Mbeya. Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amewaagiza wakuu wa wilaya na mikoa kuharakisha kutenga maeneo kwa ajili ya wananchi kufanya mazoezi kwa lengo la kuwakinga na magonjwa yasiyoambukiza.
Pia, amewataka wakuu wa mikoa kuwaagiza wakuu wa wilaya kupiga marufuku watumishi wa idara ya ardhi kupima na kuuza maeneo ya wazi.
Majaliwa amesema hayo leo Jumamosi Mei 11, 2024 jijini Mbeya wakati akifunga mashindano ya mbio za Mbeya Tulia Marathon 2024 msimu wa nane ambazo yamefadhiliwa na kampuni mbalimbali.
Majaliwa amesema Serikali imekuwa ikitumia gharama kubwa kwa ajili ya magonjwa yasiyoambukiza na ndiyo maana inaongeza bajeti kwa Wizara ya Habari, Sanaa na Michezo ili kuhamasisha jamii.
“Wakuu wa mikoa waagizeni wakuu wa wilaya kutenga maeneo na kutangaza kwa wananchi kwa ajili ya mazoezi ya siku za Jumamosi angalau kwa saa tatu, lengo ni kupunguza tatizo la magonjwa ambayo yanapoteza nguvu kazi kwa taifa kutokana na vifo,” amesema.
Majaliwa ametumia fursa hiyo kumpongeza Spika wa Bunge, Dk Tulia Ackson ambaye pia ni Rais wa Mabunge Duniani (IPU) na kwa ubunifu kupitia taasisi yake ya Tulia Trust kuandaa mashindano hayo.
Amesema fedha zinazopatikana zitatumika kuboresha sekta ya elimu, vifaa na ujenzi wa mabweni.
“Dk Tulia amekarabati mabweni Shule ya Wasichana ya Loleza ambayo alisoma, nitoe wito kwa viongozi wote, rejeeni kwenye shule mlizosoma kuchangia ili kuunga mkono jitihada za jamii na Serikali ya awamu ya sita,” amesema Majaliwa.
Kuhusu ushiriki wa wabunge, Majaliwa amesema wameonyesha mapenzi ya kumuunga mkono Dk Tulia Ackson na kwamba anawahakikishia atarejea tena Mbeya kupiga kambi Jimbo la Mbeya Mjini kumpigia kampeni katika uchaguzi mkuu wa 2025 ili kuunga mkono juhudi zake za kugusa jamii.
“Wabunge leo mmeonyesha heshima kubwa kama Bunge linavyomheshimu Dk Tulia, kuwasha magari yenu kuja kushiriki mbio za Mbeya Tulia Marathon 2024, nina hakika mtamuunga mkono, pia wananchi hawakupoteza kura na wasipoteze kura zao 2025,” amesema Majaliwa.
Amesema jitihada za Dk Tulia ni kutekeleza Ilani ya Uchaguzi na kuwataka wabunge, viongozi wa Chama cha Mapinduzi (CCM) kumuunga mkono ili kumuwezesha kufikia mikakati yake ya kuhudumia wananchi.
Majaliwa ameagiza Wizara ya Maliasili na Utalii, wafanyabiashara, wakuu wa wilaya na mikoa kutumia mashindano ya hisani ya mbio za Mbeya Tulia Marathon msimu ujao kutangaza vivutio vya utalii.
Wakati huohuo, ametoa maelekezo kwa Taasisi ya Tulia Trust kutangaza fursa katika nchi za jirani kama Malawi na Zambia ili kuwezesha ushiriki wa kimataifa kutokana na kuwa chachu ya idadi kubwa ya wanaridha kutoka mataifa mbalimbali nchini.
Kwa upande wake, Dk Tulia amesema fedha zilizopatikana zilielekezwa katika kuboresha miundombinu ya elimu ukiwamo ujenzi mabweni ya wanafunzi wa kike.
Dk Tulia amesema katika msimu huu matarajio ni kwenda kitaifa kwa kujenga kambi ya vijana wanariadha huku wakihitaji eneo lenye ukubwa wa eka 15, lengo ni kuhudumia ndani na nje ya nchi.
Naibu Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Hamis Mwinjuma amesema Watanzania watumie fursa ya mbio za Mbeya Tulia Marathon kujenga afya na kuimarisha uchumi.
Mkuu wa Mkoa, Juma Homera amesema matukio yanayofanywa na Dk Tulia mkoani humo ni fundisho kwa viongozi.
Diwani wa Makogorosi Wilaya ya Chunya, Sophia Mwanautwa amesema huu ni msimu wake wa saba kushiriki na anafanya hivyo kwa lengo la kuchangia kuboresha miundombinu ya elimu na afya.