‘Nyoka mstaarabu’ alivyoibua jina kisima cha kihistoria Dodoma

Dodoma. Yapo maeneo kadhaa katika Jiji la Dodoma ambayo yamebaki kuwa majina tu katika historia.

Hiyo ni kwa sababu ya miundombinu ya barabara kupita na hivyo kuyapunguzia umaarufu wake wa zamani. Maeneo hayo inawezekana hujawahi kuyapita, lakini umewahi kuyasikia na ungependa kufahamu nini kilisababisha kuitwa kwa majina hayo.

Kisima cha Nyoka, Chang’ombe na Makulu ni miongoni mwa maeneo yaliyobeba historia ya Jiji la Dodoma tangu ukoloni.

Akizungumza na Mwananchi, Mwenyekiti wa Mtaa wa Mazengo, Abdallah Mtosa, anasema yeye alihamia katika eneo hilo miaka ya 1980 na kukikuta Kisima Nyoka ambacho kilikuwa kikitumiwa na watu kuchota maji.

Anasema miaka hiyo katika eneo hilo hakukuwa na maji safi ya kuchota, kutokana na mfumo wa maji wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dodoma (Duwasa) kutofika hapo.

Mtosa anasema wakati huo maji safi ya bomba yalikuwa yamefikishwa katika Kata ya jirani ya Chamwino, hali iliyowafanya kutegemea kwa kiasi kikubwa kisima hicho.

“Sasa ilikuwa ukienda asubuhi ama mchana mle ndani ya kisima ulikuwa ukimkuta nyoka ambaye hana madhara kwa jamii. Ukifika nyoka yule alikuwa akitoka kwenye kisima na kuhamia katika pango pembeni hadi hapo unapomaliza kuchota maji,” anasema.

Anasema kutokana na uwepo wa nyoka huyo kila wanapokwenda kuchota maji, watu walikipachika jina kuwa ni kisima cha nyoka hadi leo eneo hilo linajulikana kwa jina hilo.

Anasema kutokana na mabadiliko ya kiteknolojia, hivi sasa mahali palipokuwa na kisima hicho imejengwa barabara ya lami ambayo inatokea Wajenzi kwenda Nkhungu.

“Ukifika njiapanda ya barabara inayokwenda Shule ya Hijira ndipo kulikuwa na kisima hicho ambacho kimefukiwa kutokana na mabadiliko ya miundombinu ya barabara,” anasema.

Mtosa anasema kisima hicho kilikuwepo tangu miaka ya 1970 hadi 2010, ulipoanza ujenzi wa barabara hiyo ya lami ambapo kilifukiwa ili kupisha ujenzi huo.

Alipoulizwa sifa nyingine ya kisima hicho, Mtosa anasema maji yake yalikuwa safi kwa kuwa yalitokana na mwamba uliopita eneo hilo na hayakuwa na chumvi.

“Anasema sababu hiyo ndiyo ilifanya watu wengi kwenda kuchota kwa ajili ya matumizi ya nyumbani. Kisima hicho kilikuwa kikitumiwa na watu wa Kata ya Chang’ombe na majirani wa Kata ya Chamwino.

Anasema kwa kufukia kisima hicho na kujenga barabara ya lami na daraja kumepoteza alama ya uwepo wa kisima hicho cha kihistoria.

“Nawashauri wakati wa mabadiliko ya teknolojia, wanaohusika wajaribu hata kuchepusha ili kuendelea kutunza maeneo yetu ya kumbukumbu,” anasema.

Anasema kabla ya kufukiwa kisima hicho, watu wa Idara ya Maji na Afya walikuwa wakifika na kuchukua maji kwa ajili ya tafiti zao za ubora wa maji hayo.

Alipoulizwa iwapo nyoka huyo aliwahi kuleta madhara kwa watu waliokuwa wakienda kuchota maji, Mtosa anasema hajawahi kuleta madhara kwa watu ambao walikuwa wakienda kuchota maji.

Anasema walianza kusogeza udongo, hali iliyosababisha kisima kuanza kuwa finyu, nyoka huyo alipotea katika mazingira anayoyajua mwenyewe Mwenyezi Mungu na hatukumuona tena.

“Ina maana hakudhuriwa kwa kuuawa, bali nyoka alipotea katika mazingira ambayo hatuyajui, lakini hakuna mtu aliyemuua wakati wa ujenzi wa barabara hiyo,” anasema Mtosa.

Mzee Yusuph Hassan ambaye alianza kuishi katika eneo hilo mwaka 1960, anasema kuwa ilikuwa ni nadra sana kumuona nyoka huyo.

“Ilikuwa ni nadra sana kumuona nyoka huyo, unaweza kumkuta ametoa kichwa na wewe unapishana naye, bila kukudhuru,” anasema.

Anasema hawajawahi kumuona nyoka huyo akitoka nje ya kisima, labda kama alikuwa akitoka usiku wakati ambapo watu wamelala.

Hassan, kama ilivyo kwa wengine, anasema kuwa haijulikani nyoka huyo alikwenda wapi baada ya barabara hiyo kujengwa na kukifukia kisima hicho.

Asili ya jina la Chang’ombe

Kwa upande wa jina Chang’ombe, Mtosa anasema jina hilo lilitokana na eneo kuwa na wafugaji wengi wa ng’ombe ambao walikuwa wakipita wakiwa wanaswaga mifugo kupeleka minadani.

“Kulikuwa na nyumba moja ambayo ilikuwa inaitwa milango mitatu, hapo ndipo walipochinja ng’ombe, baada ya hapo watu waliokuwa wakitoka vijijini huko walikuwa wakielekezwa pale Chang’ombe,” anasema.

Anasema baada ya hapo ikazoeleka akilini mwa watu, wakitaka kuelekeza wageni wanaambiwa nenda pale Chang’ombe, yaani pale palipochinjwa ng’ombe.

Kwa mujibu wa mipango miji ya Halmashauri ya Wilaya ya Dodoma, eneo hilo lilitanuka na kupewa hadhi ya kuwa kata.

Siri maeneo yenye neno Makulu

Akizungumzia maeneo yenye neno Makulu jijini Dodoma, Chifu Lazaro Chihoma anasema miongoni mwa sifa ya maeneo yenye neno makulu jijini Dodoma ni yale yaliyokuwa na nyumba nyingi za zinazomilikiwa na mtemi wakati wa ukoloni.

“Unajua Mtemi alikuwa hana mke mmoja, sasa zile nyumba ndio zilikuwa zikiitwa Makulu, halafu ana miji mikubwa ambayo ilikuwa na watemi,” anasema.

Chihoma anataja sifa nyingine ya Makulu ni kuwa walikuwa wakikusanyika machifu wengi mahali hapo kwa ajili ya kufanyia mikutano.

“Hapa anakusanya utemi mwingi kutoka maeneo tofauti ya Mkoa wa Dodoma na maeneo mengine kulikuwa na mabaraza ambayo yanakusanya watemi wengi,” anasema.

Hata hivyo, Chihoma anasema zipo himaya nyingine za watemi zilibakia kuwa ni himaya bila kupewa majina ya makulu.

“Hizi ni zile ulizokuta zina msaidizi wa mtemi, karani (mlugaluga ambaye hivi sasa mnasema mtendaji) na mgambo ambaye aliitwa mkatikilo (mgambo wa Ikulu),” anasema.

Baadhi ya maeneo ambayo yamepewa majina yenye neno makulu ni Mahoma Makulu, Bahi Makulu, Mvumi Makulu, Dodoma Makulu na Hombolo Makulu

Related Posts