Las Vegas. Shirika la Upelelezi la Marekani (FBI) ikimtaja Matthew Livelsberger, kuwa mtu aliyefariki ndani ya gari aina ya ‘Tesla Cyber truck’ iliyolipuka nje ya hoteli maarufu ya Trump jijini Las Vegas, polisi nao wamesema ni tukio la kujitoa muhanga.
Tukio kilo lilitokea zikiwa zimepita saa chache tangu, tukio lingine la dereva wa gari aina ya Pickup kugonga na kuwaua watu 15 jijini New Orleans nchini Marekani wakati wa mkesha wa mwaka mpya.
Hata hivyo, FBI wamesema matukio hayo hayana uhusiano.
“Hadi sasa hakuna usahidi kwamba haya matukio yote mawili yana uhusiano wa aina yoyote,” alisema Mkuu wa Kitengo cha FBI jijini Las Vegas FBI, Spencer Evans.
“Hatua za kiuchunguzi na taarifa za ndani ya Jeshi la Marekani zinaonyesha kuwa alikuwa anasumbuliwa na tatizo la afya ya akili, pia tumebaini kuwa kulikuwa na changamoto za kifamilia zilizokuwa zikimsumbua na kusababisha tatizo hilo,” alisema Evans.
Ripoti ya uchunguzi wa maofisa wa FBI nchini humo, imebaini kuwa dereva wa Cyber Truck iliyolipuka Jumatano Januari Mosi 2025, nje ya hoteli hiyo Jijini Las Vegas alikuwa akisumbuliwa na tatizo la afya ya akili yaani ‘Post-traumatic stress disorder (PTSD).
Livelsberger, ambaye ni mwanajeshi wa Jeshi la Marekani katika kambi iliyoko Corolado, alikutwa akiwa amefariki ndani ya gari hiyo huku akitajwa kuwa na mgogoro binafsi uliokuwa ukimsumbua.
Polisi pia ilisema taarifa zilizochotwa kwenye simu ya Livelsberger, zimeonesha mtitiriko wa notisi alizokuwa akiandika mwanajeshi huyo mwenye umri wa miaka 37, akidai kuwa changamoto hiyo ameipata alipokuwa katika shughuli za kijeshi.
Mabaki ya mwili wake yalikutwa ndani ya gari hiyo ya Tesla, ambayo ililipuka. Taarifa hiyo pia ilibaini kuwa kulikuwa na madumu ya mafuta na mabaruti ndani ya gari hiyo ambayo yalichangia mlipuko huo.
Utambulisho wa Livelsberger ulibainika kupitia sampuni zilizofanyiwa kipimo cha Vinasaba (DNA) kilichochukuliwaa na mamlaka nchini humo.
Polisi pia wamesema mwili wake unaonekana kuwa na jeraha linalodhaniwa kuwa la risasi.
Maofisa hao wamesema baada ya kupitia notisi iliyoandikwa na kuhifadhiwa kwenye simu yake, Livelsberger aliandika kuwa tukio hilo halina uhusiano wowote na ugaidi ila suala linalopaswa kupewa uzito.
Livelsberger alikuwa ni Ofisa wa cheo cha sajini wa jeshi la nchi hiyo ambaye akihudumu nchini Ujerumani, hata hivyo alipaswa na mkasa huo alipokuwa likizo nchini humo.
Baba yake mzazi, aliieleza CBS News kuwa kijana wake alikwenda jijini Colorado kumtembelea mke wake na binti yake mwenye umri waa miezi nane. Alisema mara ya mwisho kuzungumza naye ilikuwa kwenye Sikukuu ya Krismas.
Mtalaka wa mwanajeshi huyo, amelieleza The Washington Post kuwa mwanamme huyo aliwahi kupata jeraha kichwani katika moja ya kazi alizowahi kutumwa kwenda kufanya nje ya nchi.
Alicia Arritt, (39) ambaye ni Muuguzi, aliyewahi kuwa na mahusiano na Livelsberger kati ya 2018 hadi 2021, anasema mwanajeshi huyo aliwahi kumtamkia kuwa anasumbuluwa na tatizo ya afya ya akili huku akisema anajutia baadhi ya matendo aliyowahi kuyafanya kwenye uwanja wa vita.
Tovuti ya Daily Beast imeripoti kuwa mwanajeshi huyo alikuwa mfuasi mkubwa wa Rais Mteule wa taifa hilo, Donald Trump. Ofisa wa Juu ndani ya jeshi hilo alipozungumza na familia yake aliieleza kuwa Livelsberger alimpigia kura Trump.
Ufuatiliaji uliofanywa na polisi nchini humo ulibaini kuwa Livelsberger alikodi gari hiyo ya Tesla kupitia Aplikesheni inayoitwa Turo Desemba 28 mwaka huu na kuitumia kusafiri nayo kwa zaidi ya Kilometa 900 hadi Las Vegas kujitoa muhanga.
Pia alikodisha silaha mbili katika kipindi hicho, hata hivyo, Mkuu wa Polisi jijini Las Vegas, Kevin McMahill amesema hadi sasa hawajabaini chanzo cha mwajeshi huyo kwenda kujiua nje ya hoteli hiyo ya Trump.
McMahill pia alisema watu saba walipata majeraha kutokana na mlipuko huo, hata hivyo majeruhi hao wameshapatiwa matibabu na kuruhusiwa kutoka Hospitalini.
Imeandikwa na Mgongo Kaitira kwa msaada wa Mashirika.