya wazazi wake kutomnunulia nguo za sikukuu za Krismasi na Mwaka Mpya.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Januari 3, 2025 Kamanda wa Polisi Mkoa wa Katavi, Kaster Ngonyani amesema jana Januari 2 saa 9 alasiri walipokea taarifa za tukio hilo.
Amesema walipofuatilia eneo la tukio walipata taarifa kwamba baada ya kutonunuliwa nguo mtoto huyo alihuzunika na kuchukua hatua ya kujiua.
Kamanda amewaomba wazazi na walezi kuwatimizia mahitaji muhimu watoto wao yakiwamo ya mavazi, chakula na malazi kwa kuwa ni wajibu wao.
Mama wa mtoto huyo, Matrida Kalibi akizungumza na Mwananchi kwa njia ya simu amesema aligundua mwanawe amejinyonga baada ya kukaa muda mrefu bila kumuona akicheza nje.
Amesema alipoingia ndani alikuta amejinyonga kwa kutumia sweta lake la shule.
Mama huyo amesema hawakumnunulia nguo mpya kwa sababu ya hali duni, vinginevyo angekuwa na fedha angemnunulia.
Wakati huohuo, Polisi imetoa taarifa ikisema Januari hadi Desemba mwaka 2024 watuhumiwa 8,064 wamekamatwa na kufikishwa mahakamani, ikilinganishwa na kipindi kama hicho mwaka 2023, ambao watuhumiwa 7,931 walikamatwa.
Kamanda Ngonyani akizungumza na waandishi wa habari leo Januari 3, amesema watuhumiwa walikamatwa kwa makosa ya ukatili wa kijinsia, uvunjaji, wizi, mauaji, utapeli kwa njia ya mtandao, biashara ya dawa ya kulevya, gongo na matukio ya ukiukwaji wa sheria za barabarani.