ABIRIA WATAKIWA KUKATA TIKETI KWA KUTUMIA MFUMO WA KIDIGITALI

Na Mwandishi Wetu,  Dodoma. 

Abiria wametakiwa kuwajibika kwa kuhakikisha wanakata tiketi zao kwa kutumia mfumo wa kielektroniki ili kupunguza changamoto ambazo wamekuwa wakikumbana nazo hasa wakati wa kusafiri.

Hayo yameelezwa leo Januari 4,2025 Jijini Dodoma na Koplo Esther Makali kutoka Ofisi ya Mkuu wa kikosi cha usalama barabarani mkoa wa Dodoma, Dawati la Elimu kwa Umma, wakati akitoa elimu kwa abiria na madereva waliokuwa wakisafiri kwenda mikoani kupitia stendi ya Mabasi Nanenane.

“Ni lazima abiria uwe na tiketi mtandao usikubali kupewa tiketi kwa mkono tiketi ya mkono kwasasa hazikubaliki na sasa hazina matumizi tumeshaelekezana na tunaendelea kukumbushana kila siku kwamba sasa hivi tunahitaji tiketi mtandao,”amesema.

Amesema tiketi hizo zipo katika mfumo na zinajulikana hivyo ni rahisi kwa bairia kuweza kupata m,saada pale anapokutana na changamoto yoyote ambapo pia amewasisitiza abrira kuhakiki taarifa zinazojazwa kwenye hiyo tiketi ili kuondoa mkanganyiko na sintofahamu inayoweza kujitokeza wakati wa safari.

Koplo Esther pia ameendelea kuwakumbusha abiria anapokuwa safarini kuhakikisha anatiketi ya kampuni ya gari husika na imejazwa taarifa zake vyema kwa maana ya jina la kampuni ya basi, jina la abiria, nauli husika na namba ya siti anayokwenda kukaa.

Kwa upande wake Balozi wa usalama barabarani Tanzania kanda ya kati Dodoma Petro Edward amesema lengo kuu la kutoa elimu hiyo ni kuendelea kuwakumbusha abiria na madereva wajibu wao na kufuata sheria za usalama barabarani.

“Ni kwamba hii elimu ni kwaajili ya abiria ili wapaze sauti pamoja na madereva ili kuweza kufuata sheria, taratibu na kanuni za usalama barabarani na kwamba tusipofanya wataendelea kufanya makosa ya mara kwa mara na kuweza kusababisha ajali kama ambavyo tumekuwa tukishuhudia hususani kipindi hiki cha msimu wa kusafiri,”amesema.

Ameongeza kuwa katika elimu waliyoitoa siku ya leo ni pamoja na kuwatahadharisha abiria kuwa makini na watu wanaokuwa wamepanda nao kwenye magari kwani wapo baadhi yao ni wezi na wanakuwa na madawa ya kulevya hivyo wawe makini na zawadi za vyakula na vinywaji wanavyopewa na watu wasiowajua.

Nao baadhi ya madereva wameendelea kuwakumbusha madereva wenzao kuwa makini hasa wawapo barabarani hususani katika kipindi hiki cha mwanzo wa mwaka ambapo magari ni mengi njiani.

“Tunaomba madereva wenzetu tuwe makini tunapokuwa barabarani na kuhakikisha tunazingatia sheria za usalama barabarani kwasababu kipindi huiki cha mwanzo wa mwaka barabarani kluna magari mengi watu wanasafiri kwa wingi kutoka sehemu moja kwenda sehemu nyingine kwahiyo hapa klazima tuongeze umakini na kuhakikisha tunafika salama,”wamesema.

Related Posts