Straika Coastal Union atwishwa zigo

KOCHA wa Coastal Union, Juma Mwambusi amesema mshambuliaji mpya wa kikosi hicho raia wa Mali, Amara Bagayoko atakuwa na msimu bora ndani ya timu hiyo kutokana na uwezo alionao, licha ya kutopata muda mwingi wa kucheza kikosini.

Nyota huyo ametambulishwa katika dirisha hili dogo la usajili, japokuwa Mwanaspoti linatambua Bagayoko alikuwa na timu hiyo tangu msimu huu umeanza, ingawa viongozi wa kikosi hicho walikuwa bado hawajakamilisha taratibu zote za vibali ili kuanza kumtumia.

“Ni mchezaji mzuri ambaye naamini ataleta mageuzi makubwa ndani ya kikosi chetu, kadri anavyozidi kucheza na kuzoeana na wenzake ndivyo anavyojitengenezea hali ya kujiamini, kwa sababu bado ni mgeni na Ligi ya Tanzania hajaizoea,” alisema.

Mshambuliaji huyo msimu uliopita akiwa na ASKO de Kara, alikuwa mfungaji bora wa Ligi ya Togo baada ya kufunga jumla ya mabao 19, huku akichezea timu mbalimbali za FC Nouadhibou ya Mauritania, Al-Hala SC ya Bahrain na Djoliba AC ya Mali.

Bagayoko ni miongoni mwa washambuliaji waliopendekezwa na aliyekuwa kocha wa timu hiyo, Mkenya David Ouma aliyevutiwa na uwezo wake hivyo kuwataka mabosi kumsajili, ingawa licha ya kutua tu nchini mapema ila hakuweza kukichezea kikosi hicho.

Tayari nyota huyo ameonyesha matumaini baada ya kucheza mchezo wake wa kwanza wa Ligi Kuu Bara Desemba 29, mwaka jana, ambao Coastal ililazimishwa sare ya kufungana bao 1-1, dhidi ya KMC, mechi iliyopigwa Sheikh Amri Abeid jijini Arusha.

Related Posts