Dar es Salaam. Mwaka 2024 Tanzania ilikubwa na jinamizi la ajali za barabarani, Desemba ukiwa kinara.
Ni kutokana na ajali hizo, Mamlaka ya Udhibiti Usafiri wa Ardhini (Latra) imekuja na mpango maalumu ukiwalenga wamiliki na madereva wa mabasi maalumu ya kukodi (Special hire) ambayo mengi ni Toyota Coaster.
Hatua ya Latra inatokana na tathimini iliyofanya Desemba inayoonyesha katika ajali sita zilizosababisha vifo vya watu saba hadi 15, ni moja pekee imehusisha basi kubwa huku tano zikihusisha mabasi hayo madogo (Special hire).
Rais Samia Suluhu Hassan akitoa salamu za Mwaka Mpya kwa Watanzania Desemba 31, 2024 alisema:
“Takwimu za Jeshi la Polisi Tanzania zinaonyesha kati ya Januari hadi Desemba mwaka huu, nchi yetu ilishuhudia jumla ya ajali 1,735. Ajali 1,198 kati ya hizo zilisababisha vifo vya ndugu zetu 1,715.
“Hii ni idadi kubwa sana. Ndugu zetu wengine 2,719 walijeruhiwa katika ajali za barabarani. Asilimia 97 ya ajali hizi zimetokana na makosa ya kibinadamu, kubwa kabisa ikiwa uzembe wa madereva, uendeshaji hatari na mwendo kasi ambayo kwa pamoja ni asilimia 73.7 ya ajali zote,” alisema.
Aliwataka Wizara ya Mambo ya Ndani na Jeshi la Polisi kuongeza mikakati ya kuzuia ajali zinazosababishwa na makosa ya uzembe.
Kwa mujibu wa kanuni ya 20(b) ya Kanuni za Latra za magari ya kukodi za mwaka 2020, Special hire yanapaswa kuunganishwa na Mfumo wa Kufuatilia Mwenendo wa Magari (VTS).
Mfumo huo huwezesha mamlaka kumtambua dereva anayeendesha gari husika endapo atasajiliwa na kutumia kitufe cha utambuzi wa dereva (i-button).
Kanuni ya 9(2) ya uthibitishaji madereva na usajili wahudumu wa vyombo vya moto kibiashara, Latra ina jukumu la kuainisha magari yanayopaswa kutumia kitufe cha utambuzi wa dereva ambapo mabasi maalumu ya kukodi ni miongoni mwa magari yaliyoainishwa.
Pia, kanuni ya 9 (3) inamtaka dereva aliyepewa kitufe cha utambuzi kuhakikisha kiko salama na kutompatia mtu mwingine yeyote.
Mkuu wa Kitengo cha Uhusiano na Mawasiliano Latra, Salum Pazzy, Januari 3, 2025 alisema kumekuwa na udanganyifu kwa magari ya Special hire kupakia abiria kwa kisingizio cha uhaba wa huduma ya usafiri Desemba.
Alisema mabasi hayo yanayopewa leseni maalumu hayaruhusiwi kubeba abiria mmoja mmoja bali kwa kukodiwa.
“Hawa wamekuwa wakibeba abiria kama mabasi makubwa tofauti na masharti ya leseni zao zinazowataka kukodiwa, lakini wamekuwa wakibeba abiria kwa kisingizio kulikuwa na uhitaji mkubwa wa huduma ya usafiri,” alisema.
Pazzy alisema wameanzisha operesheni maalumu ya kimkakati ya kuweka vituo njiani yanakopita magari hayo kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi Kikosi cha Usalama Barabarani na mafundi wao.
“Ili kurahisisha kazi hiyo, mamlaka itafanya usajili wa vitufe vya utambuzi wa dereva kwenye baadhi ya maeneo ya barabara ambayo mabasi husimama,” alisema.
Pazzy alisema wengine wamekuwa wadanganyifu kwenye VTS, ambao wamekuwa wakiwafuatilia na kuwachukulia hatua waliokiuka sheria na kuwatoza faini.
“Kwa kufanya hivi tunaamini itatuongezea hali ya usalama wa abiria na kuboresha ufanisi wa utumiaji wa huduma hizi za usafiri,” alisema.
Latra imewakumbusha madereva na wamiliki wa mabasi hayo ya kukodi kuzingatia matumizi sahihi ya kitufe, ikiwataka wasionacho kufika ofisi za mamlaka zilizo karibu ili kusajiliwa na kuunganishwa kabla ya Januari 12, 2025.
Dereva wa gari hizo za kukodi, Habibu Ramadhani akizungumza na Mwananchi amesema hawana elimu ya matumizi ya kitufe.
“Tunapokutana na Latra wakikagua wakiona haujabonyeza kitufe wanakuandikia kwa sababu haionyeshi ni nani anaendesha gari wakati huo hata ukijitetea umebonyeza hawaelewi kwa kuwa haionyeshi ishara kama umeingia au umetoka,” amesema.
Amesema kabla ya kuingia kwenye mfumo walitakiwa kupatia elimu.
Mwenyekiti wa madereva wa magari hayo, Eustack Msoka amesema wanaungana na Latra katika kupunguza ajali na kuamua kutembea na mwendo wa kilomita 80 kwa saa.
“Watu wanachoshindwa kuelewa asilimia kubwa ya magari yetu tunabeba familia moja, hivyo ni ngumu mtu kuamua kupoteza watu wa familia moja kwa sababu ya haraka,” amesema.
Amesema Latra wamekuwa wakitoa elimu kwa madereva kwenda kusoma na kufanya mitihani, jambo wanaloliona ni la muhimu katika kupunguza ajali.
Amesema kuwepo mfumo wa VTS na vitufe vya utambuzi wa dereva kutasaidia kwa kiasi kikubwa kupunguza ajali, akishauri ufuatiliaji pia ufanyike kwa madereva wa malori.
“Sina uhakika kama malori yanafuatiliwa kama sisi maana wangefanya hivyo wangepata kiini cha ajali zinazotokea,” amesema.
Kuhusu kupakiza abiria mmoja mmoja, amesema kinachofanyika ni kuwa waliokodi huruhusu wao kuongeza watu wanapoona kuna haja lakini si kuingia kituoni na kuanza kupiga debe.
“Tunakodiwa kutoka Dar kwenda Bukoba na watu 15, kwa kuwa nafasi zinakuwepo waliokodi wanakwambia unaweza kuchukua watu wawili au watatu ili kupata zawadi ya kurudi nayo nyumbani,” amesema.