Unguja. Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (Tasaf) katika utekelezaji wa afua mbalimbali, umehitimisha kaya za walengwa 400,000 nchi nzima, kati ya hizo 22,400 zinatoka Zanzibar.
Mkurugenzi Mtendaji wa Tasaf, Shedrack Mziray amesema hayo kwenye uzinduzi wa Kituo cha Afya Kinyikani, Pemba kilichojengwa na mfuko huo.
“Kaya hizi baada ya kuhudumiwa na mpango kwa takribani miaka 10, zimeboresha maisha, kuongeza rasilimali na zinaweza kuendelea kuendesha maisha yao bila ruzuku ya Tasaf. Haya ni mafanikio makubwa na ya kujivunia ambayo yanaashiria matokeo chanya ya utekelezaji wa mpango,” amesema leo Januari 4, 2025.
Amesema katika kusaidia kutatua changamoto zinazowakabili wananchi Zanzibar, Tasaf katika kipindi cha pili cha mpango imetoa fedha kwa ajili ya ujenzi wa miradi 15 ya kuendeleza miundombinu katika sekta za elimu, afya na maji ambayo imegharimu zaidi ya Sh3.1 bilioni.
Katika mamlaka ya eneo la utekelezaji Pemba, kwa mwaka 2024, amesema Tasaf inatekeleza miradi saba yenye thamani ya Sh1.32 bilioni.
Miradi hiyo amesema inahusisha sekta tofauti, ikiwemo afya ambayo miongoni mwa miradi yake ni ujenzi wa Kituo cha Afya cha Kinyikani kilichozinduliwa.
Amesema miradi miwili ambayo ni ujenzi wa Kituo cha Afya Kendwa na madarasa katika shule ya Piki ilikwishakamilika na sasa imeanza kutoa huduma kwa wananchi.
Kwa upande wa Zanzibar mpango wa kunusuru kaya masikini ulianza kutekelezwa mwaka 2013 na unaendelea hadi sasa, jumla ya kaya 56,713 kutoka shehia zote 388 zimefikiwa hadi Novemba 2024.
Tasaf imehawilisha ruzuku ya Sh50.1 bilioni kwa kaya hizo Unguja na Pemba.
Akizungumza katika ufunguzi wa kituo hicho ikiwa ni shamrashamra za miaka 61 ya Mapinduzi, Spika wa Baraza la Wawakilishi, Zubeir Maulid, amesema utekelezaji wa mpango wa kunusuru kaya masikini ni miongoni mwa matunda ya Mapinduzi ambayo yanaendelea kunufaisha Taifa.
“Mpango huu umekuja kwa dhamira ileile ya Serikali ya kuondoa umasikini wa kipato, kuimarisha huduma za afya na elimu, sambamba na kutoa fursa mbalimbali za stadi za maisha kupitia vikundi vya wajasiriamali,” amesema.
Amesema hawana budi kujivunia matunda yaliyopatikana baada ya Mapinduzi na kuendelea kuyatunza kwa hali na mali kwani kabla ya Mapinduzi huduma za afya na elimu zilikuwa zikitolewa kwa matabaka na kwa watu maalumu, hivyo wengi waliachwa bila kupata haki hizo za msingi.
“Ni faraja kubwa leo hii tunafungua mradi wetu wa ujenzi wa kituo cha afya ili wananchi muweze kupata huduma bora za matibabu na kuwapunguzia masafa hasa kina mama na watoto ambao hutembea masafa marefu kuzifuata huduma za afya ya mama na mtoto, huduma za maabara, chanjo na nyingine muhimu,” amesema.
Amewataka wananchi kutunza mradi huo ili uweze kuhudumia vizazi vijavyo.