MABOSI wa Tabora United wapo katika hatua za mwisho kukamilisha usajili wa kipa namba moja wa timu ya taifa ya Gabon, Jean-Noel Amonome.
Kipa huyo wa zamani wa Amazulu ya Afrika Kusini na AS Arta Solar ya Djibouti ujio wake utaongeza ushindani dhidi ya Hussein Masalanga ambaye ndiye kipa namba moja kwa sasa na Haroun Mandanda.
Chanzo cha kuaminika kutoka Tabora United kimeliambia Mwanaspoti kuwa, uongozi umesafiri kumalizana na kipa huyo ambaye wanaamini ataongeza nguvu kikosini
“Ni kweli mchakato wa kumalizana na kipa huyo unaendelea vizuri na upo kwenye hatua nzuri kwani tayari mazungumzo ya pande zote mbili yapo kwenye hatua za mwisho za ukamilishaji,” alisema mtoa taarifa na kuongeza:
“Ujio wake utaongeza chachu ya ubora wa timu yetu sambamba na kuimarisha ukuta ili tuweze kufikia mafanikio tunatakiwa kuwa bora kila eneo tuna imani kubwa na kipa huyu ambaye ni namba moja timu ya taifa ya nchi yake.”
Mtoa taarifa huyo aliongeza kuwa bado wanaendelea kuimarisha kikosi kutokana na ripoti ya kocha Anicet Kiazayid ambaye amewataka kuongeza nguvu kikosini dirisha hili la usajili. Ilielezwa kocha huyo aliweka wazi anahitaji mshambuliaji mmoja, viungo watatu, beki na kipa ili kuongeza nguvu zaidi katika kikosi hicho kwa ajili ya mechi za duru la pili ambalo ni la lalasalama kila moja ikipambana kujihakikishia kucheza tena ligi msimu ujao.