Dar es Salaam. Baraza la Mitihani la Tanzania (Necta) limetangaza matokeo ya upimaji wa kitaifa wa darasa la nne na kidato cha pili, takwimu zikionyesha kwa darasa la nne wasichana wamefaulu zaidi ikilinganishwa na wavulana. Kwa kidato cha pili wavulana ndio wameongoza.
Matokeo yametangazwa leo Januari 4, 2025 na Katibu Mtendaji wa baraza hilo, Dk Said Mohamed, mbele ya waandishi wa habari.
Akitangaza matokeo ya darasa la nne, Dk Mohamed amesema wanafunzi 1,320,227 kati ya 1,530,805 wenye matokeo sawa na asilimia 86.24, wamefaulu kuendelea na darasa la tano mwaka 2025 kwa kupata madaraja A,B,C na D.
Amesema matokeo hayo ni tofauti na mwaka 2023 ambao wanafunzi waliofaulu walikuwa 1,287,934 sawa na asilimia 83.3.4, hivyo kuwa na ongezeko la ufaulu kwa asilimia 2.9 kwa wanafunzi waliopata fursa ya kuendelea na darasa la tano ikilinganishwa na mwaka 2023.
Kutokana na matokeo hayo, Dk Mohamed amesema kati ya wanafunzi waliofaulu kuendelea na darasa la tano, wasichana ni 699,901 sawa na asilimia 87.75 na wavulana ni 620,326 sawa na asilimka 84.61.
Kwa upande wa kidato cha pili, amesema wanafunzi 680,574 kati ya 796,825 wenye matokeo ambayo ni sawa na asilimia 85.41 wamefaulu kuendelea na kidato cha tatu ambao wamepata madaraja ya 1, 2,3 na 4 huku wavulana wakiongoza.
Amesema hii ni tofauti na mwaka 2023 ambapo wanafunzi waliofaulu walikuwa 592,741 sawa na asilimia 85 na kufanya ufaulu kuongezeka kwa asilimia 0.1.
Kwa matokeo hayo, amesema kati ya wanafunzi 680,574 waliofaulu kuendelea na kidato cha tatu, wasichana ni 367,457 na wavulana ni 313,117.
Endelea kufuatilia Mwananchi.