Kwa nini kipato chako hakilingani na juhudi zako kazini

Dar es Salaam. Si kila mavuno yanaakisi ulichopanda. Kifungu hiki cha maneno kinabeba uhalisia wa maisha ya baadhi ya watu ambao juhudi zao katika kazi wanazofanya hazilingani na matokeo.

Kama umewahi kumwona mtu anayefanya kazi bila kupumzika, kiwango cha juhudi zake kinatazamwa kuwa mfano, lakini hali ya uchumi wake imebaki bila mabadiliko, huo ndiyo muktadha wa andiko hili.

Matumizi ya nguvu kupitiliza si sababu ya kupata zaidi, kitakachoamua matokeo chanya ni mbinu sahihi, kama inavyofafanuliwa na wataalamu wa uchumi.

Akizungumza na Mwananchi jana Januari 3, 2025 mwanazuoni wa uchumi, Profesa Haji Semboja anasema kukosekana matumizi ya mbinu sahihi katika kazi inayofanyika ni sababu ya matumizi ya nguvu nyingi bila faida.

Anasema watu wengi huwekeza katika malengo ya kutumia nguvu, kuliko mbinu.

“Kutumia mbinu za tembo kumuua sisimizi ni matumizi mabaya ya nguvu,” anasema.

Analihusianisha hilo na utendaji wa ngazi ya kitaifa, akisema bila sera sahihi zinazosimamia rasilimali, hakutakuwa na uzalishaji utakaoleta mafanikio.

“Mifumo ya kuondoa umasikini inatakiwa iendane na rasilimali zilizopo nchini, vinginevyo kazi zitafanyika na umasikini utabaki palepale,” anaeleza.

Kwa mujibu wa Profesa Semboja, hoja kubwa si kujishughulisha, bali ni kuelewa jinsi ya kujishughulisha.

Linganisha nguvu na faida

Ni muhimu kabla hujaanza kazi chambua ulinganifu wa gharama itakayotumika na faida inayotarajiwa, kama anavyoeleza Profesa wa uchumi Stephen Kirama.

Uchambuzi huo, anasema unawezesha kujua gharama zinazotarajiwa na faida itakayopatikana, jambo linalotoa mwongozo muhimu iwapo kazi husika inafaa kufanywa au la.

Hata hivyo, anasema gharama na faida hizo zinaweza kuwa za fedha au vinginevyo, muhimu ni kufanya uchambuzi.

Kwa upande mwingine, Profesa Kirama anasema kila kazi hupimwa kwa misingi ya uzalishaji wake na hilo linategemea zaidi nguvu au nishati inayotumika na kiasi cha kipato kinachopatikana.

Anasema uzalishaji hupimwa kwa ufanisi, kadhalika inaangaliwa iwapo kuna uwiano kati ya kinachoingizwa na kinachotolewa.

“Kilicho bora ni kuhakikisha gharama inayotumika ni ndogo huku kinachozaliwa ni kikubwa zaidi,” anasema.

Kinachowaponza wengi, anasema wamekosa mipango madhubuti, hivyo hufanya kila kitu kwa kufuata mkumbo.

“Wakisikia kilimo kinalipa, wanaanza kulima. Wakisikia Uber inalipa, wanahamia Uber,” anasema.

Mwanazuoni mwingine wa uchumi kutoka UDSM, Julieth Julius anasema kuna uhusiano wa aina ya shughuli na kiwango cha kipato.

Kwa mujibu wa Julius, baadhi ya shughuli kipato chake ni kidogo kiasi kwamba hata akijishughulisha kiasi gani, huoni mabadiliko ya kiuchumi katika maisha.

“Hawa ndiyo wale watu wanaoitwa ‘cheap labor’ (vibarua), anafanya kazi kubwa anapata kiasi kidogo cha fedha, yaani malipo yao ni madogo hayalingani na ukubwa wa kazi,” anasema.

Mwanazuoni huyo anasema msingi wa tatizo ni kiwango cha elimu walichonacho wanaofanya shughuli hizo, akitoa mfano wa wafanyakazi wa kazi za nyumbani.

“Unakuta dada wa kazi anafanya kazi nyingi za ndani kutwa nzima, lakini ndio watu wenye mishahara midogo, kwa hiyo juhudi au kufanya kazi kwake hakumfaidishi,” anaeleza.

Hata hivyo, anapendekeza Serikali iweke kima cha mshahara kwa aina mbalimbali ya kazi ili kila shughuli iwe na manufaa kwa anayeifanya.

Kwa mujibu wa machapisho mbalimbali kupitia mitandao ya kijamii, yameainishwa mambo 10 yanayoweza kusababisha mtu afanye juhudi kubwa katika kazi lakini asipate mafanikio

Mojas ya mambo hayo ni ukosefu wa malengo mahususi, yaliyo wazi na yanayoweza kupimika, hivyo ni muhimu kuwa na malengo yanayoweza kufikiwa.

Pili, ni ukosefu wa mpango wa kufanya kazi, tatu ni kukosa maarifa au ujuzi sahihi. Hivyo, ni muhimu kuinua kiwango cha ujuzi kupitia mafunzo, kozi au kusoma vitabu vinavyohusiana na kazi husika.

Nne ni mazoea au mbinu zinazokosewa. Cha kufanya ni tathmini ya njia unazotumia na kutafuta mbinu bora kutoka kwa wataalamu au watu wengine waliofanikiwa.

Jambo la tano ni kutokuwa na mtandao wa watu sahihi na sita ni kukata tamaa haraka. Ni muhimu kuwa na uvumilivu na kujifunza kutokana na changamoto.

Saba ni kutokujifunza kutokana na makosa. Ili kukabiliana na hilo, fanya tathmini kwa kila hatua unayochukua na kujifunza kutokana na makosa.

Jambo la nane ni mazingira yasiyofaa ya kazi kama vile ukosefu wa rasilimali au usaidizi wa kutosha. Hivyo, kuboresha mazingira ya kazi au kutafuta nafasi zinazokidhi mahitaji ni jambo la muhimu.

Ukosefu wa kujitunza ni jambo la tisa ambalo kutokana na uchovu wa mwili au akili unaweza kupunguza uwezo wa kufanikisha malengo. Ni muhimu kupumzika, kula vizuri na kufanya mazoezi.

Jambo la 10 ni matarajio yasiyo ya kweli. Kuna haja ya kuwa mkweli kuhusu uwezo wako na kuongeza juhudi kwa awamu zinazowezekana.

Related Posts