Na John Walter -Babati
Mbunge wa Jimbo la Babati Vijijini na Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mheshimiwa Daniel Sillo, ameweka jiwe la msingi la ujenzi wa mradi mkubwa wa maji katika Kata ya Arri.
Mheshimiwa Sillo ameweka jiwe hilo la msingi leo Januari 3,2025, ambao unatekelezwa chini ya usimamizi wa Wakala wa Usambazaji Maji safi na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) Wilaya ya Babati, ukikadiriwa kugharimu jumla ya shilingi bilioni 2.482.
Mfadhili mkuu wa mradi ni shirika la Karim Foundation, ambalo limechangia kiasi kikubwa cha fedha, huku wananchi wa eneo hilo wakichangia shilingi milioni 128.
Sillo amesema hayo ni matokea na matunda ya kazi nzuri inayofanywa na Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kujenga mahusiano mazuri na sekta binafsi na mataifa mbalimbali duniani.
Akizungumza wakati wa hafla hiyo, Meneja wa RUWASA Mkoa wa Manyara, James Kionaumela, ameipongeza Karim Foundation kwa moyo wao wa upendo na msaada mkubwa kwa wakazi wa Babati.
Amebainisha kuwa mradi huo utaongeza upatikanaji wa maji safi na salama mkoani Manyara, ambapo kwa sasa vijijini ni asilimia 71 na mijini asilimia 83.
Mradi huo ambao kwa sasa umeanza kutoa maji, unahudumia vijiji saba vilivyoko katika Kata ya Arri, na hivyo kuondoa adha ya kutembea umbali mrefu kwa ajili ya kutafuta maji.
Kwa upande wake, Katibu wa Umoja wa Vijana wa Chama cha Mapinduzi (UVCCM) Wilaya ya Babati, George Sanka, amesema kuwa utekelezaji wa mradi huo unaendana na Ilani ya CCM ya 2020-2025, na kwamba wanaridhika na juhudi za Serikali katika kuboresha huduma kwa wananchi.
Mkurugenzi wa Karim Foundation Tanzania, Shau Erro Ae, amesisitiza dhamira ya shirika hilo kuendelea kushirikiana na Serikali na wadau wengine katika kuhakikisha huduma muhimu zinawafikia wananchi.
Wananchi wa Kata ya Arri walimshukuru Mheshimiwa Daniel Sillo na Karim Foundation kwa juhudi zao, wakisema mradi huo wa maji utakuwa suluhisho la changamoto kubwa waliyokuwa wanakabiliana nayo kwa muda mrefu.
Aidha walionyesha shukrani zao kwa hatua hiyo, wakieleza kuwa mradi huo utaboresha maisha yao kwa kiwango kikubwa.