Watano wafariki dunia Russia, Ukraine zikikoleza vita

Kiev. Takriban watu watano wamefariki dunia katika majibizano ya makombora kati ya vikosi vya Russia na Ukraine, Ijumaa Januari 3, 2025.

Miongoni mwa mashambulizi yaliyosababisha vifo hivyo ni shambulizi la kombora la Russia katika Jiji la Chernigiv nchini Ukraine.

Tovuti ya The Guardian imeripoti kuwa kombora hilo lilirushwa na kupiga eneo la makazi na kusababisha kifo cha mtu mmoja huku kadhaa wakijeruhiwa.

“Nyumba kadhaa zilijaribiwa vibaya kutokana na shambulizi hilo, pia kuna majeruhi,” alisema Gavana wa Jiji la Chernigiv, Vyacheslav Chaus.

Gavana huyo alisema operesheni ya kutafuta walionasa kwenye vifusi na majeruhi inaendelea. Kombora hilo lilipiga katikati mwa jiji hilo lililoko takriban kilometa 75 kutoka ulipo mpaka wa Russia na Ukraine.

Gavana huyo alisema taarifa za awali zinaonyesha watu wanne walijeruhiwa kutokana na shambulizi hilo.

Katika shambulizi lingine, mabomu yaliyotegwa na vikosi vya Russia yamesababisha kifo cha dereva wa lori karibu na Jiji la Kyiv, huku bomu lingine lililotegwa likimuua mzee mstaafu Kusini mwa Mkoa wa Zaporizhia nchini humo.

Wakati huohuo, watu wanne wamejeruhiwa katika mlipuko wa mabomu katika mji wa Sloviansk karibu na ilipo kambi ya kijeshi ya Ukraine inayopambana kuurejesha Mkoa wa Donetsk.

Rais wa Ukraine, Volodymyr Zelenskyy, akizungumza kupitia mtandao wa Telegram, alisema katika siku tatu za Januari 2025, Russia imetekeleza mashambulizi ya kutumia droni zaidi ya 300 kwenye maeneo mbalimbali nchini Ukraine.

Hata hivyo, Zelenskyy alisema mashambulizi mengi yaliyodhibitiwa na mifumo ya kujilinda iliyosimikwa nchini Ukraine kwa kulipuliwa ama kuzuiwa kulipuka.

Kwa upande mwingine, mashambulizi ya Ukraine mpakani mwa Russia yamesababisha vifo vya watu wawili. Kifo kimoja kati ya vifo hivyo kimetokea katika kijiji kilichopo Mkoa wa Bryansk, nchini Russia.

Shambulizi lingine lililosababisha kifo nchini Russia, limetokea katika Mkoa wa Kursk nchini Russia ambapo raia aliyekuwa akitembea aliuawa kwa kushambuliwa na droni iliyorushwa na vikosi vya Ukraine jana Januari 3, 2025.

Moscow na Kyiv zimeendeleza mashambulizi ya anga katika siku tatu za mwanzo wa mwaka 2025, katika kipindi ambacho kila upande unapambana kuvutia kwake uongozi unaotarajia kuingia madarakani nchini Marekani.

Uongozi wa Rais mteule wa Marekani, Donald Trump unatarajia kuingia madarakani Januari 20, 2025 huku mtangulizi wake, Rais Joe Biden akitangaza kupeleka msaada wa mwisho wa silaha nchini Ukraine.

Uamuzi wa kupeleka misaada hiyo ya kijeshi na silaha ulitangazwa na Msemaji wa Ikulu ya taifa hilo, John Kirby, jana, Ijumaa.

Kirby alisema msaada huo utakaopelekwa (bila kutaja aina ya msaada huo) utagharimu zaidi ya Dola za Marekani bilioni 5.9 (Sh12 trilioni) na kusema kikao cha kikao cha mwisho kati ya pande hizo kitafanyika Januari 9, mwaka huu nchini Ujerumani.

Katika hatua nyingine, inaelezwa kuwa makali ya kukoma kwa mkataba wa usambazaji wa gesi asilia kutoka nchini Russia yameanza kung’ata huko nchini Moldova baada ya taifa hilo kuanzisha mgawo wa umeme.

Ukraine iligomea kufufuliwa kwa mkataba huo wa bomba la gesi lililokuwa likissafirisha gesi asilia kutoka nchini Russia kwenda barani Ulaya kwa bei nafuu kupitia Ukraine jambo ambalo limeanza kusababisha madhara kwa mataifa ya ulaya.

The Guardian imeripoti kuwa tayari wananchi nchini Moldova wameanza kukosa huduma za msingi ikiwemo nishati ya kupasha nyumba na kuchemshia maji kuanzia Jumatano Januari Mosi mwaka huu.

“Katika Mji wa Transnistria leo (jana) siku ya tatu ya Januari, kutakuwa na giza kutokana na mgawo wa umeme. Hiyo ni kwa sababu wakazi wake wanatumia kiasi kikubwa cha nishati inayozalishwa na gesi kuliko uwezo wa kuzalisha wa Moldova,” iliandika Wizara ya Nishati ya Moldova kupitia akaunti ya Telegram.

Wizara hiyo pia iliandika kuwa miongoni mwa maeneo mengine yatakayoguswa na mgawo huo ni Jiji la Tiraspol, baadhi ya wodi za wazazi, miji na vijiji vilivyoko katika jiji hilo.

Imeandikwa na Mgongo Kaitira kwa msaada wa Mashirika.

Related Posts