KAMA wewe ni mpenzi na shabiki wa Simba, basi tegemea kuona maajabu zaidi kutoka kwa kiungo mshambuliaji, Jean Charles Ahoua hasa kwa mechi za kimataifa, baada ya kocha Fadlu Davids kueleza mipango ya kumchorea ramani mpya ili azidi kufunika.
Kiungo huyo raia wa Ivory Coast anayeichezea Simba msimu wa kwanza akisajiliwa kutoka Stella Club d’Adjam huku akiongoza kwa mabao na asisti katika kikosi – akifunga saba na kuasisti tano katika Ligi Kuu Bara, lakini hajafanya makeke katika Kombe la Shirikisho Afrika akifunga moja na asisti moja.
Ahoua alifunga bao lililoipa Simba ushindi wa kwanza wa Kundi A dhidi ya Bravos, kisha akaasisti katika ushindi wa 2-1 dhidi ya CS Sfaxien akimsetia Kibu Denis aliyefunga bao la kusawazisha.
Akizungumza na Mwanaspoti, Fadlu alisema ingawa Ahoua ameanza vizuri katika ligi, lakini sasa anatakiwa kutanua namba alizonazo hadi kwenye michuano ya CAF, ambapo Simba kesho itakuwa ugenini kurudiana na Sfaxien jijini Tunis, Tunisia.
Alisema Ahoua hajachangamka katika mashindano hayo ambayo anaamini kama ataongeza kasi basi timu hiyo itafanya makubwa zaidi.
“Nimeshakaa naye na kuzungumza ili kutengeneza mipango mipya ya namna gani anatakiwa kuinuka haraka kwenye mechi za Afrika, kwani kutampa faida yeye na hata timu kwa ujumla,” alisema Fadlu.
“Sasa ni zamu ya kimataifa tayari katika ligi ameonyesha makali yake, kimataifa tunatakiwa kufanya vizuri na kujihakikishia nafasi kwa kupata matokeo, hivyo wachezaji wote wanatakiwa kuwa na viwango bora ili kuvuka.” Mabao saba alimefunga Ahoua kwenye mechi 14 kati ya 15 ilizocheza Simba za ligi akitumia dakika 957, matatu ni ya penalti, moja la friikiki na mengine matatu ya muvu za kawaida, huku akiwa ni mmoja ya washambuliaji tegemeo Simba.