Dar es Salaam. Jeshi la Polisi limeanzisha msako wa kitaifa kumtafuta mtu anayeonekana kwenye video akitangaza kuwa anauza mtoto aliyembeba kwa Sh1.6 milioni.
Taarifa iliyotolewa na Msemaji wa Jeshi la Polisi kutoka Makao Makuu, Dodoma leo Ijumaa Januari 3, 2025, imesema msako huo ni wa kuhakikisha mtuhumiwa anakamatwa na kufikishwa mbele ya sheria ili hatua stahiki zichukuliwe dhidi yake.
Jeshi la Polisi limeeleza kuwa kitendo hicho ni cha kikatili na kinyume na sheria na limekemea vikali tabia hiyo.
Aidha, limewashukuru wananchi wanaotoa taarifa kuhusu matukio kama hayo na kuwahimiza kuendelea kushirikiana na mamlaka katika kupambana na vitendo vya uhalifu, hasa vinavyohatarisha usalama wa watoto.
“Jeshi la Polisi linalaani kitendo hiki na linaomba wananchi kuvilaani na kuvikemea vitendo vya aina hii, kwani vinaweza kusababisha madhara kwa watoto. Ushirikiano wa mapema utawezesha hatua kuchukuliwa kabla madhara hayajatokea,” imeeleza taarifa hiyo.
Jeshi limeahidi kuendelea kushirikiana na jamii ili kuhakikisha usalama wa watoto unalindwa, na kwamba sheria itachukua mkondo wake kwa wahusika wa vitendo vya aina hii.
Katika hatua nyingine Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalumu, Dk Dorothy Gwajima amekemea vikali kitendo cha kijana huyo kutangaza kumuuza mtoto huku akiwaachia polisi wamtafute.
“Watanzania salaam. Kijana huyu anatangaza eti tajiri apeleke Sh1.6 mil mtoto aliyembeba anazo figo 2.
“Baadhi content creator (watengeneza maudhui) kama @jideboy_tz mmefikia hatua mbaya. Nakemea vikali, tayari nimewakabidhi polisi wamtafute huyu, Watanzania tusaidiane kumjua huyu ni nani na aliko,” ameandika Waziri Gwajima.