Dar es Salaam. Zikiwa zimesalia siku 13 kuelekea uchaguzi wa viongozi wa mabaraza ya Chadema, baadhi ya wagombea wameanza kurejesha fomu.
Wagombea waliorudisha fomu ni Sharifa Suleiman anayewania uenyekiti wa Baraza la Wanawake Taifa (Bawacha) na Glory Tausi anayeomba kuwa naibu katibu mkuu wa Baraza hilo bara.
Hatua ya wagombea hao kurejesha fomu, inatoa nafasi kwa kamati kuu kuketi na kuwapitisha wale itakaowaona wanafaa kuingia kwenye kinyang’anyiro hicho.
Uchaguzi wa viongozi wa nafasi hizo, unaotarajiwa kufanyika Januari 16, 2025, siku nne kabla ya mkutano mkuu Taifa.
Hata hivyo, katika nafasi ya uenyekiti wa Bawacha wagombea wawili waliochukua fomu hawazijarejesha ambao ni Celestine Simba na Suzan Kiwanga.
Msafara wa Sharifa kurudisha fomu, ulianzia katika Viwanja vya Biafra, Kinondoni, Dar es Salaam akiambatana na mamia ya wanawake wafuasi na makada wa Chadema.
Idadi kubwa ya waliokuwepo kwenye msafara huo uliokwenda hadi zilipo ofisi za mabaraza ya chama hicho Kinondoni, walivalia sare za Bawacha.
Shamrashamra na burudani ya muziki vilivyohusisha nyimbo za sifa kwa Chadema, vilikuwa sehemu ya matukio hayo.
Akizungumza baada ya kurejesha fomu, Sharifa amesema hatua yake ya kugombea imetokana na kushawishiwa na viongozi wenzake na wanachama.
Baada ya hatua hiyo, amesema alijadiliana na familia yake na wamekubaliana na hilo.
Amesema anaistahili nafasi hiyo kwa sababu ndiye aliyekuwa akiikaimu tangu mwaka 2020 na amekuwa mwanachama wa Chadema tangu miaka 18 iliyopita.
“Kama mlivyoniomba nami nimeridhia, tutakwenda kujenga baraza lenye umoja, mshikamano na kushajihisha wanawake wagombee katika nafasi mbalimbali za ngazi za maamuzi,” amesema.
Amesema kwa wanaoidai chama hicho kina udini na ukabila wapuuzwe kwa kuwa, amekuwa kiongozi kwa muda mrefu ilhali ni Mzanzibari.
Kwa upande wa Glory, yeye alipokelewa katika ofisi za mabaraza ya chama hicho na kurejesha fomu.